Magufuli na Siasa Za Chuki: Atavuna Anachopanda

Ukipanda Maputo (Balloons) Ardhini Hutovuna Magimbi Bali Maputo. Ukipanda Chuki Hutovuna Upendo Bali Chuki

Moja ya masuala yanayotikisa katika anga za habari huko nyumbani na huku Ughaibuni ni ziara za Bwana Tundu Lissu katika nchi mbalimbali. Tayari ametembelea hapa Uingereza ambapo mahojiano mawili aliyofanyiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) yanamnyima raha Magufuli na majahili wenzake.

Kwanza Lissu alihojiwa na Zuhura Yunus wa Dira ya Dunia ya Idhaa ya Kiswahili ya BBC

Baadaye, Lissu alihojiwa na Steven Sackur wa kipindi maarufu cha Hard Talk.

Kwa tathmini yangu, Lissu alifanya vema zaidi kwenye mahojiano na Zuhura kuliko kwenye Hard Talk. Nilihitimisha hivyo kwa sababu, wakati katika mahojiano na Zuhura, Lissu alifanikiwa kujenga hoja zake na kuzitetea zilivyo - pengine kwa vile muda ulikuwa mfupi - katika Hard Talk, kuna nyakati “alisuasua” kidogo, pengine kutokana na urefu wa mahojiano, sambamba na asili ya kipindi cha Hard Talk ambapo mhojiwa huwekwa kiti moto.

Hata hivyo, mahojiano yote hayo yalirudia kuonyesha kitu ambacho wengi wenu mnakipuuza: Tanzania ipo katika utawala wa kidikteta ambao unatisha watu, unateka watu na unaua watu. Lissu alipaswa kuwa marehemu muda huu, lakini kwa vile Mungu sio Jiwe, sio tu Lissu yupo hai bali bado ni mwiba mchungu kwa Magufuli.

Kabla ya kwenda mbali zaidi, ni vema nikatanabaisha kuwa mie sio shabiki wa Lissu wala chama chake cha Chadema. Mie, kama Lissu, ni mhanga wa siasa za chuki, ukatili, ujahili na mauaji (ninaweza bila shaka yoyote kujitambulisha kama Mtanzania ambaye nimenusurika majaribio mengi mno ya kuuawa kuliko yeyote yule. Na hadi muda huu, Magufuli na majahili wenzie wanahangaika kutafuta mbinu za kunidhuru.)

Nii rahisi kuliangalia suala la Lissu kama “janga lake binafsi” lakini ukweli ni kwamba kwa muda mrefu, Tanzania yetu imekuwa ikisherehesha matumizi ya vitisho/mateso/mauaji kama nyenzo ya kulazimisha matakwa ya watawala. Unaweza kusoma

SOMA HAPA: Mtazamo Wangu Kuhusu Mauaji Ya Kisiasa Tanzania

Na moja ya sababu za kudumu kwa utamaduni ni “ukondoo” wa Watanzania. Ukisoma makala yangu hiyo utabaini kuwa Watanzania wengi tu wameuawa kwa sababu za kisiasa lakini mamilioni ya Watanzania walionusurika kutouawa hawana muda na janga hili lililodumu muda mrefu sasa. Muda huu tunaoongea, Lissu angeweza kuwa amesahaulika kama Watanzania walivyomsahau Marehemu Akwilina, Marehemu Diwani Luena na Katibu Kata ya Hananasifu (Chadema) Marehemu Daniel.

Laiti Watanzania wangekataa kuafikiana na Mkapa pale serikali yake ilipouwa Wazanzibari kadhaa mwaka 2001 basi huenda watangulizi wake wangehofia kutumia mauaji kama silaha ya kisiasa.

SOMA: Mauaji Ya Kutisha Zanzibar Mwaka 2001 Kufuatia Uchaguzi Mkuu

Naam, “ukondoo” wa Watanzania ndio umeifikisha nchi yetu mahala ambapo Jiwe anaendeleza unyama “ulioruhusiwa na Watanzania kwa watawala wao.”

Turejee kwenye suala la Lissu. Nimetanabaisha awali kuwa mie sio shabiki wa Lissu wala Chadema. In fact, mie sina ushabiki kwa wanasiasa au vyama vyao. Kipaumbele changu ni Tanzania yetu.

Lakini pia hata kama ningekuwa nafanya ushabiki kwa wanasiasa/vyama vyao, ningepata tatizo kidogo kwa Lissu. Kama kuna mapungufu katika mwanasiasa huyo mahiri basi ni “kutojichanganya.” Lissu ni mtu wa kutoa kauli na machapisho mbalimbali, ni mtu wa kutoa miongozo na ufafanuzi mbalimbali.Lakini Lissu si mtu wa kujichanganya na “watu wa kawaida” hususan huko kwenye mitandao ya kijamii, sehemu inayotoa fursa nzuri kwa wanasiasa/watu muhimu “kujichanganya” na kila mtu.

Pengine nitumie fursa hii kumshauri Lissu kwamba ili kutimiza ndoto zake za Urais mwaka 2020 basi ni muhimu kwake kuanza “kujichanganya” na watu mbalimbali. Natambua wanasheria wengi huwa na “dharau ya kisomi” (intellectual arrogance) lakini kwa mtu mwenye nia ya kuwa Rais basi ni muhimu kujifunza kwa wanasiasa kama vile Zitto Kabwe “tunaojichanganya nao” kwenye mitandao ya kijamii.

Hata hivyo hii ni kasoro ndogo tu na huenda isiwe na athari zozote kwenye safari ya Urais ya mwanasiasa huyo ambaye uzalendo wake ni wa hali ya juu kabisa.

Turejee kwenye ziara za Lissu. Moja ya vitu vilivyonisikitisha mno - ukiweka kando ukweli kwamba kosa pekee la mwanasasa huyo hadi kutaka kuuawa ni chuki za kisiasa za Magufuli - ni stori kuhusu aliyekuwa Balozi wa Tanzania huo Ubelgiji, Joseph Sokione, ambaye aliondolewa kwenye wadhifa huo na Magufuli “kwa kosa la kumtembelea Lissu hospitalini.”

Swali ambalo wewe mwananchi wa kawaida unapaswa kujiuliza ni hili, IWAPO MTU MUHIMU KAMA LISSU ANAWEZA KUTENDEWA HAYA, VIPI KUHUSU MIE/MWENZANGU NA MIE?

Nimalizie toleo hili kwa kukuwekea video kadhaa zinazohusiana na ziara ya Lissu. Tukutane Jumatatu ijayo PANAPO MAJALIWA.