Kada Chadema Ashauri Chama Hicho Kiwaondoe Mawakili Wanaomtetea Mbowe Ili "Kama CCM Wameamua Kumfunga (Mbowe) Wamfunge tu" Ni Baada ya Jaji Kuonyesha Upendeleo wa Waziwazi kwa Mawakili wa Serikali

Niwe mkweli. Haikuwa rahisi kunukuu bandiko hili la kada huyu kinadkindaki wa Chadema huko Jamii Forums.

Haikuwa rahisi kwa sababu kama walivyo makada wengi wa CCM, kwa makada wa Chadema nao utakuwa mtu poa ukiongea yale tu yanayowapendeza, lakini ukiongea wasichopenda, utamwagiwa matusi. Mtu ninayemnukuu ameshanitusi mara kadhaa huko Jamii Forums kila ninapoandika asichokipenda.

Hii ni kansa inayotafuna vyama vyetu vikuu vya siasa. Ni mbaya zaidi kwa Upinzani kwa sababu matarajio yetu kwao ni kwamba wao wawe tofauti na CCM wanayotaka kuiondoa. Hata hivyo huo ni mjadala wa siku nyingine.

Kabla ya yote, ninukuu bandiko la huyo kada wa Chadema huko Jamii Forums.

Moja ya sababu za msingi za kumnukuu kada huyu ni ukweli kwamba ni mmoja wa watu watatu hivi wanaoipigania sana Chadema huko Jamii Forums. Wapo watatu, wengine ni “BAK” (Bubu Ataka Kusema) na “Erythrocyte.” Kwa bahati mbaya - au pengine makusudi - nimekuwa mhanga wa maneno yasiyofaa kutoka kwao kila ninapoandika jambo “wasiloafikiana nami” kuhusu Chadema. Pengine ujasiri wa kutumia lugha isiyofaa unachangiwa na kutumia majina feki.

Twende kwenye hoja ya kada “Salary Slip.” Nakiri kuwa ina mashiko. Kwa sababu kama Chadema wameamua kususia chaguzi zote kwa sababu hawana imani na Tumeya Taifa ya Uchaguzi, kwanini basi waruhusu mawakili wao kuendelea na kesi ambayo sio tu ni ya kubambikizwa dhidi ya Mheshimiwa Freeman Mbowe bali pia Jaji aliyepo, kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake, ameonyesha upendeleo wa waziwazi kwa upande wa mashtaka?

Hata tusiojua sheria tunashuhudia Jaji Joachim Tiganga akitumia MTAZAMO WAKE BINAFSI badala ya kuongozwa na SHERIA, huku akifanya jitihada kubwa kuwanusuru mawakili wa serikali na mashahidi wao kila wanapobanwa na mawakili wa Mheshimiwa Mbowe.

Na kwa hakika huhitaji kuwa Jasusi kama mie kubashiri hukumu ya kesi hiyo feki itakuwaje. Ndio maana kuna mara nyingi huwa sipotezi muda wangu kufatilia mwenendo wa kesi hiyo, kwa sababu ni maigizo tu.

Japo lolote lawezekana maishani, lakini haiingii akilini kwa serikali kupoteza muda wake, na kimsingi kukubali kuaibika kwa ushahidi feki huko mahakamani, kisha serikali hiyohiyo ikubali kupoteza kesi hiyo.

Itakuwa kama kosa la Simba, wameshinda ugenini dhidi ya Wabotswana, lakini kama mzaha vile wakaruhusu kufungwa nyumbani. Sitaki kabisa kuamini kuwa serikali dhalimu ya CCM itaruhusu “kosa” hilo.

Lakini pia kinachoweza kuipa jeuri CCM kumfunga Mheshimiwa Mbowe ni ukweli kwamba licha ya kupita zaidi ya siku 100 tangu akamatwe na kubambikiwa kesi hiyo, jitihada pekee za Chadema kupinga uonevu huo umekuwa kwenye “kuupiga mwingi kwenye TwitterSpaces za wanaharakati wa mtandaoni.” Kwahiyo CCM wanafahamu fika kuwa hata wakiitumia mahakama kumfunga Mheshimiwa Mbowe, reaction pekee ya wana-Chadema itakuwa “kuupiga mwingi zaidi huko Maria Spaces.” That’s how useless the situation is.

Hata hivyo, wazo la kuondoa mawakili muda huu linaweza kuzaa matokeo yasiyokusudiwa (unintended consequences). Kuna kitu wanaita CATCH-22 ambayo Chadema wameshakumbana nayo mara kadhaa.

Kwamba, hata kama Chadema itawaamuru mawakili wanaomtetea Mheshimiwa Mbowe wajitoe, hakuna dalili kwamba CCM wataona aibu na kuamuru Mahakama itende haki.

Lakini pia, kwa vile tayari mawakili hao wameshashiriki kwenye kesi hiyo huku wakijua bayana kuwa ni ya uonevu, maana yake wamehalalisha haramu.

However, Kibatala na kundi lake wanaweza kubaki na roho nyeupe endapo wataamua kujitoa kwa sababu moja ya msingi - kukataa kuifanya najisi kuwa halali. Waingereza wanasema “it’s never too late to do a honourable thing.”

Nihitimishe kwa kutanabaisha kuwa wenye mamlaka ya kundelea au kutoendelea na kesi hii ni Chadema wenyewe, kwa ushauri wa wanasheria wake pamoja na Mheshimiwa Mbowe mwenyewe. Sie wengine tunachangia hoja tu.