Kwaheri Da Mwele: Nitaenzi Heshima Uliyonipa 2015 Kuwa Mmoja wa Washauri Wako Kwenye Dhamira Yako ya Kuwania Urais. Tanzania Imempoteza Mwanasayansi Mtafiti Mbobevu. Rest in Power, Dadangu 😭😭😭
Jana jioni nilikutana na twiti iliyoashiria kuwa Dokta Mwele Malecela hayupo nasi tena duniani. Sikutaka kuamini, ikabidi niende kwa Mange kupata uhakika huku nikiomba taarifa hizo za kifo zisiwe kweli. Unfortunately, it was and it is true. Yaani kama ndoto vile, only that it isn't.
Moja ya kumbukumbu muhimu kwangu kuhusu Dokta Mwele ni mwaka 2015 alipoamua kuchukua fomu za kuwania Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na akanipa heshima ambayo itadumu nami milele - aliniomba niwe mshauri kwenye kampeni yake ya kuwania urais kwa tiketi ya CCM.
Japo sikuwahi kuongea hili kabla, mwanasayansi huyo mbobefu ambaye kwetu wengine tulizowea kumuita “Da Mwele”, alikaa nami kitako kuandaa hotuba aliyoitoa siku anachukua fomu za kuwania urais kupitia CCM. Kuaminiwa katika suala muhimu kama hilo ni heshima kubwa kabisa unayoweza kupewa maishani. Asante sana Da Mwele.
Alipoondolewa kionevu na Magufuli katika wadhifa wake kama Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, tuliwasiliana mara kwa mara, na kumpa imani kwamba kwa “akina Magufuli wakisema kwanini, dunia yenye kiu ya wataalamu wabobevu inauliza tutampata lini.” Na wiki chache baadaye akapata nafasi ya kazi katika Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, ambapo kituo chake kilikuwa Congo Brazaville.
Kama kawaida yake ya kuendekeza chuki, Magufuli aliendelea kumwandama Dokta Mwele


Lakini mwisho wa siku, chuki ya Magufuli kwa msomi huyo haikuzuwia kuteuliwa kwake kushika nafasi kubwa kimataifa, kwenye makao makuu ya WHO, ambako aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Udhibiti w a Magonjwa Yasiyopewa Kipaumbele.


Dokta Mwele Mkurugenzi wa WHO Geneva, aliendelea kuwa Dokta Mwele yuleyule wa WHO Congo Brazaville na kuendelea kuwa Dokta Mwele yuleyule wa NIMR, na Da Mwele yuleyule tuliyemzowea kwa unyenyekevu wake. Laiti usingeambiwa kuwa Baba yake, Mzee John Malecela, aliwahi kuwa Waziri Mkuu, usingeweza kubaini hilo kwani Da Mwele siku zote alikuwa mtu poa sana.
Pumziko la milele akupe Bwana, na mwanga wa milele akuangazie, upumzike kwa amani. Amen.