Kwaheri Aprili, Mei Hii Yaja na Mazito

Kuna Ishara Za Matukio Makubwa Yatakayoweza Kubadili Mwenendo Wa Taifa

Naomba nianze #BaruaYaChahali kwa kumshukuru Mungu kwa kunisuru tena sijui kwa mara ya ngapi. Muda huu unaposoma Barua hii ningekuwa marehemu. Kwa kifupi, Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa, Mchungaji Modestus Kipilimba alimtuma “afisa muuaji wa Kitengo” anaitwa Allan (naomba nihifadhi jina la pili kwa sababu maalum) kuja kuniua hapa Uskochi.

Bahati nzuri, mie “paka mwenye roho tisa” nikasalimika kwa mapenzi ya Mungu.

Awali, huyo muuaji Allan alishatumwa nchi mmoja ya Skandinavia kwenda kumuua Mtanzania flani lakini bahati nzuri msamaria mwema flani aliisikia hiyo ishu akamshtua mhusika, ambaye nae ikabidi aitangaze ishu hiyo hadharani, na kupelekea muuaji huyo kuachana na mpango huo wa kishetani.

Kipilimba sio tu ni kiongozi wa dini lakini pia ni mkuu wa kanisa analomiliki.

Kwamba anaweza kumtuma afisa wake Allan (au mwingine) kuja huku kwa dhamira ya kutuua, ni ishara kuw serikali ya Magufuli inaongozwa na mashetani. Na yeye Magufuli mwenyewe ni shetani pia kwa sababu aliridhia mpango huo wa Allan kuja kuniua. Hata hivyo, Mungu wangu ni mwema sana, na kamwe hawa majahili hawatofanikiwa katika azma zao za kishetani.

Kuna shetani anaitwa Jack Zoka, alikuwa Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa, zama za Kikwete, alitumia muda wake wote ofisini kujaribu kuniangamiza, akaishia kuondoka madarakani bila azma yake hiyo ya kishetani kutimia. Akapewa ubalozi Canada lakini akaishia kutumbuliwa baada ya serikali ya nchi hiyo kutoafiki utendaji kazi wake.

Mrithi wake, Robert Msalika Makungu, nae akaendeleza aliposhia Zoka, akafanya jitihada kadhaa za kutaka kunidhuru, akaishia kutumbuliwa na Magufuli, na sasa anahangaika kama RAS huko Tabora.

Huyu shetani kwa kushirikiana na “m-Kanda wa Ziwa” mwenzake, ambaye nae ni RAS kama yeye, Eliakim Maswi, walitumia toilet paper ya Musiba kuandika habari ya kunichafua.

Kabla ya kumtuma huyo muuaji Allan, Kipilimba alijaribu kumtumia Diwani mmoja wa Chadema ambaye sio tu ni pandikizi la Idara ya Usalama wa Taifa bali ni afisa mwandamizi wa taasisi hiyo. Diwani huyo anasoma PhD yake hapa Uskochi, na kwa takriban miaka miwili amekuwa kwenye jitihada endelevu za kunidhuru akishirikiana na binti mmoja ambaye hadi majuzi niliposhtukia mpango huo dhalimu, alikuwa rafiki yangu wa karibu kwa kama miaka minne hivi.

Tunaingai Mwezi Mei baada ya Aprili kusheheni kila aina ya madudu - kuanzia Magufuli kupokea ripoti ya CAG kimya kimya

hadi Mtu Mfupi Ndugai kutangaza kuwa Bunge lake halitofanya kazi na CAG,

kabla ya kufahamishwa kuwa serikali ya Magufuli imefanya ufisadi wa kutisha kama ulivyotanabaishwa kwenye ripoti hiyo ya CAG,

na tukapata ahueni baada ya kupatikana taarifa kuwa jitihada za kumng’oa CAG Prof Assad zimegonga mwamba,

na mwezi ukahitimishwa na kituko cha karne kwa Mbilikimo Ndugai kuendeleza mashambulizi yake dhidi ya CAG Assad

huku mmoja wa mawaziri wa ovyo kabisa katika historia ya Tanzania, mvaa mabendera Kangi Lugola akitishia kuvua nguo kufuatia tuhuma za ufisadi katika Wizara yake kama zilivyotanabaishwa na CAG na kuthibitishwa na Magufuli.

Kuna ishara kwamba mwezi huu wa Mei utatawaliwa na matukio mazito sana, ambayo yanaweza kuutikisa mno utawala wa kidikteta wa Magufuli.

Naomba nisieleze kwa undani zaidi ya kuwakumbusha kuwa USHIRIKA WA WACHAWI HAUDUMU, na likitokea la kutokea, msikose kunipa pongezi zangu kwa “kuwatonya mapema.”

Nakutakia siku na wiki njema, na pia nakutakia mwezi Mei mwema.

Mtumishi wako,

Evarist Chahali