Jinsi ya Kufanya Tahajudi, Moja Ya Nyenzo Muhimu Nyakati Kama Hizi Za Janga La #Coronavirus

Jana niliahidi kuwa muda ukiruhusu nitaeleza jinsi ya kufanya tahajudi (meditation). Tahajudi ni muhimu mno katika maeneo mbalimbali ya maisha yetu, lakini inakuwa na umuhimu wa kipekee katika nyakati za hofu na mashaka kama zama hizi za janga la korona.

Kuna aina mbalimbali za tahajudi, na zenye malengo mbalimbali na zinazofanywa kwa njia mbalimbali. Mie leo naomba kukupatia namna moja tu lakini pengine rahisi kuliko zote ya kujifunza na kufanya tahajudi.

Let's go! Nenda sehemu iliyotulia. Kaa kitini au sakafuni lakini hata ukisimama pia ni sawa. Relax. Fumba macho au kaza macho kuangalia mshumaa au kitu chochote kile. Fanya kuhisi kama wewe ni unyoya unaoelea angani kwa kusukumwa na upepo au fanya kuhisi unaelea mawinguni

Vuta pumzi ndani taratibu kabisa. Isikilize pumzi inavyoingia mwilini. Izuwie kwa sekunde chache, yaani kata pumzi kidogo. Kisha toa hewa hiyo nje taratibu kabisa.

Unapovuta hewa ndani, jenga picha kama unaingiza nishati mwilini. Na unapotoa pumzi jenga picha kama unatoa "uchafu" mwilini (hofu zako, shaka zako, maumivu yako, hasira zako, kilio chako, nk)

Rudia kuvuta hewa ndani, kukata pumzi kidogo, na kutoa hewa (kupumua hewa nje) mara kadhaa upendavyo, lakini ushauri wangu ni kuanza na dakika tano tu hivi, kisha unaweza kuongeza dakika 10, then robo saa, au hata nusu saa.

La muhimu ni kuepuka kelele za aina yoyote ile. Hakikisha unazima simu yako. Jitahidi pia "kuzima akili yako" kwa maana ya kutofikiria, kwa mfano, "sijui kuna ubuyu gani kwa naniliu."

Kwa kuanzia, fanya mara moja kwa wiki. Then waweza kuongeza hadi mara kadhaa kwa wiki, au kila siku. Unaweza pia kufanya kabla ya kulala au mara baada ya kuamka.

Ukishamudu njia hii rahisi kabisa unaweza kuhamia kwenye njia nyingine ambazo pindi muda ukiruhusu nitaziweka hapa huko mbeleni.

Ni matumaini yangu kuwa tahajudi itakusaidia sio tu katika kipindi hiki cha hofu na mashaka kutokana na janga la korona bali pia katika nyanja mbalimbali maishani mwako.

Nakutakia wikiendi njema. Jitahidi kuepuka mikusanyiko (ni lazima uende Church kesho?). Kaa tu nyumbani ikiwezekana. Nawa mikono mara kwa mara. Epuka kufikicha uso. Na chukua hatua stahili ukiona dalili za korona.

Ndimi mtumishi wako,

Evarist Chahali