Magufuli Amefanikiwa Kumnunua Kiongozi Mmoja Muhimu wa Upinzani

Lakini Hiyo Sio Mada Yetu Ya Wiki Hii, Twaendelea na Ile Topic ya UKIMWI

Jana nilipata tip flani kutoka kwa chanzo kimoja cha kuminika 100 kwa 100. Tip hiyo ilikuja wakati ninajiuliza maswali kadhaa kuhusu mwanasiasa flani wa upinzani. Na kilichozua maswali hayo ni swali la dada yangu flani, aliyeuliza “vipi ‘naniliu’ mbona kimya?”

Enewei, jana nikapata jawabu kupitia kwa chanzo changu hicho. Ninachoweza kusema hapa ni kwamba vyama vyetu vya upinzani vina safari ndefu sana. Na sio tu safari ndefu kwa sababu mara nyingi kabla ya kufikia mafanikio inaweza kugharimu safari ndefu ya maisha, bali pia kumudu kukabiliana na ‘shetani’ akiwa katika sura ya faranga…ndjuluku…mapene…moolah…benjamins…namaanisha FEDHA…aka…HELA.

Yahitaji moyo kweli kwa mzalendo kuweza kumudu ushawishi wa fedha. Na sie Wakristo tunafahamu fika jinsi fedha ilivyomfanya Yuda kumsaliti Bwana Yesu. Na kwa huko nyumbani, miaka nenda miaka rudi mmekuwa mkishuhudia jinsi CCM inavyotumia umasikini wenu na kuwalaghai kwa fedha ambazo kimsingi chama hicho huwa kimewaibia.

Sasa katika kutekeleza azma yake ya kutawala milele, Magufuli amewekeza vya kutosha katika kununua wapinzani. Japo zoezi hilo lilitangazwa kuwa limefikia kikomo, ukweli ni kwamba linaendelea kimyakimya. Na kwa hakika “ununuzi” huu unaofanyika kimyakimya ni wa hatari zaidi kuliko ule wa wabunge na madiwani waliotangaza waziwazi “usaliti” wao.

Anyway, nisiongee mengi, nina hakika mtakuja kushuhudia wenyewe.Lakini pia mtu yeyote akijihangaisha vya kutosha kuelewa yanayojiri katika duru za siasa zetu, hatoshindwa kubaini ni mwanasiasa gani huyu ambaye Jiwe “kampandia bei.”

Naomba nimalizie sehemu ya mwisho ya mada niliyowaletea wiki iliyopita kuhusu Ukimwi, ambapo nilidokeza kwamba wanasayansi wamepiga hatua muhimu katika kusaka tiba ya ugonjwa huo.

Kwa kifupi, changamoto moja kubwa kwa wanasayansi kupambana na virusi vya ukimwi ni ukweli kwamba virusi hivyo “vinajua sana kuzuga.” Ninachomaanisha hapa ni kwamba virusi hivyo vinaweza “kulala” kwa miaka kadhaa wakati mwathirika anatumia ARVs, lakini huibuka kwa kasi mpya pindi akisitisha au kuacha matibabu.

Nakumbuka stori moja ya kusikitisha iliyotokea mwaka jana hapa ninapoishi ambapo dada mmoja wa Kizimbabwe aliyekuwa akitumia ARVs alipokutana na mchungaji mmoja wa Kizimbabwe pia aliyedai anatibu kila maradhi ikiwa ni pamoja na ukimwi. Dada huyo akaamini porojo za mchungaji huyo, akaacha kutumia ARVs, na jumapili moja akatoa ushuhuda kuwa amepona. Siku chache baadaye akaanza kuvuimba mwili kama puto na ndani ya wiki moja akafariki.

Kwahiyo licha ya ARVs kuwa na ufanisi mkubwa katika kuvidhibiti virusi vya ukimwi, bado hakuna dawa yenye uwezo wa kuviangamiza completely virusi hivyo.

Hata hivyo, jitihada za wanasayansi watafiti wa chuo kikuu cha Pittsburgh nchini Marekani wamefanikiwa kugundua tiba ya majaribio ambayo sio tu inavifurumusha virusi vya ukimwi mahala ambapo vimejificha baada ya “kushambuliwa” na RVs bali pia inaviuwa kabisa virusi hivyo.

Mkakati huo wa matibabu ya majaribio unaitwa “kick-and-kill” ambapo “tiba” huvishambulia virusi vya ukimwi (kama zinavyofanya ARVs) lakini inakwenda mbali zaidi na kuvingamiza virusi hivyo. Kwahiyo, pindi “tiba” hiyo ikithibitishwa baada ya majaribio mengine kadhaa, itawafaya waathirika wa ukimwi wanaotumia ARVs kumudu kuacha dawa hizo bila hofu ya virusi hivyo “kukurupuka” upya.

Kwa lugha ya kitaalamu zaidi, takriban asilimia 95 ya waathirika wa ukimwi husumbuliwa pia na virusi vinavyojulikana kama “Cytomegalovirus” kwa kifupi CMV. Hata hivyo, wakati njia ya kudhibiti virusi vya HIV vinavyosababisha ukimwi ni hizo dawa (ARVs), udhibiti dhidi ya CMV hufanywa na kinga ya asili ya mwili. Ni kinga hiyo iliyowapa wanasayansi hao watafiti wazo la kujaribu kuitumia dhidi ya HIV, na ikafanikiwa kuviangamiza virusi hivyo.

Nimalizie makala hii kwa kukumbushia kwamba moja ya sababu zinazoufanya ukimwi uendelee kuwa “tishio la kimyakimya” huko nyumbani ni pamoja na watu wengi kuogopa kwenda hospitali kufahamu kama wapo salama au wameathirika. Bila kujua kama unao au la, ni vigumu kushiriki katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu.

Rafiki yangu mmoja daktari ananiambia kuwa vitendo vya ngono kinyume cha maumbile vimeshamiri mno huko nyumbani, na vinachangia sana maambukizi ya ukimwi. Hili ni janga ambalo kwa bahati mbaya - au makusudi - watu wengi hawaliongelei.

Nakutakia siku na wiki njema. Tukutane tena Jumatatu ijayo

Ndimi mtumishi wako,

Evarist Chahali