Hakuna tatizo ACT-Wazalendo kuanza na kudai tume huru wala Chadema kuendelea na kudai katiba mpya, tatizo ni kwamba mchakato huo ukienda vema utawaathiri "wanufaika wa mifarakano ya kisiasa."
Nimeshatanabaisha mara kadhaa kwamba kuna watu wanaonufaika na mifarakano ndani ya Tanzania yetu. Na manufaa makubwa wanayopata ni ya kifedha.
Naomba ieleweke simaanishi kila anayefanya harakati kwa ajili maslahi ya Tanzania yetu au wananchi kwa ujumla ananufaika binafsi. Na simaanishi kuwa ni kosa la jinai kunufaika kwenye harakati za maslahi ya jamii. Hata hivyo ninatatizwa na watu wanaofanya harakati kwa kutumia matatizo halisi, lakini harakati hizo zinalenga kuwaufaisha wao badala ya Watanzania.
Moja ya mijadala mikubwa inayoendelea muda huu ni kuhusu suala la Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba Mpya. Mijadala yote hii ni kwa maslahi ya Watanzania.
Na kwa minajili ya kufupisha maelezo, mjadala uliopo sasa ni je “tuanze na kudai tume huru ya uchaguzi kwanza kabla ya kudai katiba mpya” au “tudai kwanza katiba mpya kisha ndio tudai tume huru ya uchaguzi”?
Tunafahamu kuwa Chadema wamekuwa wakitilia mkazo zaidi kwenye madai ya katiba mpya japo pia ajenda ya kudai tume huru imekuwa kipaumbele chao. Kwa upande mwingine, ACT-Wazalendo wametamka bayana kuwa wao wataanza na kudai tume huru ya uchaguzi, kisha ndio wawekeze nguvu kwenye kudai katiba mpya.
Hadi hapo hakuna tatizo kwa sababu Chadema wakiwezesha kupatikana kwa katiba mpya na ACT-Wazalendo wakawezesha kupatikana kwa tume huru ya uchaguzi, itakuwa kile Waingereza wanaita “wini-win” kwa maana sio tu ushindi kwa vyama vyote viwili bali kwa Watanzania wote pia.


Lakini kuna genge dogo la “wanaharakati wa mtandaoni” - watu wanaoamini kuwa wana akili zaidi ya Watanzania wengine, kwa sababu ya taaluma zao au kwa sababu ya familia wanazotoka - ambao wanataka “lazima iwe A tu” kana kwamba “B” au hata “C” ni kosa la jinai.
“Wanaharakati” hao wanailaumu ACT-Wazalendo kwa kuamua kuanza na tume huru ya uchaguzi. Wanataka vyama vyote vianze na kudai katiba mpya.
Lakini kimsingi tatizo sio kwamba ACT-Wazalendo wafuate uamuzi wa Chadema kuanza na katiba mpya. Tatizo ni kwamba “wanaharakati” hao wanaowaona ACT-Wazalendo na Watanzania kwa ujumla kuwa HAMNAZO, kwamba hawawezi kuwa na maamuzi sahihi, kwa vile ni wao (“wanaharakati” hao) tu ndio wanaoweza kuwa na maamuzi sahihi.
Na hii ni moja ya changamoto inayomkabili Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Mheshimiwa Freeman Mbowe, kwa sababu “wanaharakati” hao wamekuwa wakiitumia Chadema kama jukwaa la ajenda zao.
Uwepo wa Mheshimiwa Mbowe gerezani ulipelekea ombwe ambalo “wanaharakati” hao walilitumia ipasavyo kukiendesha chama hicho kwa rimoti.
Bahati nzuri dalili zote zinaashiria kuwa Mheshimiwa Mbowe anakirejesha chama hicho mikononi mwa mwenye chama. Na nina imani kuwa muda si mrefu, chama hicho kitafanikiwa kujitenga na “wanaharakati” hao kwa sababu moja kuu: ajenda za Chadema ni kwa maslahi ya taifa ilhali ajenda za “wanaharakati” hao zimejikita katika maslahi binafsi.
Kama nilivyotanabaisha awali, sio kosa la jinai kuwa “mwanaharakati.” Lakini ni tatizo pale “uanaharakati” unapotumika sio tu kwa ajili ya maslahi binafsi bali pia kuwaaminisha Watanzania kuwa “kila kitu kipo ovyo.”
Yayumkinika bila shaka kuhitimisha kuwa “wanaharakati” walichangia sana “kumtibua Mama Samia” baada ya kumwandama na baadhi ya kumtukana matusi ya nguoni licha ya kiongozi huyo kutamka bayana tangu mwanzoni wa utawala wake kuwa moja ya malengo yake makuu ni kuwajengea Watanzania mshikamano na umoja wa kitaifa.
Walimuandama kiongozi huyo kwa sababu walishahisi kuna hatari ya “kukosekana mifarakano ya kisiasa, ambayo huwaingizia kipato.”

Uwepo wa kesi ya Mheshimiwa Mbowe ulikuwa kama “mbuzi kagongwa kwa muuza supu.” Huenda siku moja jamii itafahamishwa kiasi cha fedha kilichopatikana kupitia kampeni za kudai Mheshimiwa Mbowe sio gaidi, na fedha hizo “kutiwa kibindoni.” Kwa sababu Mheshimiwa Mbowe si mtu wa kwanza ambaye matatizo yake yaliishia kuwanufaisha watu wengine.

Tukirejea kwenye suala la tume huru na katiba mpya, ni wazi kwamba “wanufaika wa mkwamo kwenye mchakato wa katiba mpya/tume huru” hawatopendezwa na kuondoka kwa mkwamo huo. Watapigaje pesa kwa hashtag ambazo sasa ni ajenda rasmi za vyama husika?
Kwa upande mwingine, chuki kubwa inayozagaa mtandaoni dhidi ya ACT-Wazalendo inachangiwa na haohao wanaotaka kuvitumia vyama vya siasa kwa maslahi yao. Mheshimiwa Zitto Kabwe anawaita “party hoppers” yaani “wadandia vyama.”


Jasusi @Chahali
Alikuwa CCM. Magufuli alimponyima nafasi wa Mkurugenzi Mawasiliano Ikulu, akajisogeza ACT-Wazalendo. Huko nako walipomshtukia anataka kukiendesha chama kama ofisi yake, akajisogeza kwa makamanda. Na akamleta kaka yake, Mlawa. Ni suala la muda tu kabla hajakimbilia kwingine.Na kwa kiasi kikubwa “mafanikio” ya wadandia vyama hao yanachangiwa na janga linalowasumbua Watanzania wengi: usahaulifu.

Nihitimishe kwa kutanabaisha kuwa kwa mtazamo wangu, tume huru inaweza kupatikana kirahisi zaidi kuliko katiba mpya. Kwa sababu kimsingi, tume huru ni kuhusu uteuzi tu wa watu husika wenye sifa husika. Lakini katiba mpya ina mchakato mrefu ikiwa ni pamoja na kukubaliana endapo “tuendelee pale lilipoishia bunge maalum la katiba” au “tuanze upya.”
Nina “reservations” zangu binafsi kuhusu both tume huru na katiba mpya lakini hapa sio mahala pake. Nitaongelea kuhusu hilo wakati mwingine.
Nawatakia siku na wiki njema
Create your profile
Only paid subscribers can comment on this post
Check your email
For your security, we need to re-authenticate you.
Click the link we sent to , or click here to sign in.