Magufuli, Chadema Na Mauaji Ya Kisiasa

Imefika Mahala Mauaji Ya Kisiasa Yamezoeleka, Hadi Yanapuuzwa.

Kabla ya kuingia kwenye mada ya wiki hii ningependa kutumia fursa hii kuwashukuru wasomaji 28 mliojitolea kuchangia kijarida hiki ambacho sasa kinajumuisha vijarida vitano kwa wiki.

Pengine watu 28 sio wengi hasa ikizingatiwa kuwa jumla ya mliojisajili kupokea #BaruaYaChahali ni takriban watu 2,000. Hata hivyo, jana nililazimika kuwaondoa takriban subscribers 800 ambao hawajawahi kufungua emails 10 na zaidi ninazotuma kwenu.

Napata shida sana kuelewa kwanini mtu ajisajili kupokea kijarida ambacho hana mpango wa kukisoma.

Kwa upande wa mabadiliko ya muundo wa kijarida hiki ambapo sasa ninawatumia vijarida vitano kwa wiki, na nilitoa rai kwa wasomaji kujisali upya, na baada ya usajili watoe mchango kidogo wa sh 50,000 kwa mwaka au sh 5,000 kwa mwezi, waliojitokeza ndio hao 28 hadi sasa. Ninawashukuru kwa sababu endapo hiyo ndio itakuwa idadi kamili hadi kufikia Juni 30 mwaka huu nitakapofunga usajili, basi sina tatizo kuwatumikia hao 28 kwa sababu nadhani hawa ndio haswa wenye uhitaji wa dhati wa kutumikiwa nami.

Jumla ya waliojisajili kuwa wapo tayari kuchangia malipo yako kidogo ni takriban watu 300 lakini again, walioona umuhimu wa kutekeleza ahadi zao ni hao 28 tu. Kwa hakika kuwatumikia Watanzania kwataka moyo.

Anyway, nihitimishe utangulizi huu kwa kurudia tena kutanabaisha kuwa wazo la kuchangia malipo kidogo halikulenga kupata fedha/faida bali kuboresha utumishi wangu kwenu. Atakayejiskia kuungana na hao 28 anakaribishwa. Utaratibu wa jinsi ya kuchangia ni huo pichani

Twende kwenye mada ya wiki hii. Wiki iliyopita, wa mara nyingine tena, mwanasiasa mmoja wa upinzani aliuawa kwa kupigwa risasi.

Nami mtumishi wako nikaripoti

Na kustaabishwa na ukimya wa Chadema

Na mdau mmoja akaenda mbali zaidi

Mimi mtumishi wako nimekuwa nikifuatilia suala la mauaji ya kisiasa kwa muda mrefu. Niliwahi kufanya uchambuzi wa kina katika MAKALA HII

Kwa upande mmoja, yayumkinika kuhitimisha kuwa kuuawa kwa kiongozi huyo wa Chadema sio tu ni mwendelezo wa mauaji ya kisiasa yanayoshamiri katika Awamu hii ya Rais Magufuli bali pia ni matokeo ya siasa za chuki zinazohubiriwa mara kwa mara na kiongozi huyo.

Kwa upande mwingine, Chadema imezidi kuonyesha udhaifu wake katika kutetea haki za viongozi na wanachama wake mbalimbali ambao aidha wameuawa, wamtupwa jela au wamedhuriwa na serikali ya Magufuli.

Mifano ni mingi, lakini ukimywa wa chama hicho kuhusu “kupotea” kwa kada wake Ben Saanane, ukimywa wake kufuatia kuuawa viongozi wake Diwani Luena na Katibu Kata ya Hananasifu Daniel, na jaribio la kuuawa Tundu Lissu, kifungo cha uonevu kwa Sugu, Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho Mbowe na mbunge Matiko kuwekwa ndani miezi…yote hayo yamejiri mchana kweupe pasi shinikizo lolote kutoka kwa Chadema kudai haki itendeke.

I am really disappointed with mwelekeo wa chama hicho kikuu cha upinzani. Tangu kilipofanya “kosa la karne” kumpokea Lowassa (na kutulazimisha baadhi ya akina sie tuliokuwa tunakiunga mkono tujiweke kando nacho), chama hicho kimekuwa kipo kipo tu.

Na kwa hakika kinapaswa kumshukuru Magufuli kwa kuzuwia shughuli za vyama vya upinzani, kwa sababu kinyume cha hivyo, udhaifu wa Chadema ungebainika waziwazi. Tangu kilipolazimika kutelekeza ajenda yake kuu ya vita dhidi ya ufisadi (ili kisimuudhi mtu ambaye chama hicho tangu 2006 hadi 2015 kilikuwa kinamuita baba la ufisadi, yaani Lowassa) chama hicho hakina ajenda zaidi ya kudandia hoja.

Chadema inaonekana kama ipo usingizini na inatarajia kuwa ikiamka itakutana na muujiza ambapo ghafla Magufuli anaamua kutoa haki stahili kwa wapinzani kama zawadi vile.

Lakini Marehemu Profesa Kighoma Ali Malima alishawahi kutuusia kuhusu upatikanaji wa haki, kama inavyoonekana kwenye nukuu hii ya kitambo ya mtumishi wako huko Twitter

Hivi katika mazingir yaliyopo, nini hasa cha kum-discourage Magufuli au #WatuWasiojulikana kumdhuru kiongozi mwingine wa Chadema? Nauliza hivyo kwa sababu kama yote yaliyojiri katika miaka minne hii ya utawala wa Magufuli dhidi ya Chadema hayajapelekea hatua yoyote kutoka kwa chama hicho, hatuwezi kumlaumu Magufuli akidhani kuwa Chadema wanafurahi ukatili anaowafanyia.

Kwa vile lawama hazijengi, ni muhimu kwa sisi kama taifa kukemea vitendo hivi ambavyo vinaweza kuliingiza taifa letu katika janga kubwa. Ikumbukwe tu, leo inaweza kuwa “Magufuli dhidi ya wapinzani.” Akishawamaliza wapinzani, atahamia kwa wengine. Na siku ya siku, wewe nawe utakuwa mhanga wa udikteta wake.

Najua baadhi ya wasomaji wangu ni wafuasi wa CCM. Mtaniwia radhi kama nawakwaza lakini Mwenyekiti wenu anaipeleka nchi kusikofaa. Na kwa hakika mna jukumu la kutuondolea mtu huyu kwa sababu nyie ndo mlimleta. This man is really bad news.

Nakutakia siku na wiki njema

Ndimi mtumishi wako,

Evarist Chahali