Barua Ya Chahali

Share this post
Ilipokuwa Juu, CUF Iliidhihaki Chadema.Twajua Kilichotokea Baadaye. Je ACT-Wazalendo Nayo Inaweza Kufanya Kama Chadema, na Kuja Kuwa Mbadala Tarajiwa wa CCM (Badala ya Chadema)?
www.baruayachahali.com

Ilipokuwa Juu, CUF Iliidhihaki Chadema.Twajua Kilichotokea Baadaye. Je ACT-Wazalendo Nayo Inaweza Kufanya Kama Chadema, na Kuja Kuwa Mbadala Tarajiwa wa CCM (Badala ya Chadema)?

Evarist Chahali
Dec 19, 2021
Share this post
Ilipokuwa Juu, CUF Iliidhihaki Chadema.Twajua Kilichotokea Baadaye. Je ACT-Wazalendo Nayo Inaweza Kufanya Kama Chadema, na Kuja Kuwa Mbadala Tarajiwa wa CCM (Badala ya Chadema)?
www.baruayachahali.com

Jana nilitwiti kwa kimombo kwamba ACT-Wazalendo, kwa kutumia uzoefu wao wa siasa za maridhiano huko Zanzibar, na endapo wataweza kuhamishia uzoefu huo katika “siasa za Bara,” basi watakuwa katika nafasi nzuri ya kuwa mbadala tarajiwa wa CCM badala ya Chadema.

Twitter avatar for @ChahaliJasusi @Chahali
2022-2025: If @ACTwazalendo would be able to emulate gains from consensual politics approach in Zanzibar, and apply them to "Mainland's context," wouldn't be many hardles to stop them from becoming main opposition (not in terms of number of MPs but credible alternative to CCM)

December 18th 2021

16 Likes

Japo twiti za kimombo husaidia kupunguza matusi, baadhi ya makada wa Chadema walinirukia kama mwewe huku baadhi wakiniambia ninaota, na wengine wakidai nawaliwaza tu ACT-Wazalendo.

Twitter avatar for @dr_lucky_martonlucky marton @dr_lucky_marton
@Chahali @ACTwazalendo Never on this Earth!! They are not credible now and they will never be in 2020-2025. ACT is equally to TLP and the likes.

December 18th 2021

1 Like

Kulikuwa na twiti kadhaa za matusi zilizopelekea niwabloku wahusika. Kanuni yangu mtandaoni ni rahisi: “kuwa muungwana au kula bloku” (be nice or get blocked).

Twitter avatar for @ChahaliJasusi @Chahali
Be nice or get blocked.

November 28th 2021

2 Retweets26 Likes

Wakati sikushangazwa na jinsi wafuasi wa Chadema walivyoipokea twiti hiyo, nilishangazwa kidogo na ukimya wa walengwa, yaani AC-Wazalendo. Hapana, lengo la twiti yangu haikuwa kuwafurahisha wao bali ilikuwa ni mwendelezo wa tathmini niliyoifanya kwa mara ya kwanza mwaka 2016, ambapo pamoja na mambo mengine nilikitabiria chama hicho kupanuka zaidi na huenda kuja kuwa mbadala wa Chadema kama mbadala tarajiwa wa CCM.

Lakini ili kuizungumzia ACT-Wazalendo kuwa mbadala tarajiwa wa CCM, ni muhimu kuiongelea Chadema wanaoshikilia “cheo” hicho kwa sasa.

Kwa takriban miaka 10 hivi, mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 uliomwingiza madarakani Jakaya Kikwete, Chadema iliibuka kuwa sio tu chama tishio kwa CCM bali kilikuwa sauti ya mamilioni ya Watanzania. Kilichowavutia Watanzania wengi, ikiwa ni pamoja na wafuasi wa chama tawala CCM, kwa chama hicho cha upinzani kilikuwa msimamo wake mkali na usioyumba dhidi ya ufisadi. Chama hicho kikiwa na “utatu mtakatifu” wa Mheshimiwa Freeman Mbowe, Mheshimiwa Zitto Kabwe na Dokta Willbrord Slaa, kilifanya kazi takatifu, kuibua ufisadi mbalimbali uligubika muda wote wa utawala wa Kikwete, kuanzia Richmond, Kagoda, Buzwagi, EPA, nk.

Chadema itaingia kwenye historia kama chama pekee cha upinzani kilichoweza kumng’oa Waziri Mkuu madarakani, ambapo baada ya chama hicho kuikalia kooni serikali ya Kikwete kuhusu ufisadi wa Richmond, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alilazimika kujiuzulu Februari 2008.

