Licha Ya Uchafuzi Unaofanywa Mtandaoni Dhidi Yake, Wasifu Huu Kuhusu Rostam Aziz Unaonyesha Mchango Wake Mkubwa Kwa Tanzania Yetu

Jana niliweka taarifa za kukanusha tuhuma zinazosambazwa mtandaoni kuhusu mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania, Rostam Aziz, ambazo wahusika wamezifanya zionekane zinatoka kwangu.

Ni wazi kuwa lengo la wahusika ni kuua ndege wawili kwa jiwe moja. Kwa upande mmoja ni hilo la kumchafua Ndugu Rostam, na upande wa pili kunihujumu mimi binafsi, kwa kutumia jina langu kinyume na ukweli, kufanya  uchafuzi huo. Hii sio sahihi hata chembe.

Hata hivyo, tukio hilo limenipa fursa ya kumwangalia Rostam “kwa jicho jingine.” Na japo kuna wanaoweza kutafsiri tofauti makala hii, lakini katika zama hizi mpya chini ya utawala wa Mama Samia Suluhu, tunapaswa kuwaangalia pia watu mbalimbali kwa “mtazamo mpya.”

Mimi nafungua ukurasa kwa kutupia jicho nafasi ya Rostam katika Tanzania yetu, ambayo kwa sababu moja hau nyingine imekuwa haiongolewi kwa mtazamo chanya vya kutosha.

Lakini kama ilivyo kwa Rostam, mimi pia ni mhanga wa uchafuzi wa mtandaoni. Na katika tukio hilila sasa jina langu limetumika kufanya uchafuzi. Kwahiyo, ninaelewa vema maumivu yanayotokana na viendo hivi vya kihalifu.

Mara nyingi matarajio ya wanaofanya hujuma kama hizi za kuchafua watu mitandaoni ni kuona mtu asiye na hatia akidhalilika au kupatwa na maumivu. Lakini kuna namna moja mwafaka ya kukabiliana na maharamia wa aina hii, na ndio ninayoitumia kwenye makala hii: kugeuza hujuma zao kuwa kuni za kuchochea kitu chanya, ambacho kwa makala hii ni kueleza wasifu adimu wa Rostam, ambao sidhani kama umeshawahi kuandikwa na chombo chochote kile cha habari.

Japo mie binafsi siwahi kukutana au kuzungumza na Rostam, lakini naamini kila Mtanzania anamfahamu kuwa ni mfanyabiashara maarufu sio Tanzania tu bali pia duniani na  ambaye amejijengea heshima ya pekee duniani.

Akiwa Mbunge wa Igunga tangu miaka ya mwanzo ya tisini hadi mwaka 2012, Rostam alijipambanua kuwa mmoja wa wabunge walioacha alama za kipekee si katika jimbo hilo tu, bali pia kwa taifa kwa ujumla.

Kutokana na kulitumikia jimbo la Igunga kwa ufanisi mkubwa, wanachi katika jimbo hilo walikataa kata kata kuruhusu Rostam ang’atuke kwenye nafasi ya kuwa mwakilishi wao, japo yeye aliona kuwa ameshawatumikia vya kutosha na kuonelea ni vema akikabidhi kijiti cha uongozi kwa mwana-Igunga mwingine. Hata hivyo, taarifa kutoka jimboni humo zinaeleza kuwa wito wa kumtaka Rostam abadili mawazo na kurudi tena kuongoza jimbo hilo umekuwa endelevu.

Pengine ni Watanzania wachache wanaofahamu kuwa Rostam ndiye Mtanzania aliyeileta nchini Tanzania kampuni kubwa kuliko zote za mawasiliano ya simu za mkononi ya Vodacom.

Lakini licha ya kuileta kampuni hiyo, Rostam pia alifanya uwekezaji mkubwa uliowezesha kampuni hiyo sio tu kuwa ya kwanza kufikisha huduma zake hadi vijijini bali pia imeendelea kuongoza katika upatikanaji wa huduma za simu na mtandao Tanzania kote.

