Guest Column: "Tanzania Anayoitaka Mama Samia."

Makala kutoka kwa mdau. Naomba niiwasilishe kama ilivyo.

Tarehe 19/03/2021 ni siku ambayo aliapishwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama. Hatimaye Tanzania iliingia kwenye historia kupata Rais Mwanamke ambayo kwa jicho la kawaida hapo kabla ilionekana ni safari ndefu wanawake kufikia uongozi wa juu ya Nchi yetu.

Mataifa hasimu na marafiki wa Tanzania wanafuatilia kwa umakini mkubwa hali ya nchi yetu kila mhula wa uchaguzi unapowadia. Vuguvugu la kisiasa lilikuwa juu mara baada ya Uchaguzi Mkuu 2021 ambapo matokeo ya kishindo ambayo chama cha CCM iliyapata yalikumbana na shangwe, bumbuwazi na sintofahamu kutoka pande zote zenye maslahi kwenye uchaguzi huo. Kwa mara ya pili mgombea wa CCM Hayati John Pombe Joseph MAgufuli alipata ushindi wa kishindo akiongoza pia kupata wabunge wengi kwenye majimbo ya uchaguzi. Wagombea kutoka vyama shindani vya siasa waliachwa kwa mbali sana.

Tarehe 17/03/2021 Tanzania ilipatwa na msiba mkubwa wa kuondokewa na Rais wake John Pombe Joseph Magufuli ambapo kwa mujibu wa Katiba ya Nchi, Makamu wa Rais anapaswa kuapishwa kushika madaraka ya Urais kwa mujibu wa masharti na muongozo wa Katiba hiyo.

1.       Endapo itatokea Rais aliyepo madarakani ataaga dunia miaka ndani ya miaka miwili kabla ya kumalizika muhula wake, Makamu wa Rais ataapishwa na kuongoza kumalizia muda uliosalia lakini hatogombea Nafasi ya Urais kwenye uchaguzi unaofuata

2.       Endapo Rais aliyepo Madarakani ataaga dunia kabla ya miaka mitatu au zaidi kumalizia muhula wake, Makamu wa Rais ataapishwa kushika Nafasi ya Urais lakini ataruhusiwa kugombea Nafasi ya Urais katika Uchaguzi Mkuu unaofuata.

Baada ya mazishi ya Kitaifa ya Rais John Magufuli, Rais Samia Suluhu Hassan alihutubia Bunge kuelezea mtazamo na mwelekeo wa serikali anayoiongoza ya awamu ya sita. Rais Samia hakuishia hapo, aliendelea na kutoa muelekeo huo wa serikali alipozungumza na Wazee wa Jiji la Dar es Salaam, alitoa ufafanuzi wa matarajio ya serikali yake kupitia pia Mkutano wake na Wanawake kupitia jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT) uliofanyika Dodoma tarehe 08/06/2021

Kwa kuweka kumbukumbu vizuri, ni vyema tukaenda kwenye kuainisha vipaumbele vya serikali ya Awamu ya Sita.

1.       KODI

Rais ameelezea na kutoa maelekezo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuhakikisha inaachana na mtindo wa kukusanya kodi kwa mabavu.

Ameelekeza kusiwepo na ubambikiziaji wa madeni ya Kodi kupitia compliances hasa ikichukuliwa walipakodi wengi wakubwa wamekuwa wakibanwa kwa mtindo huo ilihali mkononi wanazo clearance certificates za TRA kwa mihula yote ambayo wanaonekana wana areas kwenye Kodi

Amekipangua kikosikazi cha kuwabana wawekezaji wakubwa kwenye eneo la kodi. Kwa hatua hizi za awali ni wazi kwamba nia ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Taifa linasonga mbele kiuchumi bila kuumiza wawananchi wake na wawekezaji.

2.       KUFUNGUA NCHI/ DIPLOMASIA YA UCHUMI

Katika teuzi bora ambazo amezifanya ni nafasi ya Waziri wa Mambo ya nje ambaye anabeba sera ya nchi kwa nchi za ulimwengu. Balozi Mulamula ni chaguo sahihi kabisa kwa nafasi ya Waziri wa Mambo ya Nje na Afrika Mashariki. Diplomasia ya Uchumi inahusika kwa kiwango kikubwa uhusiano wetu na mataifa ya ulimwengu huu.

Tanzania haijajitoa kutoka kundi la Nchi zisizofungamana na upande wowote, bado imesalia kuwa kisiwa cha amanin na mpatanishi huku ikitoa vijana wake kushiriki kwenye vikosi vya kulinda Amani ndani ya mataifa yenye vita vya ndani.

Hivi juzi tumemsikia Rais wa Namibia ambaye alitembelea nchi yetu akitoa mualiko kwa Rais na wataalam wetu kwenda kujifunza na kubadilishana mawazo kwenye eneo la rasilimali za madini na Uchumi.

Rais SSH akihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano alisema kuwa anataka kuifungua nchi ili kwa kuhakikisha mazingira ya uwekezaji na kuondoa urasimu kwenye eneo hilo ili kuvutia wawekezaji wa ndani nan je kuanzisha viwanda, miradi na huduma mbalimbali.

