Kifo Cha Mengi Na Kutekwa Mdude Chadema

Nianze toleo hili la #BaruaYaChahali kwa kuwashukuru nyote mlionitumia salamu za pole kutokana na mkasa niliouleza katika toleo lililopita.Naahidi kuwajibu kila mmoja wenu. Mungu awabariki sana.

Pia naomba nitumie fursa hii kuwatakia ndugu zangu Waislamu mfungo mwema wa Mwei Mtukufu wa Ramadhan. Kwa hapa Uingereza kuna waliaonza mfungu huu leo (Jumatatu) alfajiri hii lakini kwa mujibu wa taarifa, mfungo kwa Tanzania utaanza kesho (kulingana na madhehebu).

Nina wito wa aina mbili kwenu ndugu zangu Waislamu. Kwanza, mwezi huu wa toba unatoa fursa adimu kurekebisha kasoro mbalimbali maishani, si kwa ajili ya mwei huu tu bali milele kabisa. Kwa mfano, kama mtu alikuwa anakwama katika jinsi ya kuacha sigara, huu ni wakati mwafaka kwa sababu “kama unaweza kupitisha masaa 12 bila kugusa sigara basi kwa hakika unaweza kuachana kabisa na uvutaji sigara.” Hivyo hivyo kwenye matumizi ya pombe. Kadhalika, mwezi unatoa fursa nzuri ya kuachana na mapungufu mengine ya kibinadamu.

Hata hivyo, mwezi huu pia unatoa fursa nzuri zaidi kwa dua mbalimbali kwa watu binafsi na jamii kwa ujumla. Na hapa ndio nina wito wangu wa pili.Ninawaomba sana ndugu zangu mnaofunga kutumia mfungo huu kuiombea Tanzania yetu ambayo kwa hakika inaelekea kusikostahili chini ya utawala wa dikteta Magufuli (ambaye pamoja na maovu yake lukuki ni ubaguzi wa bayana dhidi ya Waislamu).

Nawasihi sana ndugu zangu kukazani dua za kuinusuru Tanzania yetu sambamba na kuombea apatikane mtu stahili wa kumrithi huyu dikteta kwa njia za amani (kwa sababu hana mpango wa kuodnoka madarakani hata baada ya mihula yake miwili hapo 2025).

Baada ya utangulizi huo twende kwenye mada ya wiki hii. Kuna habari mbili zilizotawala wiki iliyopita. Ya kwanza ni kifo cha bilionea Reginald Mengi. Naomba nitumie fursa hii kuongelea shutua kwamba mie mtumishi sijatoa pole kufuatia msiba wa tajiri huyo. Naomba tu niwe mkweli kwamba mtu ambaye hatukuwa na mahusiano mazuri wakati wa uhai wake, hatuwezi kuwa na mahusiano mema baada ya kifo chake. Na uthibitisho kuwa hatukuwa na mahusiano mazuri ni pamoja na bloku hii huko Twitter.

Hapana sio kama inaniuma kuwa blocked (mie ni mmoja wa Watanzania ambao wamebloku watu wengi mno 😁) bali naonyesha tu ishara za kutofautiana kwetu.

Na ningetamani sana watu tusiwe wanafiki wa kujifanya tunapendana baada ya kifo cha mtu ilhali hali ilikuwa tofauti wakati wa uhai. Kama wanichukia muda huu, tafadhali usihangaike kunipenda nitapofariki. It simply won’t help me. Nipende sasa, sio usubiri niondoke ndio ulete porojo za “oh marehemu alikuwa hivi, marehemu alikuwa vile.”

Kwa atakayesema “marehemu hasemwi vibaya” ninaafikiana na hilo na ndio maana nimeamua kutoeleza sababu ya kwanza.

Anyway tuliache hilo linalohusiana nami, lakini tuendelee kubaki kwenye suala la kifo cha mfanyabiashara huyo. Moja ya mambo ninayoona yana haja yakuongelea ni kauli ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete kukemea alichoita “taarifa za uongo kuhusu kifo cha tajiri huyo.”

Sijui ni kuzeeka vibaya au ukosefu wa busara tu, lakini Jk alipaswa kuelewa kuwa yeye si msemaji wa familia ya Mengi na kwamba alikuwa Rais huko nyuma haimpi mamlaka ya kuwaziba watu midomo.

Na angekuwa na busara angekaa kimya kwa sababu what if eventually ikibainika kuwa kifo hicho kilikuwa na walakini? Haitotafsiriwa kuwa kauli yake ya kukemea “uongo” ililenga “kuficha mambo fulani”?

Huko Jamii Forums kuliibuka mjadala kufuatia kauli hiyo ya Jk, na mdau mmoja alionyesha kuwa hii si mara ya kwanza kwa rais huyo mstaafu “kukurupuka,” ambapo ilielezwa kuwa hata wakati wa msiba wa Ruge, Jk alidai marehemu ameacha watoto wawili wakati sio kweli. Kukaa kimya nako ni busara.

