Japo Nyakati Hizi za Janga La Korona Zahimiza Kuwajali Wenzetu, Ni Muhimu Kutosahau Kujijali Wewe Mwenyewe Pia.

Mada hii inahusu umuhimu wa kunijali mwenyewe ili uweze kuwajali wengine pia.

Mie nitakuwa mtu wa mwisho kukushawishi "uwe mtu mbaya" au katili (kama Bashite) au uwe na "roho mbaya" (kama Babake Bashite).

Kwa sababu uzuri kidogo wa sayari hii pekee tunayoishi unachangiwa na japo matone kidogo tu ya upendo, huruma, roho ya kusaidia wengine, nk.

Siwezi kusema "mie nina roho nzuri kweli" au "nina huruma mno" au "najali sana shida za wengine." Wa kusema hayo, au kinyume chake, ni nyie naowatumikia.

Ninachoweza kusema bila shaka ni kwamba kila siku najibidiisha kufanya japo kidogo kwa ajili ya wengine. Iwe kumkumbusha Jiwe kuhusu hili au lile, au kumkemea mwanae, Bashite, ambaye haishiwi drama, au kukuhamasisha uwe mtu bora, na kama tayari upo bora basi uwe bora zaidi.

Lakini mada hii inaweza kuonekana tofauti na hicho nachojibidiisha kukifanya na ninachojitahidi kukuhamasisha ukifanye - kuwa mtu mwema, mwenye upendo, mwenye huruma, mwenye kusaidia wengine, nk.

Mada hii inakushauri "uwe mbinafsi" Japo kidogo. Lengo si kujijali wewe tu bali kukusanya nguvu, nishati na muda wa kujali wengine.

Dada zangu wenye watoto mwafahamu hili. Usipojipa muda wa kupumzika pindi nafasi ikipatikana utaishia kulala badala ya kupika, kunyonyesha mtoto au kutimiza majukumu mengine ya mama.

Sasa nyakati hizi za janga la korona ni muhimu "kubalansi" kati ya kujali wengine na kujijali mwenyewe. Na ni muhimu kutambua kuwa huwezi kujali wengine bila kujijali mwenyewe kwanza. Huwezi kuwapa watu upendo kama hujipendi mwenyewe.

Ili kujua kama "unabalansi" kujijali na kujali wengine, jiulize maswali haya yafuatayo

👉 Unajiskia vibaya kusema "no" hata kama ni lazima iwe hivyo?
👉 Unajilaumu kusema "yes" kwa vile inakuathiri kwa namna flani?
👉 Huna muda kwa ajili yako mwenyewe?
👉 Unaona hustahili kushughulikia mahitaji yako kwa vile mahitaji ya wengine ni muhimu zaidi muda wote?
👉 Unadhani "dunia itakutenga" pindi ukishindwa kumjali/kumsaidia mtu kwa sababu umetingwa au huna uwezo wa kusaidia?

Maswali ni mengi zaidi ya hayo lakini haya yanaweza kusaidia kwa kuanzia.

Kumbuka, kujali wengine haimaanishi usijijali wewe mwenyewe pia.

Take care!

Ndimi mtumishi wako,

Evarist Chahali