Lowassa Kurudi CCM: Mtumishi Wako Nilibashiri Hilo Kitambo

Lowassa nje ya CCM ni kama samaki nje ya maji

Machi Mosi mwaka huu, siku moja baada ya kifo cha mmoja wa watu maarufu nchini Tanzania, Ruge Mutahaba, aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema/UKAWA katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Edward Lowassa alitangaza kurudi CCM.

Uamuzi huo wa Lowassa ulipokelewa kwa mshtuko mkubwa hasa kwa vile akili ya Watanzania wengi ilielekezwa kwenye msiba wa Ruge.

Hata hivyo, mie binafsi sikushangazwa na kitendo cha Lowassa kurudi CCM. Na miongoni mwa sababu za kutoshangazwa ni kwa vile nilikuwa Mtanzania pekee aliyebashiri tukio hilo.

Nimejenga tabia ya kubashiri matukio yajayo nchini mwetu, sio “kupora kipaji cha Marehemu Sheikh Yahya (RIP)”

bali kutumia vema uelewa wangu wa siasa za Tanzania. Na hata baada ya kutimia kwa ubashiri wangu kuhusu Lowassa, ninaendelea kuamini kuwa kuna tukio kubwa litakaloitikisha Tanzania hivi karibuni (pengine ni matukio na si tukio). Time will tell.

Back to ishu ya Lowassa na Chadema. Labda ukifuatilia mlolongo huu wa matukio unaweza kupata picha nzuri ya msimamo wa mie mtumishi wako katika suala hili kwa ujumal.

Kabla ya Julai 2015, nilikuwa miongoni mwa Watanzania waliokuwa wakiiunga mkono Chadema. Sio kama mwanachama bali nilikuwa naafikiana nao katika harakati zao za kisiasa hususan vita dhidi ya ufisadi. 

Lakini ghafla wakampokea Lowassa, mwanasiasa ambaye Chadema hao hao walimwandama kwa takriban miaka tisa mfululizo (tangu mwaka 2006 hadi 2015) wakimuita fisadi. 

Na wala sikutafakari mara mbili, nikaamua kuacha kuiunga mkono Chadema. Bahati nzuri Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt Slaa ambaye pia alikuwa mgombea urais mwaka 2010, nae aliamua kuachana na chama hicho. Niliandika HAYA kumpongeza,

Baadaye niliwananga Chadema na MAKALA HII


Na baada ya Chadema kulamba matapishi yao na kumkumbatia Lowassa, chama hicho kiligeuka kuwa "chama cha mtu mmoja" kama nilivyotanabaisha katika MAKALA HIINa the latest ni tahadhari niliyotoa baada ya Lowassa kukutana na Magufuli Ikulu mwaka jana, niliandika MAKALA HII ya kina.Sidhani kama Chadema wanahitaji kupewa pole kwa sababu kila aliyejaribu kuwatahadharisha kuhusu Lowassa aliishia kutukanwa. 

Uamuzi wa Lowassa kurejea CCM si jambo la kushangaza kwa sababu (a) alihama CCM kwa ajili tu ya kusaka urais huko Chadema (b) kwa kugombea urais kupitia Chadema, Lowassa aliweza kukihenyesha chama hicho kilichomuita fisadi huko nyuma, lakini kikalazimika kuzunguka nchi nzima kumsafisha Waziri Mkuu huyo wa zamani. 

Kwa kifupi, Chadema wamevuna walichopanda. Hatma ya chama hiki sasa itategemea sana jinsi kitakavyoweza kuhimili kipigo hiki kikubwa kabisa kwao. As it stands, kuna uwezekano mkubwa kabisa kwa chama hicho kutoambulia japo jimbo moja katika uchaguzi mkuu ujao, sio kwa kushindwa bali sio siri kuwa kuna wabunge kadhaa wa chama hicho wapo njiani kwenda CCM. 

Na liwalo na liwe, wabunge wawili wasiotarajiwa kabisa kuwa ipo siku wataikimbia Chadema - Kubenea na Bulaya - wapo njiani kwenda CCM. Na ninabashiri uwezekano wa lundo la wabunge na madiwani wa chama hicho kikuu cha upinzani kuhamia CCM “kumuunga mkono Lowassa.”

Kwa bahati mbaya, kama ambavyo imekuwa ikitokea mara kwa mara, kuna jitihada kubwa miongoni mwa viongozi na wafuasi wa Chadema kujihadaa kuwa kuondoka kwa Lowassa “sio big deal” na “maisha yanaendelea kama kawaida.” Wito wangu kwa chama hicho ni kukaa chini na kufanya tafakuri ya kina kuhusu kilipotoka, kilipo na kiendako.

Na pengine kuna haja kwa chama hicho kuendana na jina lake la CHAma cha DEMOKRASIA na MAendeleo. DEMOKRASIA ni pamoja na kufanya uchaguzi mkuu wa kupata viongozi wapya au kubariki kuendelea na viongozi wa zamani. Mwenyekiti wa taifa wa chama hicho Freeman Mbowe sio tu amekuwa madarakani muda mrefu mno lakini pia anapaswa kubebeshwa lawama katika usanii ambao chama hicho kimefanyiwa na Lowassa. Hoja kwamba Mbowe ana mchango mkubwa sana haina mashiko, kwani hata Nyerere alikuwa na mchango mkubwa sana kwa taifa lakini aling’atuka.

Nimalizie kwa kueleza hofu yangu kubwa kuhusu mustakabali wa siasa za upinzani nchini Tanzania. Kwa upande mmoja ni mazingira yasiyo rafiki kwa demokrasia ya vyama vingi - kwa mfano sheria mpya ya vyama vya siasa, upendeleo wa waziwazi wa taasisi za umma kwa CCM sambamba na kuvionea vyama vya upinzani, chuki ya wazi ya Jiwe dhidi ya Upinzani, nk. Kwa upande mwingine ni kasoro mbalimbali ndani ya vyama vya upinzani, ambazo baadhi zinafichika kutokana na uwepo wa “mbuzi wa kafara” yaani Jiwe/CCM, kwamba kila kinachojiri ndani ya upinzani, kisingizio huwa “Jiwe huyo” au “CCM hao.”

Nakutakia wiki njema, tukutane wiki ijayo