Makala Ya Wazi: #ChahaliNaTeknolojia Ishara Za Akaunti Feki Twitter

Karibu katika makala hii ya wazi ya kijarida cha #ChahaliNaTeknolojia ambacho ni moja ya vijarida vitano vinavyounda #BaruaYaChahali.

Mada hii inawahusu watumiaji wa mtandao wa kijamii wa Twitter, ambao pamoja na uwepo wa watu wengi wazuri, kuna idadi kubwa tu ya akaunti feki.

Kuna aina mbalimbali za akaunti feki huko Twitter lakini katika makala hii nitajikita kwenye aina moja tu: akaunti feki inayotumia jina na picha ya binti/mwanamke.

Niende moja kwa moja kwenye dalili za kuwa akaunti husika ni feki. Ya kwanza kabisa ipo kwenye wasifu (bio). Mara nyingi akaunti feki za Twitter zonazotumia jina+picha feki huwa na wasifu ambao “ukiuangalia mara mbili mbili, unaweza kuona una walakini.”

Na kitu muhimu kabisa kwenye akaunti feki ni picha. Kama una utaalam kidogo kuhusu jinsi ya kuhakiki picha kwenye Google (yaani Google image search) basi ukiingiza profile picture ya akaunti husika itakuonyesha asili ya picha anayetumia mwenye akaunti feki.

Mara nyngi akaunti feki za “Twitter ya Tanzania” hupendelea kutumia picha za mabinti warembo wa Afrika Kusini, na mara nyingi “huziiba” picha hizo huko Instagram.

Cha kufanya, pakua picha husika kisha nenda HAPA halafu ingiza picha husika, utaweza kujiridhisha kuhusu endapo picha hiyo ni halisi au feki. Kama ni feki basi akaunti husika nayo ni feki pia.

Njia ya pili ambayo pengine ni rahisi zaidi ni kuchunguza “followers” na watu ambao mhusika anawafolo. Takriban mara zote, mtu mwenye akaunti feki huwa anaifolo akaunti yake/zake halisi.

Watu anawafolo (following) ni muhimu zaidi ya wanaomfolo. Na katika hili, ishara muhimu ni aina ya hizo akaunti anazozifolo. Moja ya ishara za wazi ni kwa mhusika ku-folo akaunti zenye “picha ya yai la Twitter.”

Katika mazingira ya kawaida tu, hutarajii “binti mrembo” afanye kuifolo akaunti yenye picha ya yai.

Dalili nyingine ni “picha za kutatanisha.” Kumbuka lengo la mtu husika kufungua akaunti hiyo ni kuwazuga watu kwa sababu maalum. Kwa vile katika Twitter, idadi ya wanaume ni kubwa zaidi kuliko wanawake, basi “picha za kutatanisha” hupelekea akaunti husika kufanikiwa kupata followers kwa kasi.

Sambamba na picha hizo ni jitihada za kusaka attention aidha kwa kutumia hizo picha au kutwiti vitu ambavyo ni rahisi kuwavutia “watu ambao akili yao ipo sehemu za siri.”

Nimalizie makala hii kwa kukupa hamasa ya kwenda “kufanya ushushushu” leo au siku yoyote ile kwa kuzingatia mbinu hizo nilizokupa hapo juu.

Mwisho ni tangazo la vitabu hivi viwili kwa wanaovihitaji.

Ndimi mtumishi wako,

Evarist Chahali