Ofkoz, kifo ni kifo lakini kifo cha bilionea huwa na kawaida ya kuzua udadisi wa aina flani. Nisingependa kuingia kwa undani kuhusu suala hili japo naweza kukuacha na tafakuri hii

Jingine linalohusiana na msiba huo ni matarajio yangu kwamba mshikamano ulioonyeshwa na wanasiasa, kuweka kando tofauti zao za kiitikadi katika kuomboleza kifo cha Mengi, utaelekezwa pia kwenye suala la pili nitakalojikita kuliongelea baada ya “ishu ya Mengi,” yaani suala la “kutekwa” kwa mwanaharakati maarufu na kada wa Chadema, Mdude Nyangali almaarufu “Mdude Chadema.”

Lakini kabla ya kuingia kwa undani kuhusu suala hilo, jana zilizonekana picha za wanasiasa watatu vijana, Zitto Kabwe - kiongozi mkuu wa ACT Wazalendo, na January Makamba na Nape Nnauye wa CCM. Kwa tunaojua kusoma lugha za ishara tunaweza kuwa na tafsiri pana zaidi ya mjumuiko wa wanasiasa hao.

Kabla ya kuingia kwa undani kuhusu suala la Mdude, ni matumaini yangu makubwa kuwa January na Nape hawatoishia kuungana na Zitto kwenye msiba wa Mengi tu bali pia wataungana nae kupaza sauti kudai Mdude arejeshwe.

Ikumbukwe kuwa both January na Nape ni wahanga wa ukimya wao kunapojitokeza maovu mbalimbali katika jamii yanayohusiana na Jiwe au serikali yake au CCM.

Kwa upande wa January, “mbwa wa Magufuli” Musiba amekuwa akimwandama kwa siku kadhaa sasa

Ni matarajio yangu kuwa mifano hii michache itawasukuma wanasiasa hao wa CCM kutambua kuwa wanalolikalia kimya leo laweza kuwa jambo wanalotaka jamii ilipigie kelele huko mbeleni.

Kikwazo kikubwa cha ushiriki wa wanasiasa kama January na Nape kwenye masuala yanayohusu mustakabali wa taifa ni wao kuweka mbele maslahi yao binafsi kisiasa kuliko maslahi ya taifa. Na kwa hakika laiti wanasiasa vijana hawa wangeweka kando ubinafsi basi huenda muda huu wangeukuwa wameungana na Zitto huko ACT Wazalendo. Tuwe wakweli, si rahisi kuwa mtumishi wa dhati wa umma ukiwa ndani ya CCM. Hii sio sayansi ya roketi, ni fact ya wazi.

Kuhusu kutekwa kwa Mdude, binafsi naomba nielekeze lawama nyingi kwa wewe unayenisoma muda huu.

Naam, je ni lini uliwahi kusmama kidete dhidi ya udhalimu mbalimbali unaoendelea katika Tanzania yetu? Magufuli asingefika hatua ya kuamuru Mdude atekwe laiti jaribio lake kupitia kwa mwanae Bashite kumuua TunduLissu lingepelekea maandamano ya kulaani unyama huo.

Na kamwe asingeamuru Mdude atekwe laiti Watanzania wangeandamana kudai uchunguzi huru kuhusu idadi ya Watanzania waliouawa huko MKIRU (Mkuranga, Kibiti na Rufiji). Kadhalika, “angetuliza mshono” laiti huko nyuma wananchi wangemshikia bango kuhusu “kupotea” kwa mwanahabari Azory Gwanda au kada wa Chadema Ben Saanane.

Tumefika hapa kwa sababu wewe mdau unayenisoma muda huu umezembea kuchukua hatua stahili. Aidha kwa vile unadhani haya yanayojiri hayakuhusu au kwa kuamini kuwa kazi ya kupigania haki zako ni jukumu la “akina Chahali pekee.” Hapana ndugu yangu. Wewe, yeye, ninyi na jamii kwa ujumla ndio wenye jukumu la kumwambia dikteta Magufuli YATOSHA. ENOUGH IS ENOUGH.

Ni wakati wa kuchukua hatua. Kama Magufuli anaweza kutuma majahili wake kuwachukua akina Mdude huku akijua kabisa itazua kelele kutoka kwa akina sie, je hali ikoje kwa wewe mwenzangu ambaye “unajificha kwenye masuala ya siasa kwa kuhofia akina Bashite na mashetani wengine kama yeye?”

CHUKUA HATUA. KAMA SI LEO NI LINI BASI?

Tukutane wiki ijayo.

Mtumishi wako,

Evarist Chahali