Hongera Mama @SuluhuSamia, Mwanamke wa Kwanza Kuwa Rais wa Tanzania, kwa Kuendelea na Teuzi za Kihistoria, Hongera Zuhura Yunus (@venusnyota), Mwanamke wa Kwanza Kuwa Mkurugenzi Mawasiliano Ikulu
Nianze makala hii kwa pongezi zangu za dhati kwa Zuhura Yunus, sio tu kuteuliwa na Mama Samia Suluhu Hassan kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, bali pia kwa kuandika historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kabisa katika historia ya Tanzania kushika wadhifa huo muhimu.
Pongezi pia kwa Mama Samia, sio tu kwa vile Machi mwaka jana aliingia kwenye vitabu vya kumbukumbu kwa kuwa mwanamke wa kwanza kabisa kushika nafasi ya urais nchini Tanzania, bali pia kwa kuendelea kufanya teuzi za kihistoria, kama uteuzi huo wa Zuhura.
Ikumbukwe, awali Mama Samia aliandika historia nyingine alipotupatia Dkt Stargomena Tax kuwa mwanamke wa kwanza nchini Tanzania kushika nafasi nyeti ya Waziri wa Ulinzi.
Naomba nitanabaishe mapema kuwa mie ni muumini wa haki za makundi mbalimbali katika jamii, ikiwa ni pamoja na wanawake ambao kwa muda mrefu wamekuwa wahanga wa mfumo dume.
Kuna vitu viwili vinavyonifanya kuwa muumini wa haki za wanawake. Cha kwanza ni mafundisho ya wazazi wangu nilipokuwa mdogo, ambapo waliniusia kuwa “kila mwanamke ni taswira ya mama yangu.”


Kingine ni ukwelikwamba nilipokuwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es Salaam, kampasi ya Mlimani, nilisomoa kozi ya Family and Gender Relations (SO222). Kozi hii ambayo wanafunzi wanaume tulikuwa watatu tu, ilinfungua macho sana kuhusu nafasi ya mwanamke katika jamii zetu za Tanzania, Afrika na duniani kwa ujumla. Yayumkinika kutanabaisha kuwa kozi hii ilinaimbukiza virusi vya utetezi wa haki za wanawake.
Hata hivyo, kama sie wanafunzi wa kiume tulivyoonekana vituko hapo chuoni kwa kusoma “kozi ya wanawake,” utetezi wa haki za wanawake sio mgumu kwa wanawake wenyewe tu bali pia hata kwa wanaume wanaotambua umuhimu wa suala hilo. Mara kadhaa nimejikuta nikitukanwa kuwa ni shoga kwa kosa tu la kutetea wanawake.
Kibaya zaidi, mmoja wa watu ambao nilihangaika sana kutetea haki zake mtandaoni, leo hii ni mmoja wa wasambaza chuki wakubwa, pengine nambari wani kwa Tanzania.
Tukirudi kwenye uteuzi huo, kwa hakika nimefarijika mno. Sio kwa sababu mie na Zuhura tunafahamiana bali ukweli usiopingika kuwa ni mmoja wa wanahabari wachache kabisa wa Kitanzania walio mahiri mno kupindukia, katika ngazi ya kimataifa. Ni wazi, mwahabari kama Zuhura aliyemudu majukumu yake kwa ufanisi akiwa Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la hapa Uingereza (BBC Swahili), ukichanganya na uzoefu aliokuja nao hapa kutoka Tanzania, atayamudu vema majukumu yake hayo mapya.
Nihitimishe makala hii kwa kichekesho kidogo. Kuna mzushi mmoja aliniuliza jana “we jasusi, naona umefurahia Zuhura kuteuliwa kana kwamba umeteuliwa wewe. Utaishia kushangilia teuzi za wenzio tu, lakini wewe usitarajia hata ukatibu kata.” Kweli akutukanae hakuchagulii tusi.
Ukweli ni kwamba mie ni muumini mkubwa wa kusherehekea mafanio ya wenzetu.

Na hili nitaliongelea katika kozi endelevu ya Jinsi ya Kuwa Mtu Bora ambayo inapatikana hapa kwenye kijarida.
Hongera sana Zuhura na kila la heri katika majukumu yako mapya.