Jinsi Ya Kugeuza Nyakati za Hofu/Mashaka Kama Zama Hizi Za #Coronavirus Kuwa Fursa ya Kuwa "Mtu Bora"

Mada hii inahusu jinsi nyakati ngumu za hofu na mashaka kama nyakati hizi za janga la korona zinavyoweza kutoa fursa adimu kwako kwenye maeneo mbalimbali.

Kwa mfano, japo pengine waajiri wengi huko Tz hawajaamua kuwaruhusu msiende kazini ili kupunguza maambukizi, janga hili kwa kiasi kikubwa limepelekea kupungua kwa pilika na "mishemishe."

Na kupungua kwa pilika na "mishemishe" maana yake kunakupatia muda ambao pengine usingekuwa nao.

Kwa mfano, ni lini ulipata wasaa wa kulala vya kutosha kabla hujakurupuka kukimbilia kwenye pilika zako? Moja ya vitu ambavyo wengi wetu hatupati muda wa kutosha ni kulala vya kutosha.

Kwahiyo kama janga la korona limepelekea uwe na muda wa kutosha, jitahidi "kuchapa usingizi" vya kutosha pia.

Kingine, japo chatisha, ni kifo. Yes, korona yaua. Na uwepo wake inatufanya "tunuse harufu ya kifo."

Majuzi nimesoma stori ya dada mmoja aliyeugua korona akieleza kuwa hajawahi maishani kujiona yupo karibu na kifo kama kipindi anaumwa.

Sasa, hofu kama hofu haina faida, sana sana itaishia kukuchanganya zaidi tu. However, hofu kama sababu ya kuchukua hatua chanya, ni kitu kizuri.

Kwa mantiki hiyo, hofu ya "huenda nikafa kwa korona" inaweza kukufanya sio tu utambue thamani ya maisha bali pia ujaribu kufanya uwepo wako duniani kuwa na manufaa kwa watu wengi zaidi yako.

Lini ulijiuliza, kwa mfano, "hivi nikifa, nitakumbukwa kwa lipi?" Kama wewe ni mbinafsi, hili halitokusumbua. Lakini kama ni mtu wa kujali, swali hilo laweza kuamsha ari ya kuanza kusaidia wenzetu wenye uhitaji mbalimbali.

Nyakati za mashaka na hofu kama hizi za janga la korona zaweza pia kukufanya utafakari mahusiano yako na Mola wako. Na kwa kufanya hivyo waweza kuelewa jinsi gani Mola wako "anashikilia uhai wako."

Hiki la kufanya tafakuri kuhusu uhusiano wako na Mola wako ni la muhimu zaidi ya yote niliyoandika katika mada hii. Zingatia hilo.

Pia nyakati hizi zinaweza kukupa fursa ya kujifunza vitu vipya, kwa mfano "jinsi ya ku-Google kwa ufanisi kupata taarifa za korona." Au kujifunza tahajudi, moja ya nyenzo muhimu na bora kabisa maishani.

Niishie hapa. Take care of yourself and others.

Ndimi mtumishi wako,

Evarist Chahali