Katiba Mpya Itapatikana, Tume Huru ya Uchaguzi Pia Itapatikana Lakini Si Kwa Matusi Bali Majadiliano
Jana nilifanya maongezi marefu na kada mmoja wa Chadema, daktari kitaaluma. Huyu msomi alinilaumu juzi baada ya mie kuwakemea wanaofanya siasa za chuki. Yeye alitaka niwakemee kwanza “waliosababisha hao wenye chuki wawe na chuki.”
Nikajitahidi kumuelimisha kwamba “two wrongs don’t make a right,” yaani “kwa vile kuna kosa lilishafanyika kabla, haimaanishi kosa hilo likifanyika tena linakuwa kitu sahihi.” Nikamueleza kwamba sio siri kuwa CCM na serikali zake, hususan ya marehemu Magufuli, imechangia mno kutengeneza na kusambaza chuki.
Nikatanabaisha pia kuwa sio siri kwamba Chadema walikuwa wahanga wakubwa zaidi wa siasa za chuki za marehemu Magufuli. Hata hivyo, hiyo haiwapi kisingizio nao kufanya siasa za chuki kwa vile tu nao walifanyiwa siasa za chuki.
Daktari huyo akadai kwamba sio sahihi kuwalaumu wahanga wa siasa za chuki ambao sasa nao wanafanya siasa za chuki, kwa vile wanachofanya wao ni matokeo tu ya kilichofanywa na CCM.
Baada ya maongezi marefu kwa DM nikahitimisha kuwa nilikuwa natwanga maji kwenye kinu. Huyo msomi alikuwa amevaa miwani ya mbao ya ukada, na usomi wake haukuwa na nafasi ya kubadilisha mtazamo wake.
Kuna msomi mwingine. Yupo huku ughaibuni. Huyu bwana alikuwa shabiki mkubwa wa Mlawa aka Kigogo wakati anatutukana watu tusio na hatia. Baada ya Mlawa kuhamia CCM, msomi huyo licha kuendelea kuwa mmoja wa “think tanks” za Chadema, pia ametokea kuwa miongoni mwa wasambazaji chuki wakubwa hususan dhidi ya chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo.
Mifano hii ya wasomi hawa wawili inatosha kueleza kwanini wengi wa wasomi waliopo CCM “hawana maana.” Kwamba tatizo sio CCM as such bali ukada. Kuvaa miwani ya mbao ya ukada inayonyima fursa usomi kuwa na msaada wa aina yoyote ile.
Kabla ya kuamua kuachana na maongezi na daktari kada, nilimuomba akumbuke maongezi yetu kwa sababu huko mbeleni -Mungu akitujalia uhai -nitamkumbusha. Kwa sababu hakuna kiumbe aliyewahi kufanya chuki kisha akapata manufaa kwa chuki hiyo. Chuki ni kama concentrated acid ambayo ukiiweka kwenye chombo cha plastiki, inakiyeyusha. Chuki humtafuna mwenye chuki taratibu.
Sasa suala la chuki linahusiana vipi na Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi? Kwa sababu Watanzania kwa asili yao ni watu wastaarabu. Na pengine wastaarabu kupita kiasi. Matusi na chuki si sehemu ya utamaduni wa Kitanzania. Pamoja na jitihada za akina Magufuli kuwarakanisha watu, bado mshikamano wetu kama taifa upo juu kulinganisha na majirani zetu.
Watanzania si vipofu.Wanaona wanaodai Katiba Mpya/Tume Huru ya Uchaguzi kwa matusi na chuki. Watawahukumu wakati utapofika kutoa hukumu.
Nimeshaongelea mara kadhaa kuwa kundi muhimu la wapigakura nchini Tanzania ni watu wasio na vyama. Kwamba kama CCM ina wanachama milioni 8 (hawafiki idadi hiyo ila ni makadirio ya juu) na kama wapinzani jumla ni milioni 5 hivi (kwa makadirio), maana yake Tanzania yenye watu milioni 61 hivi, ina watu takriban milioni 48 wasio na vyama. Tukiondoa watoto na figure hiyo inaweza kuwa takriban watu milioni 30. Yaani takriban nusu ya Watanzania wote.
Sasa hawa ndio wanaohitaji kushawishiwa kukiunga mkono chama kinachodhamiria kwenda Ikulu. Lakini kwa masuala ya katiba mpya na tume huru ya uchaguzi yanaweza kuhitaji kupigiwa kura huko mbeleni -moja ya mbinu za kupata katiba mpya ni kura ya maoni - ni wazi kuwa hawa wanaokimbizwa na matusi na siasa za chuki hawawezi kukiunga mkono chama kinachoendekeza matusi na siasa za chuki.
Kwa upande mwingine, hakuna uwezekano wa kupata Katiba mpya au tume huru ya uchaguzi pasipo majadiliano. Kwa sababu, kwa upande mmoja, CCM ndio imeshikilia mpini, na kwa upande mwingine, chama hicho tawala kitakuwa mhanga wa katiba mpya na tume huru ya uchaguzi.
Sasa huhitaji kuwa na busara kubwa kubaini kwamba ili kupata kitu kutoka kwa mtu ambaye kitu hicho kinampa nguvu dhidi yako, unapaswa kutumia njia mbili tu, kwa nguvu au kuomba. Hilo la kutumia nguvu halipo, kwa sababu lingekuwepo basi huenda hata Mheshimiwa Mbowe asingekuwa jela muda huu. Nguvu pekee waliyonayo watu ni kutukana mtandaoni na kujazana upepo “Spesi.”
Laiti nguvu hiyo ingekuwepo, akina Halima Mdee wasingeendelea kuwa wabunge wa kuteuliwa ndivyo sivyo (endapo madai kuwa Spika na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wameihujumu Chadema yana ukweli).
Kwahiyo, kwa vile hakuna uwezekano wa kutumia nguvu kulazimisha katiba mpya na tume huru ya uchaguzi, njia pekee iliyosalia ni kuomba. Na kisiasa, maombi hayafanywi kwa matusi bali majadiliano ya kistaarabu.
Na hiki ndicho kinafanywa na ACT-Wazalendo. Wanaweza kuchekwa, kudharauliwa, kukebehiwa na hata kutukanwa, lakini endapo watajipanga vyema, wana kila sababu ya kunufaika na siasa za kistaarabu. Kwa sababu Watanzania wengi pia ni wastaarabu.
Watanzania wengi wanakerwa na “demokrasia ya matusi” inayotumika kudai katiba mpya na tume huru ya uchaguzi. Lakini pia wanaona kuwa “kumbe hawa nao ni walewale” kwamba MATAGA wanatukana, na hawa nao wanatukana. MATAGA wanasambaza chuki, na hawa nao wanasambaza chuki.
Nihitimishe kwa kutanabaisha bila shaka kuwa Katiba mpya itapatikana, na tume huru ya uchaguzi itapatikana. Si rahisi kupatikana kabla ya uchaguzi mkuu ujao, lakini wanasema “never say never in politics.” Yanaweza kutokea ya kutokea, na mchakato huo ukaharakishwa. Lakini lililo wazi ni kwamba si katiba mpya wala tume huru ya uchaguzi itakayopatikana kutokana na matusi na chuki bali kwa mijadala ya kistaarabu.
Na hao wanaotukanwa leo kwa kufanya siasa za kistaarabu, wana tuzo inawasubiri huko mbeleni - endapo watajipanga vizuri.
Nakutakia maandalizi mema ya mwaka mpya 2022