Makala Ya Wazi: #BaruaYaShushushu Wazalendo (kama mpo) TISS Mjifunze Kinachoendelea Marekani

Kwenda Kinyume na Sheria/Kanuni Ili Kuinusuru Nchi Ni Uzalendo Uliotukuka

Karibu katika makala ya wazi ya toleo la wiki hii la kijarida cha #BaruaYaShushushu ambacho hutumwa Ijumaa kwa wanachama wa #BaruaYaChahali yenye mkusanyiko wa vijarida vitano kwa wiki.

Unaweza kujiunga uanachama  KWA KUBONYEZA HAPA (na kama unakerwa kutumiwa baruapepe kutoka kwangu,BONYEZA HAPA KUJIONDOA)

Twende kwenye mada. Jana, kaimu Mkuu wa taasisi mama ya taasisi za ushushushu za Marekani (Director of National Intelligence - DNI) Joseph Maguire alihojiwa na Kamati ya Usalama ya Seneti ya nchi hiyo, kuhusiana na taarifa iliyovujishwa na shushushu mmoja kuhusu vitendo kadhaa vya Rais Donald Trump ambavyo vinatafsiriwa kama kuhatarisha usalama wa taifa hilo.

Marekani ina “idara za usalama wa taifa” 16 ambazo kwa pamoja hufahamika kama “jumuiya ya intelijensia” (intelligence community), na DNI ndiye mkuu wa “jumuiya” hiyo.

Sasa wenzetu hawa licha ya shughuli zao za ushushushu kufanyika kwa usiri, taasisi hizo na viongozi wake wanawajibika kutoa maelezo kwenye Kamati za mabunge mawili ya nchi hiyo. Na ndio kilichotokea jana.

Bwana Maguire aliitwa kuhojiwa kuhusu suala hilo la huyo “mvujisha siri” (whistleblower). Na katika maelezo yake, kiongozi huyo alisema kuwa kitengo kilichifanywa na shushushu husika ni cha kijasiri na cha kizalendo.

Kwa mujibu wa taratibu, maafisa mbalimbali wa taasisi hizo 16 za nchi hiyo hupangiwa majukumu ya kikazi katika Ikulu ya nchi hiyo. Na shushushu aliyevujisha siri alipata fursa ya kufahamu siri hizo wakati alipokuwa kwenye “zamu” Ikulu ya nchi hiyo.

Lakini kwa vile wenzetu wanaweka mbele maslahi ya nchi kuliko ya Rais au chama chake, shushushu huyo alipofahamu kuwa kuna mambo yanayofanywa na Rais Trump yanayoweza kuhatarisha usalama wa nchi hiyo, akalazimika kutoa taarifa.

Tayari sakata hilo limepelekea chama pinzani cha Democrats kuanzisha mchakato wa kumng'oa Trump madarakani (impeachment).

Wakati nafuatilia suala hilo nilikuwa najiukiza kimoyomoyo, hivi kweli katika Idara yetu ya Usalama wa Taifa hakuna kabisa watu wenye uchungu na nchi yetu kiasi cha kujitoa mhanga kuvujisha siri ili kulinusuru taifa letu?

Naelewa kuwa tofauti na wenzetu wa Marekani ambao wana kitu kinaitwa “oversight” yaani mfumo wa uangalizi/usimamizi iwe kwa taasisi za ushushushu au taasisi nyingine kama vile nafasi ya urais, nk lakini sie tumejaliwa ubabaishaji, ukiritimba, nk.

Hata hivyo kuna sie ambao nina hakika mkitupatia mnayoyajua tutawawezesha kufanya kama alichofanya huyo “whistleblower” wa Marekani.

Je ni mangapi mnashuhudia na mnafahamu kabisa kwamba sio tu hayapo sahihi lakini pia yanahatarisha mustakabali wa Tanzania yetu? Ndio kanuni zinakataza kutoa siri za ofisi lakini kipi bora kwenu: kuzingatia taratibu, sheria na kanuni huku nchi inaangamia au kukiuka sheria, taratibu na kanuni kisha kuinusuru nchi yetu?

Najua takriban nyote mmezibwa macho na marupurupu makubwa kabisa mnayopewa bila kusahau OP na posho za “operesheni hewa.” Ni rahisi katika mazingira hayo kusema “ah kwanini nihatarishe ajira yangu na maslahi yote haya?” Siwezi kuwalaumu wala kuwashawishi vinginevyo ila tu ninawasihi mkumbuke kuwa mustakabali wa Tanzania yetu upo mikoani mwenu.

Nimalizie kwa kutanabaisha kuwa simhamasishi mtu kuvunja sheria au kukiuka kanuni, taratibu na sheria bali nataka kuibua mwamko wa kutambua kuwa sio kila jambo sahihi ni zuri kama ambavyo sio kila jambo zuri ni sahihi. Kuzingatia kanuni, taratibu na sheria (huku nchi inaangamia) ni kitu sahihi lakini sio kizuri, ilhali kuvujisha siri (zitakazosalimisha taifa letu) sio kitu sahihi lakini ni kizuri.

Mwisho ni tangazo la vitabu vyangu hivi viwili na panapo majaliwa tarehe mosi Oktoba nitachapisha kijitabu kuhusu ishu ya Kipilimba kutimuliwa kazi.

Ndimi jasusi wako,

Evarist Chahali