Katiba Mpya Mnayopigia Kelele Hairuhusu Chuki Wala Ubaguzi: Kama Haikuwa Usultani kwa Mtoto wa Karume kuwa Rais Zanzibar, Kwanini Iwe Usultani kwa Mtoto wa Mwinyi Kuwania Unaibu Spika?
Jana nilikutana na twiti ya mwanaharakati mmoja akidai kwamba kitendo cha Abdulla Mwinyi, kutangaza nia ya kugombea nafasi ya unaibu spika, ni USULTANI.
Kuna mapungufu kadhaa katika hoja ya mwanaharakati huyo ambaye hujiweka mstari wa mbele kutetea haki, sambamba na kuhamasisha mapambano ya kudai Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi.
Pungufu la kwanza katika hoja yake ni ukweli kwamba kuwa mtoto wa Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, sambamba na kuwa mdogo wa Rais wa Zanzibar, Dkt Hussein Mwinyi, hakumuondolei Abdulla haki yake ya kikatiba kuwania nafasi ya uongozi katika taifa letu, ikiwa ni pamoja na nafasi hiyo ya unaibu spika.
Pungufu la pili ni hiyo “selective blindness” ya mwanaharakati huyo ambaye wakati anatafsiri kitendo cha Abdulla kuwania nafasi hiyo kuwa sawa na USULTANI, hakuwahi kulalamika pale Amani Karume, mtoto wa Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume, alipowania na kushinda urais wa Zanzibar.
Haukuwa usultani kwa sababu Rais Mstaafu Amani Karume hakugombea nafasi hiyo kutokana na kuwa mtoto wa Marehemu Karume bali kwa kuwa na sifa stahili za kuwaongoza Wazanzibari, sambamba na ukweli kwamba ilikuwa haki yake ya kikatiba.
Hali kadhalika, Abdulla hawanii unaibu spika kwa vile baba yake alikuwa Rais au kwa vile kaka yake ni Rais, bali mwanasiasa huyo sio tu ana haki kikatiba kuwania nafasi hiyo bali pia ana uzoefu wa kutosha kwenye masuala ya bunge, ndani na nje ya Tanzania, ambapo huko nyuma alikuwa mbunge kwenye bunge la Aafrika Mashariki.
Lakini kwa upande mwingine, mwanaharakati huyo pia ni mtoto wa viongozi wa zamani wa serikali na chama tawala CCM, na hajawahi kunyooshewa kidole kuwa “aemfika hapo alipo kwa sababu ya nyadhifa alizoshika baba yake.”
Kichekesho ni kwamba mwanaharakati huyo na kundi lake wapo mstari wa mbele kupigania KATIBA MPYA. Kwanini ni kichekesho? Kwa sababu msingi mkuu wa katiba ni HAKI na WAJIBU wa wananchi. Haki hizo ni pamoja na hiyo ya Abdulla kuwania unaibu spika kwa sababu katiba inamruhusu kufanya hivyo. Wajibu unaosisitizwa kwenye katiba ni pamoja na kuheshimu haki za wenzetu.
Ni kichekesho kuona watu wanaopigania nyaraka ya HAKI na WAJIBU wanakuwa mstari wa mbele kusigina HAKI za wenzao, na kutelekeza WAJIBU wao kuheshimu haki hizo za wenzao. Huu ni unafiki wa mchana kweupe.
Nihitimishe kwa kueleza kuwa kwa mtazamo wangu namuona Abdulla kama mgombea sahihi zaidi ya wote waliojitokeza, kwa sababu kuu tatu.
Kwanza: Itapendeza kuwa na Naibu Spika Mzanzibari na Spika m-Bara, kwa maslahi mapana ya Muungano wetu
Pili: Abdulla ana uzoefu wa kutosha wa shughuli za bunge kimataifa kutokana na yeye kuwa mbunge wa bunge la Afrika Mashariki huko nyuma.
Tatu: Ni mtu humble sana, na hii ni moja ya sifa muhimu katika uongozi.
Mwisho, kamwe tusiruhusu sumu ya ubaguzi na chuki kuwa ndio njia stahili ya kuendesha maisha yetu.
Wiki njema