Kinyago walichochonga wenyewe sasa kinawatisha: Chadema wahaha kumzuia Prof Hoseah asichaguliwe tena TLS japo Chadema haohao ndio waliomnadi kwa nguvu zote uchaguzi uliopita
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kipo kwenye jitihada kubwa za kupiga kampeni dhidi ya Profesa Edward Hoseah asirudi kwenye nafasi ya urais wa Chama cha Wanasheria Tanzania Bara (TLS) licha ya ukweli kwamba chama hichohicho ndio kilichopiga kampeni ya nguvu kuhakikisha Profesa Hosea anapata nafasi hiyo kwenye uchaguzi mkuu wa chama hicho mwaka jana.
Jasusi alikuwa mmoja wa watu aliokikosoa chama hicho kilipokuwa kinampigia debe Profesa Hoseah (wakati huo akiwa Dokta) kwa hoja za msingi kwamba mwanasheria huyo hakuwa na msaada kwa chama hicho hususan kuhusiana na jaribio lililofanywa na “watu wasiojulikana” dhidi ya Tundu Lissu mwaka 2017, na pia mwanasheria huyo alikuwa kimya wakati Chadema ikifanyiwa uonevu wa waziwazi na serikali ya Magufuli.
Lakini hoja zangu zilijibiwa kwa matusi - kama ilivyo kawaida kwa chama hicho - japo nafsini niliamini kuwa haitochukua muda kabla hawajageuza gia angania
Kwa kiasi flani kioja hiki kinakumbusha kioja kingine kilichofanywa na chama hicho mwaka 2015. Kwa wasiofahamu yaliyojiri miaka ya nyumba, Chadema ilianza kumuandama aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Awamu ya Nne (utawala wa Rais Jakaya Kikwete), Edward Lowassa, tangu Februari 2006 na baadaye kumtuhumu mwanasiasa huyo kuwa ni papa la ufisadi.
Kama mazingaombwe vile, baada ya kumuita fisadi kwa takriban miaka 9, chama hicho sio tu kilimpokea Lowassa bali pia kilimpitisha kuwa mgombea wao wa nafasi ya urais wa JMT kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Na kampeni za chama hicho kwenye uchaguzi huo zilijikita zaidi kwenye kumsafisha Lowassa kuliko kuishambulia CCM ambayo ilikuwa ikinuka kwa kashfa lukuki za ufisadi, zilizoibuliwa na Chadema haohao.
Lakini kwa vile Lowassa waliyemtuhumu kuwa fisadi sasa alikuwa mgombea wao, ilibidi waitelekeza ajenda ya kupinga ufisadi, na kuipa CCM mteremko wa kumwezesha mgombea wao John magufuli ashinde.
Kwahiyo, wakati kwa Lowassa Chadema walianza kwa kum-diss mwanasiasa huyo kisha kulamba matapishi yao, kwa Profesa Hoseah, walianza kwa kumnadi hadi akapata urais wa TLS, na sasa wanahangaika kumzuwia asirudi madarakani.
Kuna sababu kadhaa zinazoifanya Chadema kuwa hivi. Ya kwanza na ya msingi ni kwamba mara nyingi neno DEMOKRASIA lililomo kwenye jina la chama hicho haliakisi hali halisi ndani ya chama hicho. Japo CCM imekuwa mlengwa mkubwa wa lawama kutoka Chadema, lakini yayumkinika kutanabaisha kuwa CCM ina demokrasia zaidi kwa maana kuna nafasi za sauti za wengi kusikika, na wakati mwingine hata zile zenye mitazamo tofauti.
Kwa Chadema, si kwamba ndani ya chama kuna udikteta usioruhusu mawazo mbadala bali mawazo ya watu flani, kwa mfano Lissu, yanakuwa kama “maneno yaliyomo kwenye Biblia au Msahafu” ambayo waumini huyapokea kama yalivyo bila angalau kuyajadili.
Nje ya chama hicho, mtu asiye mwanachama akijaribu japo kushauri tofauti na msimamo wa chama, atavurumishiwa matusi na kuitwa kila jina baya. Uhuni huu haujawahi kukemewa na kiongozi yoyote yule, na unakinzana kabisa na neno DEMOKRASIA kwenye jina la chama hicho, kwani demokrasia ni pamoja na kusikia mitazamo tofauti hata kama huafikiani nayo.