Ikumbukwe kuwa Vodacom ndio iliyoleta moja ya ubunifu mkubwa kabisa wa teknolojia ya kutuma miamala duniani, kwa maana ya huduma ya M-Pesa. Kwa sie tulio nje ya Tanzania ambako kuna huduma mbalimbali za kutuma miamala kama vile Western Union na Moneygram, M-Pesa inazibwaga huduma hizo kutokana na unafuu na uharaka wake.

Kwa upande mwingine, wakati wa utawala wa Rais wa tatu wa Tanzania, Marehemu Benjamin Mkapa (2005 -2015), Rostam alishauri kuhusu uanzishwaji wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF). Ushauri wake uliafikiwa na hatimaye Mfuko huo kuanzishwa kwa Sheria ya Bunge Sura 395 Toleo la  2002 kwa madhumuni ya kuwawezesha wanachama wake walio katika sekta rasmi na zisizo rasmi kupata huduma za matibabu kwa utaratibu wa uchangiaji kupitia bima ya afya.

Katika kitabu chake cha “My Life, My Purpose,” Marehemu Rais Mstaafu Mkapa alitanabaisha kuwa ubunifu wa Rostam ndio uliopelekea uamuzi wa kuanzishwa kwa NHIF unaohudumia mamilioni ya Watanzania.

Kadhalika, ubunifu mwingine wa Rostam ambao unaendelea kugusa maisha ya mamilioni ya Watanzania ni wa kuleta gesi mijini na vijijini kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Licha ya uamuzi huu kuwa na ufanisi katika kupunguza matumizi ya mkaa na kuni, na hivyo kulinda mazingira kwa kupunguza mabadiliko ya tabia joto, ujio wa gesi maeneo ya vijijini umechangia kubadilisha maisha ya mamilioni ya Watanzania.

Mwaka jana, baada ya kusikika taarifa za mauaji yaliyotokana na Uchaguzi Mkuu huko Zanzibar, Rostam alikuwa mwana-CCM pekee ailyejitokeza hadharani kukemea vitendo hivyo dhidi ya vyama vya upinzani, na yayumkinika kuamini kuwa raia yake ilichangia kukoma kwa vitendo hivyo.

Awali, katika utawala wa zamani wa Zanzibar, Dokta Salmin Amour, mfanyabiashara huyo maarufu alifanikiwa kuleta hoja bungeni kuitaka serikali ya chama chake, CCM, kuwachia mara moja mara moja viongozi wa CUF waliokuwa wamebambikizwa kesi ya uhaini.

Mwaka jana, wakati janga la korona lilipoingia nchini Tanzania, Rostam alikuwa mfanyabiashara pekee aliyejitolea shilingi bilioni moja kusaidia vita dhidi ya janga hilo.

Pamoja na mchango huo mkubwa wa fedha, pia alitoa msaada wa kusambaza vitakasa mikono (sanitizers) kwenye dala dala zote jijini Dar es Salaam na Zanzibar.

Kadhalika, Rostam alinunua mashine pekee ya kupima korona na kuipa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kitendo ambacho licha ya kuchangia kuokoa maisha ya wananchi wengi dhidi ya janga hilo, pia kimeiwezesha serikali ya Zanzibar kuingiza mapato ya hadi shilingi milioni mia moja kwa siku.

Ni vigumu kuandika mchango wote wa mfanyabiashara huyo kwenye makala moja kama hii, na hata ingekuwa kitabu kizima isingetosha kulinganisha na umuhimu wa mchango wake. Hata hivyo, kwa haya machache yaliyotajwa kwenye makala hii, yayumkinika kuamini kuwa mtu mwenye akili timamu atabaini kuwa Rostam si mtu anayestahili kuchafuliwa kwa tuhuma kama hizo zilizoenezwa kwenye mitandao ya kijamii, ambapo wahusika walitumia jina langu kwa lengo la kunichafua.

Ni matumaini yangu kuwa vyombo vya dola vitachukua hatua stahili kwa kuchunguza kwa kina wahusika wa uhalifu huu, na kuchukua hatua kali ili iwe fundisho dhidi ya kasumba hii inayoathiri maisha ya watu wasio na hatia, kama ilivyotokea kwa Rostam na kwangu pia.

Mungu Ibariki Tanzania na watu wake.

Mungu mbariki Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan