Leo Tuongelee Muziki Wa Kizazi Kipya

Ali Kiba na Diamond Wanapaswa Kujitafakari

Nianze Barua hii kwa taarifa mbaya na nzuri. Taarifa mbaya ni kwamba

(a) nitalazimika kufanya usajili upya wa watu mnaotumiwa kijarida hiki. Moja ya sababu za kuchukua hatua hiyo ni kuhakikisha kuwa kijarida hiki kinawafikia watu kusudiwa tu

(b) Ninaangalia uwezekano wa kuwa na paid subscription, yaani usajili wenye malipo kidogo. Lengo sio fedha bali kuhakikisha kuwa kijarida hiki kinawafikia watu stahili. Miongoni mwa sababu zilizonifanya kufikiria kuchukua hatua hii ni baada ya kubaini idadi kubwa ya watu wa Idara ya Usalama wa Taifa waliojisajili kutumiwa kijarida hiki sio kwa madhumuni ya kuhabarika/kuelimika bali wapate cha kuripoti kwa Kipilimba na Magufuli.

Taarifa nzuri ni kwamba wiki hii kuna matoleo mawili, hili na jingine nitakalowatumia Mei Mosi ambalo ni maalum kwa ajili ya masuala flani nyeti. Nimeshiliandaa toleo hilo lijalo na litajituma automatically saa sita kamili usiku wa Mei Mosi (kwa mida ya hapa UK).

Baada ya utangulizi huo, tuingie kwenye mada ya wiki hii. Inahusu muziki. Naomba nitamke mapema kuwa mie sio mfuatiliaji sana muziki wa sasa wa Tanzania. Napenda kazi za wasanii wetu lakini nadhani muziki wa siku za nyuma ulikuwa bora zaidi kuliko huu wa siku hizi.

Sina hakika kuhusu chanzo cha kushuka kwa muziki wetu lakini nadhani kwa upande mmoja ubunifu ni mdogo, na hilo linaweza kuwa linachangiwa na ukweli kwamba kila mtu anayeweza japo kukoroma anadhani anaweza kuwa msanii wa bongofleva, na kukimbilia studio kurekodi, na kwa vile tuna “janga la online TV,” basi kila siku ni lundo la nyimbo/video mpya zinazodumu kwa siku chache kama sio masaa machache tu kabla ya lundo jingine la nyimbo/video kuibuka.

Wiki iliyopita, wasanii wawili vinara Ali Kiba na Diamond Platnumz walitoa nyimbo zao mpya sambamba na video za nyimbo hizo. Naomba nitanabaishe kuwa mie sio shabiki wa wasanii hao, japo nina nyimbo tatu za Ali Kiba kwenye playlist ya simu yangu. Nyimbo hizo ni hizi hapa chini

Hebu fanya kuzisikia tu bila kuangalia video (quality ni very poor lakini pia enzi hizo teknolojia ya kurekodi video za kibongo ilikuwa bado ya kusuasua). Sikia ladha iliyomo katika nyimbo hizi tatu, kisha linganisha na nyimbo kadha wa kadha unazozijua za msanii huyo. Ofkoz, ladha is subjective, kwamba kwa vile mie ninaona kuwa hizi ndio kazi bora kabisa za Ali Kiba, wewe msomaji waweza kuwa na mawazo tofauti.

Hata hivyo, ladha nzuri katika muziki ina tabia moja kuu, kuufanya wimbo husika kuendelea “kuwa mtamu” hata miaka 10 na zaidi baadaye. Ni kama tungo za hayati Bob Marley, miaka nenda miaka rudi, reggae za Bob zina ladha ileile tamu ya miaka zaidi ya 30 iliyopita.

Turudi kwenye hizo nyimbo/video mpya za Kiba na Diamond.

Kwa mtazamo wangu, unaoweza kuwa fyongo, si nyimbo wala video husika zinaendana na hadhi ya wasanii hao. Kwa upande wa Diamond, nyimbo zake nyingi kwa sasa zimekuwa kama ana-recycle nyimbo zake za nyuma kama sio “sampling” ya nyimbo za wasanii wengine.

Kwa upande wa Kiba, kwa mtazamo wangu, kwa muda mrefu muziki wake umetegemea zaidi jina lake kuliko kiwango cha muziki/video husika.

Nyimbo/video zote hizi mbili hazina nafasi ya kubaki kwenye kumbukumbu ya msikilizaji/mtazamaji kwa sababu “zipo jawaida sana.”

Lakini ni nani anaweza kuwasaidia wasanii hawa kwa ushauri? Hakuna. Kwa sababu asilimia 99.9 ya wasanii wetu ni manunda flani wasio tayari kupokea ushauri wa aina yoyote ile. Na ukijaribu kuwapa ushauri watakuita “hater.” At the end of the day, ni muziki wao, na wana kila haki ya kuboronga au kuupendezesha watakavyo.

Ni muhimu pia kutambua kuwa kwa kiasi kikubwa muziki wa wasanii wetu ni kwa minajili ya “ujiko” zaidi kuliko maslahi. Kwahiyo, wasanii wengi huamua kukurupuka tu na nyimbo na pengine video sio kwa minajili ya kuuza wimbo/video husika bali kuweka jina lake kwenye chati, kitu kitakachomwezesha kupata shoo mbalimbali.

Kwa mujibu wa wanaoielewa music industry ya Tanzania, wanasema chanzo kikuu cha mapato kwa wasanii wa bongofleva sio mauzo ya nyimbo/video zao bali shoo mbalimbali. Na ili msanii apate shoo shurti asikike radioni/ aonekane kwenye runinga bila kujali ladha ya muziki/video husika.

Lakini kwa kuwatendea haki wasanii hawa wawili, eneo moja ambalo wamepiga hatua sana ni kwenye ubora wa video zao. Unajua moja ya “ulemavu” wa muda mrefu wa wasanii wetu wengi ulikuwa “kuona aibu kwenye video zao wenyewe.” Lakini kwa sasa ukiangalia video za Kiba na Diamond na wasanii wengine wengi tu, sio tu kuna kujiamini kwa wasanii husika bali pia hata viwango vya video ni vya kuridhisha.

Nakutakia siku na wiki njema.

Mtumishi wako

Evarist Chahali