Sababu nyingine ni kwamba chama hicho kinaendeshwa sana na matukio. Japo ajenda kubwa kwa sasa ni suala la katiba mpya, sambamba na kampeni ya kuchangisha fedha inayofahamika kama Join The Chain, kwa kiasi kikubwa, hakuna tukio litakalopita pasi chama hicho kulidandia.
Kwa sasa uchaguzi wa TLS umekuwa kama ajenda ya chama hicho. Na hili la vyama vya siasa kujiingiza kwenye chaguzi za vyama vya kitaaluma sio sahihi, hasa kwa chama cha upinzani kama Chadema ambacho miaka nenda miaka rudi kimekuwa kikiishutumu CCM kwa kuingilia masuala ya taasisi zisizo za kisiasa.
Kuhusu upinzani wa chama hicho dhidi ya dhamira ya Profesa Hoseah kurudi madarakani kwa kipindi kingine, chanzo ni mwanasheria huyo kuwemo kwenye kikosi kazi cha Rais Samia Suluhu Hassan kinachoshughulikia mchakato wa masuala ya siasa za Tanzania ikiwa ni pamoja na katiba mpya na tume huru ya uchaguzi. Chadema wamesusia mchakato tu, na ushiriki wa Profesa Hoseah umewakera, na sasa hawataki aendelee kuwa Rais wa TLS kwa muhula mwingine.
Je Chadema wanaweza kumzuwia Profesa Hoseah kushinda urais wa TLS?
Jibu la jasusi kijasusi ni kwamba uchaguzi huu ni ule Waingereza wanaita “it’s Profesa Hoseah’s to lose,” yaani ni uchaguzi ambao akishindwa basi sio kwa sababu ya zengwe la Chadema au umahiri wa wapinzani wake bali makosa yake mwenyewe.
Kwa upande mmoja, wapinzani wake hawatoi tishio kubwa dhidi yake, lakini kwa upande mwingine, kosa walilofanya Chadema “kumpromoti mtu anayejua kuchanga karata zake vizuri” linamsaidia mwanasheria huyo na kukwaza jitihada za chama hicho kumzuwia.
Baadhi ya wajuzi wa mambo wanadai kuwa Profesa Hoseah ana ndoto za kuteuliwa kuwa Jaji, na urais wa TLS unamuweka katika nafasi nzuri ya kufikia ndoto hiyo. Kwahiyo, ni dhahiri atapigana “kufa na kupona” abaki kwenye nafsi hiyo.
Lakini pia zengwe la Chadema dhidi yake linaweza kumsaidia kupata kura za huruma kutoka kwa wana-TLS hasa kwa vile wagombea wengine wote wanaungwa mkono na Chadema. Ni rahisi kwa Profesa Hoseah kusema upinzani wa Chadema dhidi yake ni wa maslahi yao kisiasa, na hao wagombea wanaoungwa mkono na chama hicho, watatumika kisiasa pia.
Kwa vile CCM imeonekana “kutojihusisha na uchaguzi huo” itamuwia vigumu mtu yeyote kumtuhumu Profesa Hoseah kuwa ni “kibaraka wa CCM” kwa sababu CCM hawamnadi ilhali Chadema ndio inawanadi wapinzani wa mwanasheria huyo.
Kwahiyo japo, jasusi akikaliwa kooni kuwa lazima abashiri nani atashinda, jawabu litakuwa Profesa Hoseah. Na akishindwa, sio kwa sababu ya zengwe la Chadema au uwezo wa wapinzani wake bali uzembe wake mwenyewe. Jasusi anarudi kusema “it’s Profesa Hoseah’s to lose” yaani “yeye tu, goli lipo wazi.”
Kuhitimisha, labda matokeo yakienda kinyume na matakwa ya Chadema inaweza kupelekea chama hicho kutafakari kuhusu jitihada zake endelevu ku-influence chaguzi za TSL.
Siku njema.
TANGAZO: Pakua kopi ya bure ya kijitabu cha “Evarist na Anko Zake”
chenye kurasa 24 tu cha watoto kulichoandikwa na Jasusi.
Unaweza pia kuwasikilisha watoto video hii ambayo ni audio version ya kijitabu hicho