Moja ya siri ya mafanikio ya Chadema wakati huo yalikuwa kuaminika kwake ambapo baadhi ya watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa walikubali kuweka rehani ajira na uhai wao, na kuipatia Chadema taarifa mbalimbali za ufisadi wa serikali ya Kikwete.

Na japo Idara ya Usalama wa Taifa ilifanikiwa kuipora Chadema ushindi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, njia ilikuwa nyeupe kwa chama hicho kuingia Ikulu katika uchaguzi mkuu uliofuata, mwaka 2015, hasa kwa sababu CCM iliingia kwenye uchaguzi huo ikiwa vipande vipande sambamba na kugubikwa na miaka 10 ya ufisadi uliokithiri wa serikali ya Kikwete.

Lakini kama maigizo vile, Chadema ambayo ilifanikiwa kuongoza ushirikiano wa UKAWA na vyama vya CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, ikaishia sio tu kumpokea Lowassa bali pia kumfanya mgombea urais kwa tiketi ya umoja huo. Lowassa ambaye Chadema ilimuita fisadi kwa takriban miaka 9 mfululizo! Yaani umuite mtu fisadi kwa miaka tisa halafu ujaribu kumsafisha kwa miezi mitatu ya kampeni za uchaguzi!

Kama kuna jambo kubwa walilofanya Chadema kwenye uchaguzi huo lilikuwa kumsafisha Lowassa nchi nzima. Na pasipo kutarajiwa, CCM walirahisishiwa kazi na Lowassa, kwa sababu licha ya kwamba alikuwa kada wao wanayemjua vema, Chadema walishawasaidia huko nyuma kueleza madhambi ya Lowassa. Kwahiyo, Chadema walikuwa na kazi kubwa mbili. Moja ni kumsafisha Lowassa. Pili ni kumnadi.

Na ili kufanya yote hayo mawili, chama hicho kililazimika kuachana na ajenda yake kuu ya vita dhidi ya ufisadi.

Kwa bahati mbaya, au pengine makusudi, tangu wakati huo, chama hicho hakijaweza kurudi katika nafasi ya kuwa na ajenda yenye umuhimu na mvuto kitaifa, bila kujali itikadi za vyama.

Ikumbukwe kuwa umaarufu wa Chadema enzi hizo haukutokana na wafuasi wake pekee. Chama hicho kiliungwa mkono na hata baadhi ya wana-CCM. Lakini kundi muhimu zaidi kwa chama hicho lilikuwa Watanzania wasio na vyama.

Hii ni “voting bloc” muhimu sana kwenye siasa za Tanzania. Nitafafanua.

Kwa mujibu wa takwimu za jumla za uchaguzi mkuu wa 2015, idadi ya waliojiandikisha kupiga kura ilikuwa takriban watu milioni 25. Kwa ujibu wa takwimu za jumla, CCM ilikuwa na wanachama takriban milioni 8 ilhali upinzani ulikuwa na wanachama takriban milioni 5. Maana yake ni kwamba jumla ya wana-CCM (milioni 8) na upinzani (milioni 5) ni milioni 13 tu, takriban nusu tu ya wapigakura wote, takriban milioni 25.

CCM kwa kutambua kuwa hawahitaji kuwashawishi hao milioni 8 wao wamsapoti mgombea wao, na kutoona haja ya kuwashwishi hao milioni 5 wa upinzani, walielekeza nguvu kwa hao milioni 12 wasio na vyama. Kwa vile nilishiriki kwenye kampeni hizo kama msadi (consultant), nilishuhudia bayana jinsi mkakati huo ulivyofanya kazi. CCM iliwalenga watu hao wasio na vyama na “kumwaga sumu” kuhusu “kwanini Lowassa hafai kuwa Rais.”

Kwa upande wa Chadema, wao walikuwa bize na watu wao. Hawakujiahangaisha kufanya outreach yoyote nje ya wafuasi wao. Kwa bahati mbaya - au makusudi - miaka kadhaa baadaye chama hicho kinarudia kosa hilohilo kwenye “ajenda” yake mpya ya kudai katiba mpya na tume huru ya uchaguzi. Hamasa kuhusu “ajenda” hizo imekuwa miongoni mwa wana-Chadema, kwa msaada wa “wanaharakati wa mtandaoni,” na kuishia kutengeneza “echo chamber,” yaani “mnaongea na kusikilizana wenyewe tu.”

Kibaya zaidi, nafasi ya mawazo mbadala nayo imekuwa finyu kwa sababu kila anayejaribu kuongea kitu tofauti na “msimamo wa chama,” ni halali kumwagiwa mvua ya matusi. Hali hiyo pia ilitawala wakati wa kampeni za kumnadi Lowassa mwaka 2015. Kila aliyejaribu kufanya mjadala nao, aliishia kutukanwa.

