Leo Ni Mwaka Kamili Tangu Musiba Atangaze WATU HATARI

Kabla ya kuingia kwenye mada naomba kueleza kuwa nitalazimika kuondoa baadhi ya mliojisajili kwa sababu takriban nusu yenu hamfungui emails ninazowatumia. Sasa kwa vile hii sio biashara ya urembo, ni vema nikabaki na watu wachache wenye nia ya dhati ya kusoma kijarida hiki.

Baada ya tahadhari hiyo, niingie kwenye mada fupi tu ya leo. Tarehe hii mwaka jana, mtu mmoja aitwaye MUSIBA aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kutangaza orodha ya watu tisa aliowaita WATU HATARI kwa usalama wa Tanzania.

Naikumbuka vema sana siku hiyo. Ilikuwa Jumapili, ghafla majira ya jioni nikaona mwenendo usio wa kawaida kwenye akaunti zangu huko Instagram, Facebook na Twitter. Kwamba ghafla idadi kubwa ya watu wakawa wanani-folo.

Sasa kwa kawaida, ukionga ghalfa watu wengi wanakufolo kwenye mitandao ya kijamii inamaanisha kuwa kuna jambo kubwa linakuhusu. Na ndio ilivyokuwa. Baadaye nilipigiwa simu kuambiwa kuwa kuna jamaa amenitaja kwenye video ambayo ameorodhesha “watu hatari.”

Nilipoiangalia video hiyo nilipatwa na ghadhabu kali sana. Niwe mkweli, laiti ningekuwa na uwezo wa kumfikia Musiba siku ile, ingekuwa balaa kubwa.

Kana kwamba alichofanya kwenye video kilikuwa hakitoshi, kesho yake akatuweka kwenye gazeti lake.

Na tangu wakati huo Musiba amekuwa kama amenogewa na mradi wake huo wa kuchafua watu.

Hapa ndipo ilipofikia Tanzania yetu. Tulipotwa “Watu Hatari” na Musiba, watu wengi waliona ni “msala” wetu pekee. Lakini baadaye Musiba akawageukia hata wana-CCM wenzie.

Ile video ya kwanza ya “Watu Hatari” ilitengenezwa baada ya Msuiba kupewa shilingi milioni saba na Daudi Albert Bashite na mlevi mbwa Kitwanga.

Hivi karibuni Musiba alipewa shilingi milioni 100 ili aendeleze jukumu lake la kuwachafua watu ambao Magufuli na mwanae Bashite hawawapendi.

Na sasa mradi huo wa kuchafua watu umekuwa mkubwa na umezaa magazeti mawili ya Kiingereza, na mengine mawili ya Kiswahili. Baadhi ya magazeti hayo ni haya pichani

Moja ya mambo hatari sana kuhusu Magufuli ni jitihada zake za kupandikiza mbegu za mfarakano. Amefanikiwa kujenga chuki kali kabisa kwa wana-CCM wenzie dhidi ya Wapinzani (hadi leo ni wachache tu walioruhusiswa japo kumpa pole Tundu Lissu na wamepigwa marufuku kuwatembelea wapinzani waliopo jela) na anaendeleza jitihada za kuwafanya Watanzania wawachukie wale wote wanaojaribu kupiga kelele dhidi ya udkteta, udini, ukabila, ukanda na ufisadi.

Nimalizie barua hii kwa kutanabaisha kuwa sijaandika ili kuonewa huruma au kupewa pole. Lengo ni kukuonyesha mwelekeo wa Tanzania ya Magufuli ambapo watu wasio na hatia wanatendwa kama wahaini. Leo kwa “ watu hatari” kesho yaweza kuwa kwako.

Tukutane wiki ijayo

Evarist Chahali