Jinsi Kauli Za Magufuli Kuhusu Korona Zinavyofanya Watu Wengi Kulidharau Janga Hilo

Nimekutana na bandiko hili la mdau mmoja huko Jamii Forums na nikaona nilifikishe kwenu kama lilivyo

Kwanza niseme kuwa kuna makosa makubwa yanayofanywa na Administrators wa Jamii Firums kuunganisha mada nyingi kwa vile tu zote zimetaja Corona. Haya ni makosa makubwa. Hiki ni kipindi cha mapambano. Tuache threads nyingi za cotona kadiri inavyowezekana maana ndilo jambo kuu lililo mbele yetu kwa sasa. Tukifanya hivyo, JF nayo itakuwa imeshiriki kikamilifu kutoa mchango wake katuka maoambano dhidi ya corona.

Sasa nije kwenye mada yenyewe:

Nimesafiri toka Mwanza, nikaenda Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Morogoro, Iringa, Njombe mpaka Songea, huku nikichunguza uelewa wa watu, utayari wa watu, jitihada za watu na umakini wa watu katika kujikinga na shambulio la virusi vya Corona.

Kuna mambo machache ya jumla niliyoyagundua, na mengine kadhaa ya kina.

MAMBO YA JUMLA

1) Maneno ya Rais Magufuli aliyosema kuwa wananchi wasitishike na Covid-19, yamezingatiwa zaidi na wananchi kuliko maelekezo ya wataalam ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.

2) Wananchi wengi hawaujui ugonjwa huu, hawajui tishio lake na wala hakuna jitihada binafsi madhubuti za kutosha zinazofanywa kujikinga na ugonjwa huu kwa wananchi walio wengi.

Mji ambao, kwa kiasi fulani niliona kuna jitihada ni Mwanza, hasa pale Rock City ambapo kuna bomba za maji tiririka zimewekwa eneo la lango la uzio, halafu tena kuna bomba karibia na lango la kuingilia kwenye jengo, halafu kuna sanitizer iliyo na sensor kwenye lango la jengo, na ndani ya jengo, karibia maduka yote na mabenki kuna maji na sanitizer au angalao maji ya kunawa. Baadhi ya maduka, mpaka kuna watu wa kusafisha vitasa mara vikishikwa na wateja.

Maeneo mengine yote, pamoja na mji mkuu Dodoma, hakuna tahadhari yoyote ya maana.

Mapungufu ya kina niliyoyashudia:

1) Nyumba nyingi za wageni zina ndoo za maji na sabuni lakini hakuna anayemlazimisha au kumkumbusha mgeni kunawa maji wakati wa kuingia na kutoka

2) Baadhi ya nyumba za wageni, hasa Dodoma, hakuna hata maji wala sabuni za kunawa wageni wanapoingia na kutoka

3) Baadhi ya nyumba za wageni na maeneo ya kula, kuna ndoo za maji ambazo wakati mwingine huwa hazina maji wala sabuni. Ni kama wamelazimishwa, na wanachotaka kuonesha ni kuwa wametii agizo lakini hawana dhamira yoyote ya kujikinga na kuwakinga wengine

Jambo la kushangaza zaidi ni kwenye maduka ya madawa ya binadamu, ambayo kimsingi yanahudumiwa na wataalam wa afya wanaotegemewa kuwa na ufahamu mkubwa kwenye janga hili. Huko nimeyashudia yafuatayo:

1) Iringa nilishuhudia duka moja eneo la Miyomboni, kuna ndoo ya maji isiyo na maji na wala hakuna sabauni

2) Ndani ya duka, wateja wakikaribiana na wahudumu hata mpaka kwenye umbali wa sentimeta 30!

3) Milango ikiwa imefungwa wakati wote hali inayomaanisha kila anayeingia na kutoka ni lazima ashike mlango

Eneo jingine ambalo hakuna jitihada zozote ni kwenye makanisa:

1) Makanisa mengi hakuna maji wala sabuni.