3.       UWAJIBIKAJI WA WATUMISHI WA UMMA

Katika eneo hili, Rais Samia Suluhu Hassan ameshaweka bayana kwamba, kila kiongozi na mtumishi wa Umma wajitahidi kutatua kero na changamoto za wananachi wa maeneo yao. Akihutubia siku ya kuwaapisha viongozi aliowateua, alibainisha kuwa kero nyingi zinazowasilishwa kwa viongozi wa juu wa nchi zinaweza kutatuliwa na viongozi wa maeneo husika. Hivyo aliwataka Watumishi wa Umma kutenda haki na kuweka sikio lao kwa wananchi ili kupunguza usumbufu kwa wananchi hasa kwenye migogoro ya ardhi, mirathi na masuala ya haki.

Ameweka wazi kwamba, siku anayofika kwenye ziara zake za kikazi kwa wananchi halafu akakutana na mabango ya kero za wananchi, jambo hilo litapelekea kuchukuliwa hatua kwa viongozi na watumishi wa umma wenye dhamana kwenye eneo hilo. Pamoja na hayo amewaasa viongozi kutotumia nguvu za dola kuzuia malalamiko ya wananchi mbele ya viongozi wakuu.

Kwa mtazamo mpana, hapa SSH ametoa mwelekeo kwamba kila mwenye dhamana asimame kwenye nafasi yake na kutimiza wajibu wake kwa umma.

4.       HAKI ZA RAIA

Mstari umechorwa hapa. Mheshimiwa Rais. Samia Suluhu Hassan amekataza kwa msisitizo ubambikiziaji wa makosa kwa wananchi, amekemea utaratibu wa baadhi ya watumishi wa dola kufungua kesi za uongo kwa sababu mbalimbali. Pia ameviasa vyombo vya Dola kuhakikisha haki inatolewa kwa wakati, suala la kufungua kesi ili kuleta usumbufu kwa watu Fulani ama kuwashughulikia wanaharakati mbalimbali amesema hilo lisiwepo kwenye serikali ya Awamu ya Sita.

Ameiasa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutosumbua wafanyabiashara ama kuwabambikizia makosa ya Kodi. Tumeshuhudia kesi nyingi zinazohusiana na masuala ya Kodi kwa jina la uhujumu uchumi zikifunguliwa dhidi ya wawekezaji na wafanyabiashara mbalimbali.

Plea bargain imetungiwa sharia inayomruhusu Mwendesha Mshtaka DPP kufanya Trade Deals na watuhumiwa mbalimbali kwa ajili ya kununua uhuru wao.

Wakati akizindua kiwanda cha ushonaji cha Polisi hapo dar es Salaam, rais SSH aliwaambia polisi kwamba, wasigeuze sheria za Barabarani kama chanzo cha mapato. Lengo la sheria ni kurekebisha tabia na siyo kujipatia kipato. Hili tumeliona pia kwenye Bajeti ya 2021/2022 iliyowasilishwa Bungeni kushusha kiwango cha faini ya makosa ya barabarani kwa vyombo vya pikipiki na bajaji kutoka tshs 30,000/- hadi Tshs 10,000/- kwa kila kosa. Lakini kwenye hili jukumu la Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama Barabarani ni kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara kwa minajili ya kupunguza makosa na ajali za barabarani.

5.       UWEZESHAJI MAKUNDI MAALUMU

Katika hotuba yake kwa Taifa ya tarehe 08/06/2021, Rais Samia Suluhu ametaka mifuko ya uwezeshaji makundi maalumu ifanyekazi kwa weledi. Asilimia 10% ya mapato ya Halmashauri zetu inatakiwa ionyeshe tija kwa walengwa na isitumike kama nyenzo za kisiasa.

Rais ameenda mbali zaidi kwa kuelekeza Mfuko wa Rais wa Kujitegemea uanze kuandaa mpango wa kuyawezesha makundi haya maalumu kujikwamua kiuchumi. Makundi lengwa ni Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu.

Katika Tanzania ya Uchumi wa Viwanda, ni budi juhudi za kuhakikisha ukuaji wa mitaji ya wawekezaji wa ndani iendane sambamba na Diplomasia ya Uchumi kama atakavyo Rais. Bidhaa za viwandani zinapozaliwshwa zinahitaji wagavi wenye uwezo kimtaji kuliingia soko la ndani nan je. Hivyo juhudi za Rais zinaenda kusaidia ukuaji wa mitaji kwa wazalishaji na wawekezaji wa ndani ili kuweza kwenda sambamba na mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo serikali imeyaweka

Tukikaribia siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan, wadadisi wa Siasa wameanza kuona muelekeo mzuri wa Siasa za Mama.

Inawezekana kabisa, wahafidhina waliopo ndani ya CCM wasione kama hizi hatua anazochukua Rais SSH zina mwelekeo mzuri kwao. Lakini ni hatua kubwa sana kwa maana ya nchi kusonga mbele.