Lissu Amjibu Kigogo, Asema Ushauri CDM Waache Siasa Za Mtandaoni Ni 'Poisoned Advice,' Amwambia Ushauri CDM Ianzishe Jeshi Ni Wa Kijinga, Abainisha Kuwa Kigogo Hana Uzoefu Wa Kuendesha Chama Chochote

Ameandika Tundu Lissu kumjibu Kigogo

Vitu ambacho Kigogo hajasema:

👉1. ANC walihamisha Makao Makuu yake nje ya Afrika Kusini na viongozi wake kukimbilia uhamishoni mwaka 1960 baada ya ANC kupigwa marufuku. CHADEMA haijapigwa marufuku bado.

👉2. Ilikuwa rahisi kwa ANC kufungua ofisi na kuendesha shughuli zake nje ya Afrika Kusini kwa sababu utawala wa makaburu ulikuwa unapingwa na ulitengwa kimataifa, hata katika nchi za Ulaya Magharibi zilizokuwa washirika wakubwa wa kiuchumi wa utawala huo.

👉3. ANC na vyama vingine vya ukombozi - PAC, SACP, etc. - vilikaribishwa kuendesha shughuli zao kwenye nchi husika na serikali za nchi hizo.

👉4. Kufundisha watu mafunzo ya kijeshi kwa lengo la kuendesha vita vya kuiondoa CCM madarakani ni ushauri wa kijinga na wa hatari kubwa kwa CHADEMA. Katiba ya sasa na Sheria ya Vyama vya Siasa inakataza vyama kutumia mapambano kama njia ya kupata madaraka ya kisiasa. Ushauri huo utahalalisha hoja za maadui zetu za kuifuta CHADEMA kabisa.

👉5. Vyama vya ukombozi vya miaka ya '60, '70 na '80 vilifundishiwa wanajeshi wake na nchi rafiki za jirani na hata za nje ya Afrika, mfano Cuba, China, Urusi ya Kisoviet, etc. Vilianzisha kambi za kijeshi katika nchi jirani rafiki na zilipewa silaha na nchi hizo au nchi rafiki za nje. Mambo hayo hayawezekani tena kwa sababu zilizo wazi kwa yeyote anayetumia akili yake vizuri: mazingira ya sasa ya kimataifa ni tofauti kabisa na ya wakati huo.

👉6. CCM haijaanza kuwa chama dola jana au juzi. CCM ni chama dola tangu kuzaliwa kwake mwaka '77. TANU na ASP viliacha kuwa vyama vya siasa na kuwa vyama dola tangu mwaka '64/'65 tulipoingizwa kwenye mfumo wa chama kimoja cha siasa. Msomeni Pius Msekwa (Towards Party Supremacy, '77), na Issa Shivji (The State and the Working People in Tanzania, '85) kwa ufafanuzi wa hoja hii.

👉7. CHADEMA imeanzia kwenda kwenye 'grassroots' (i.e. CHADEMA ni Msingi) tangu Magufuli alipoanzisha vita dhidi ya demokrasia mwaka '16. Hata 'CHADEMA Kidigitali' imeelekezwa zaidi katika grassroots. Hoja kwamba CHADEMA isitegemee siasa za majukwaani au mitandaoni ni nyepesi sana. Maana ya hoja hiyo ni kwamba tuwakubalie maCCM wanaotukataza siasa za majukwaani.

Huko ni ku-surrender uwanja muhimu wa mapambano kwa adui, kwa sababu maCCM wanafanya siasa za majukwaani na mitandaoni pia. Kutuambia tuache siasa za mitandaoni ni poisoned advice. Hatuna magazeti, wala access to TV networks. Tunakatazwa siasa za majukwaani. Tukiacha na siasa za mitandaoni tutafanyaje siasa???

👉8. Masuala ya kutafuta fedha ni kazi inayoendelea on a daily basis. Shughuli za chama zinafanyika, licha ya matatizo mengi, kwa sababu watu wanajitolea fedha, rasilmali nyingine na muda wao katika shughuli za chama.

👉9. Kwa ujumla, mawazo ya Kigogo ni ya mtu ambaye hana uzoefu wowote katika kuendesha chama cha upinzani katika nchi hii na changamoto zake. Ana haki ya kutoa maoni na ushauri wake kwa jinsi anavyoona inafaa kwake, lakini sisi tunaopambana kila siku na matatizo na mazingira halisi ya kuendesha chama cha siasa cha upinzani hatuna wajibu au sababu ya kukubali ushauri wa aina hii.

CHANZO: Instagram