2) Waumini wanaingia kwenye makanisa na kufanya ibada kama ilivyozoeleka

3) Njombe niliwasikia walokole wakisema kwamba hakuna mlokole atakayekufa kwa covid -19. Njia ya kujiokoa na covid-19 siyo kunawa mikono bali ni kuokoka

4) Iringa nilimsikia mlinzi mmoja wa hoteli akiwaambia wenzake kuwa Rais amesema kuwa Waafrika hatufi kwa korona kwa sababu rangi yetu ni kali na ni kiboko cha korona. Hata aliyekufa ni mzungu.

Kwenye mabasi, na hasa daladala, jitihada ni ndogo sana:

1) Daladala zinachukua level seat wanakoanzia lakini njiani wanaongeza abiria

USHAURI

1) Rais atoe kauli ya msisitizo na kueleza kuwa ugonjwa huu ni janga la Dunia, na unatishia ustawi wa binadamu mahali pote, kuanzia uhai wake, mahusiano ya kijamii mpaka uchumi. Uzoefu wa sasa unatuonesha kuwa siyo ugonjwa mwepesi kama tulivyotmfikiria mwanzo. Watu wachukue tahadhari zote kwa umakini mkubwa ili kupunguza madhara.

2) Maduka, mahoteli, na sehemu zote za huduma kuwepo na maji tiririka, sabuni na mtu anayemwelekeza na kumlazimisha kila mtu kunawa mikono wakati wa kuingia na kutoka

3) Maduka yote, mahoteli na sehemu zote zinazotoa huduma, kama siyo lazima, kwa vyovyote vile, milango ikae wazi ili kuzymuia watu kushika milango/vitasa

4) Serikali ikemee mafundisho na kauli yoyote inayopotosha ukweli, ikiwemo mafundisho ya kidini, hasa yale ya baadhi ya walokole wanaosema kuwa kinga ya corona ni kuokoka na siyo kufuata maelekezo ya wataalam

5) Vituo vya daladala vipunguzwe, na vile vitakavyobakia kutoa huduma ya watu kupanda na kushuka, viwekewe bomba za maji na sabuni, na watu wanawe wakati wa kuingia na kutoka

6) Mabasi yote, kila siku, kabla ya kuanza safari yapuliziwe dawa, na abiria wapande baada ya kila mmoja kunawa mikono

7) Baada ya abiria kupanda ndani ya mabasi, mhudumu wa basi atangaze taratibu za kufuata ukiwa ndani ya basi ili kuzuia maambukizi

8) Ndani ya basi, abiria waambiwe hawaruhusiwi kushika viti isipokuwa atakachokalia tu, ahakikishe hamkaribii na asikubali kukaribiwa na abiria mwingine, wasipeane vyakula au maji au kupokezana magazeti

9) Mabasi ya mikoani yasimame kwaajili ya chakula kwenye maeneo maalum ambayo wafanyakazi wake wamepata mafunzo, na kuna miundombinu inayoweka tahadhari ya kutosha

10) Kila chombo cha usafiri kimachotoa huduma ya usafiri wa umma, angalao kiwe na mtu mmoja amepewa mafunzo ya namna ya kujikinga na virusi vya korona

11) Serikali iruhusu biashara kwenye masoko yale tu ambayo yana miundombinu ya tahadhari ya corona

12) Viongozi wote wanatakiwa wawe mfano kwa kauli na matendo yao katika kupambana na virusi vya corona

Wananchi waambiwe wasibweteke kwa kuwa na idadi ndogo ya maambukizi. Wafahamishwe juu ya hatua za ugonjwa huu.

China maambukizi Desemba - vifo vingi Februari

Ulaya maambukizi January - vifo vingi March, April

Afrika maambukizi March - hatujui May itakuwaje (sahizi ni mapema mno kusema lolote, tuchukue tahadhari)

Waafrika tungekuwa makini tusingekufa kwa covid - 19. Tulikuwa na bado tuna nafasi nzuri ya kujifunza toka kwa wenzetu waliotangulia kupata maambukizi yaani China na nchi za Ulaya. Naungana na yule aliyesema:

China wameidhibiti covid - 19 kwa sababu ya nidhamu na umakini

Italy inaangamia kwa sababu ya kupuuza

Marekani inateketea kwa sababu ya kiburi (waliamini wana teknolojia, miundombinu na rasilimali za kutosha kushinda China)

Afrika ikipukutika itakuwa ni kwaajili ya ujinga.

Ndimi mtumishi wako,

Evarist Chahali