Kozi ya Open Source Intelligence (OSINT) kwa Kiswahili imeanza rasmi. Hapa kuna somo la kwanza, la pili na la tatu.
Karibu katika kozi hii ya kipekee ya Open Source Intelligence kwa kifupi OSINT. Ya kipekee kwa sababu hii ni mara ya kwanza kabisa kwa kozi ya OSINT kufundishwa katika lugha ya Kiswahili.
Open Source Intelligence ni intelijensia inayopatikana kwenye vyanzo vya wazi.
Yayumkinika kuhisi neno “intelijensia” linaweza kuwajengea uoga baadhi ya watu kwa kudhani wanajifunza kitu ambacho ni kwa ajili ya watu walio kwenye taaluma ya intelijensia tu.
OSINT sio tu inaweza kutumiwa na kila mtu bila kujali taaluma yake bali pia ni muhimu kwa takriban kila mtu. Kwa mfano, kwa kutumia OSINT unaweza “kujitafuta mwenyewe mtandaoni” na kubaini taarifa zilizozagaa mtandaoni pasipo wewe mwenyewe kufahamu.
Lakini pia OSINT ni muhimu kwa kila anayejali usalama wake mtandaoni kwani inamwezesha mtu kubaini ubora au mapungufu katika usalama wake mtandaoni.
Katika bandiko hili kuna masomo matatu.
Somo la kwanza ni utangulizi kuhusu OSINT na kozi hii kwa ujumla.
Somo la pili linahusu tahadhari wakati wa kozi hii na wakati wa kutumia OSINT huko “uraiani.”
Somo la tatu ni malengo/matarajio ya kozi hii.
Kozi imeandaliwa katika mfumo kwamba ili uelewe somo linalofuata shurti ulielewe somo lililotangulia. Kwa mantiki hiyo, masomo haya mawili ni ya muhimu kwa safari ya kuvutia ya kuelekea kuielewa OSINT. Naam, ni ya kuvutia kwa sababu huko mbeleni utafanya vitu kwa kutumia na kubaki unatabasamu mwenyewe.