Makala Ya Wazi: Jitihada Endelevu Za Kidikteta

Msamawa Wa Jiwe Kwa Watuhumiwa Uhujumu wa Uchumi, Kioja Kuhusu Tishio La Ebola

Leo, Mahakama Kuu ya hapa Uingereza imetoa hukumu dhidi ya hatua ya Waziri Mkuu Boris Johnson "kulipeleka Bunge likizo" hadi Oktoba 14 mwaka huu. Katika hukumu hiyo, Mahakama Kuu chini ya Rais wake Lady Hale imeona kuwa hatua hiyo ya Waziri Mkuu Johnson sio halali.

Katika utetezi wake wakati wa kesi hiyo, mawakili wa serikali walitoa hoja kuwa kesi hiyo haipaswi kusikilizwa na mahakama hiyo kwa sababu inaingilia mhimili mwingine wa dola. Hata hivyo, mahakama hiyo ikasimamia wajibu wake wa kutafsiri sheria, na imetekeleza waibu huo kwa umahiri mkubwa.

Kuna funzo muhimu kwa Tanzania yetu kuhusiana na tukio hili. Naam, Tanzania sio Uingereza, lakini licha ya kuwa nasi tuna mahakama, bunge na serikali kama ilivyo Uingereza, lakini pia katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia jitihada za makusudi za kuondoa umuhimu wa bunge – aidha kupitia jitihada endelevu za Jiwe au kutokana na udhaifu wa Spika wa Bunge Ndugai anayelindwa na wingi wa wabunge wa CCM ambao nao ni completely useless kila linapokuja suala la kulinda hadhi ya bunge – sambamba na kuingilia uhuru wa mahakama.

Serikali ya Magufuli imekuwa mahiri katika kupuuza wajibu wa Bunge ambapo kwa upande mmoja imekuwa ikifanya maamuzi kadhaa bila kuhitaji baraka za Bunge na kwa upande mwingine maamuzi ya Bunge kama vile mafungu mengi ya fedha yanayotolewa kwa ajili ya matumizi ya serikali yamekuwa yakitumiwa visivyo na serikali. Sambamba na hilo, serikali ya Jiwe imekuwa mahiri wa kufanya matumizi ya fedha za umma bila kuhitaji idhini ya Bunge.

Na juzi tumemsikia Jiwe akitoa maagizo ambayo yanazidi kuifanya hali tete kuwa mbaya zaidi, ambapo amemwelekeza Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai (DPP) kuwezesha watuhumiwa wa kesi za uhujumu uchumi kuomba msamaha na kulipa fedha WANAZOTUHUMIWA kuhujumu, na hatimaye waachiwe huru.

Ni muhumu kutambua kuwa suala hili linawahusu WATUHUMIWA, kwa maana kwamba mahakama haijawatia hatiani – na wanabaki kuwa WATUHUMIWA tu japo sheria mbovu zinamaanisha waendelee kuwa jela wakati serikali inaendelea na upelelezi.

Katika mazingira ya kawaida tu, kila MTUHUMIWA -awe alifanya kosa analotuhumiwa au hakufanya – anatamani kuwa huru, na hiyo ina maana kuwa takriban KILA MTUHUMIWA ataomba msamaha ili awe huru hata kama hakufanya kosa husika.

Na hapo tunaweza kushuhudia WATUHUMIWA wenye uwezo wa kifedha (pengine ndizo walizohujumu) wakiomba msamaha na kuachiwa huru ilhali WATUHUMIWA wasio na uwezo wa kifedha wakiendelea kuozea rumande kwa vile hawawezi kumudu sharti hilo la "kutoa rushwa kwa serikali ili waachiwe."

Kwa bahati mbaya – au pengine makusudi – uamuzi huo mbovu kabisa unaonekana kukubaliwa na Watanzania licha ya baadhi yao kulalamika hapa na pale lakini bila kuchukua hatua makusudi.

Moja ya makundi muhimu katika jamii – wanasheria wetu – wamekuwa wanaharakati zaidi kuliko wataalamu wanaiweza kutumia utaalamu wao kuwatumikia wananchi kwa kupambana na maamuzi mabovu kama hayo ya Jiwe majuzi.

Kwa upande mwingine, yayumkinika kuhisi kuwa uamuzi huo wa Jiwe umetokana na vitu vitatu hivi

a)   Kuwakamua fedha watuhumiwa wa kesi za uhujumu uchumi ikiwa ni pamoja na waliobambikiwa kesi hizo.

b)   Kuwatoa rumande watuhumiwa waliobambikiziwa kesi lakini kwa kigezo cha "msamaha baada ya kukiri makosa yao" badala ya haki zao kisheria.

c)   Jitihada endelevu za Jiwe kuwa dikteta kamili.

Nihitimishe mada hii kwa kuwakumbusha Watanzania wenzangu kuwa hakuna malaika wa kuja kumzuwia Jiwe kuwa dikteta kamili. Watu pekee wanaoweza kupambana na jitihada hizo zinazoshika kasi kila kukicha ni Watanzania wenyewe.

Mada nyingine inayohusiana na mwenendo wa serikali ya Jiwe ni jinsi seriali yake inavyofanyia mzaha taarifa za uwepo wa EBOLA nchini Tanzania. Taarifa kutoka shirika la afya duniani WHO zimeilaumu serikali ya Jiwe kwa kugoma kutoa ushirikiano kwa shirika hilo kuchunguza kifo kimoja kinachodaiwa kusababishwa na EBOLA.

Tatizo kubwa la awamu hii ya Jiwe ni kulazimisha habari nzuri hata pale ambapo kuwa wakweli na kukiri habari mbaya kuna manufaa zaidi. Tumeshuhudia serikali hii ikiwalaumu "mabeberu" wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani wakieleza ukweli kuhusu mwenendo wa uchumi wetu, na kupingana na taarifa mbalimbali za kitaalamu zinazotafsiriwa na serikali hiyo kuwa "zinaichafua."

Again, hizi ni ishara za wazi za utawala wa kidikteta ambao ndio unakuwa na mamlaka kuu kuhusu kila jambo ikiwa ni pamoja na kupindisha ukweli, sheria, nk kwa minajili ya kuimarisha nafasi yake.

TANGAZO

  1. Pata nakala zako leo

  2. Unaweza kujiunga uanachama wa #BaruaYaChahali yenye vijarida vitano kwa wiki, kwa fursa ya kujiunga muda wowote ule utapojiskia, KWA KUBONYEZA HAPA (na kama unakerwa kutumiwa baruapepe kutoka kwangu,BONYEZA HAPA KUJIONDOA)

Ndimi mtumishi wako,

Evarist Chahali