Na hii ndio inanirudisha kwenye hoja yangu kwamba ACT-Wazalendo wana nafasi nzuri ya kuwapiku Chadema nafasi ya “mabadala tarajiwa” wa CCM, kwa sababu haiwezekani kuwa na “mbadala wa CCM wenye tabia kama za CCM.” Tunafahamu jinsi CCM inavyotumia wahuni wake kutukana na kudhalilisha watu mbalimbali wasiounga mkono chama hicho. Na Chadema wamekuwa wahanga mfululizo wa uhuni huo wa wafuasi wa CCM. Lakini kwa bahati mbaya, au pengine makusudi, chama hicho nacho kimekimbilia kwenye matusi na udhalilishaji kama silaha yake kuu.

Kibaya zaidi ni kwamba angalau viongozi waandamizi wa CCM hawajihusisha na matusi hayo. Kwa Chadema, baadhi ya viongozi waandamizi sio tu wamekuwa wakikalia kimya matusi yanayomwagwa na wafuasi wao bali nao wameshiriki pia. Bado kuna kumbukumbu jinsi chama hicho kilivyoshiriki kikamilifu kumwezesha Didier Mlawa aka Kigogo kutukana na kudhalilisha watu mbalimbali wasio na hatia.

Na sasa chama hicho kinatumiwa na mwanaharakati mmoja kutukana na kudhalilisha watu mbalimbali, hususan wanaopishana na msimamo wa chama hicho (mwanaharakati huyo?) kuhusu nafasi ya diplomasia katika kupata mwafaka wa kesi inayomkabili Mheshimiwa Mbowe.

Kuna Watanzania wengi tu waliochoshwa mno na CCM. Na kuna lundo la wana-CCM wanaotamani kuona chama wanachoweza kukiamini ili waachane na CCM yao. Lakini pia kuna wana-Chadema wachache wasiopendezwa na siasa za chuki/matusi. Wote hawa wanaweza kuwa mtaji muhimu wa kisiasa kwa ACT-Wazalendo.

ACT-Wazalendo haiwezi kuwa mbadala wa Chadema kwa kuangushiwa fursa hiyo kutoka mbinguni kama mana. Wanapswa wajihangaishe kufikia makundi mbalimbali -Watanzania wasio na vyama, wana-CCM wasioridhishwa na chama hicho, na wana-Chadema wasiopendezwa na matusi/siasa za chuki.

Kwa bahati mbaya, au makusudi, ACT-Wazalendo ni kama wameridhika na mafanikio waliyoyapata huko Zanzibar. Jitihada za chama hicho kitanua zimekuwa hafifu sana. Natambua changamoto za kilojistiki lakini mitandao ya kijamii inatoa fursa nzuri kwenye “recruitment drives” za vyama vya siasa.

ACT-Wazalendo wanapaswa kuondokana na mentality ya kuwa kama underdogs, second to Chadema, kwa sababu kama kweli wanataka kuingia Ikulu basi watambua kuwa kwanza watapaswa kuchukua nafasi ya Chadema kabla ya kupambana na CCM.

Wanaweza kuwa chama kikuu cha upinzani wakati wa uchaguzi mkuu ujao mwaka 2025? Yes na No. Yes, kwa sababu hawana sababu ya msingi ya kuendelea kuwa nyuma ya Chadema. No, kwa sababu muda ni mfupi. Tunaingia 2022 keshokutwa tu, na tutakuwa tumebakiwa na kama miaka mitatu tu kabla ya uchaguzi mkuu. Unless yatokee mabadiliko makubwa, ni ngumu kwa chama hicho kuipiku Chadema katika miezi 36 tu. However, kama wiki moja tu ni sawa na lifetime kwenye politics, miezi 36 ni kama uhai wa mtu, na lolote linawezekana. Lakini ili lolote liwezekane, ni lazima chama hicho sio tu kiamini kuwa kinaweza bali kianze jitihada za makusudi za kujitanua.

Jumapili njema

Share this post
Ilipokuwa Juu, CUF Iliidhihaki Chadema.Twajua Kilichotokea Baadaye. Je ACT-Wazalendo Nayo Inaweza Kufanya Kama Chadema, na Kuja Kuwa Mbadala Tarajiwa wa CCM (Badala ya Chadema)?
www.baruayachahali.com
TopNewCommunity

No posts

Ready for more?

© 2022 Evarist Chahali
Privacy ∙ Terms ∙ Collection notice
Publish on Substack Get the app
Substack is the home for great writing