Guest Column: Maoni Ya Mdau Kwako Mama Samia Kuhusu Passport, Kodi Ya Majengo Na Leseni Za Magari

Kolamu ya mgeni ina makala ya mdau huyu

MASWALI YANAYOJIBIKA

Serikali ya Awamu ya Sita imejipambanua kuwa na lengo la kufungua nchi ili iweze kupiga hatia zilizoanzwa kuelekea kwenye uchumi wa kati Nafasi ya juu. Muelekeo huu wa serikali ni muhimu sana ukaangazia maeneo yote ambayo yanaweza kuwa ni vikwazo kwa nchi kufikia huko.

Kuna kero na changamoto ndogondogo ambazo zikishughulikiwa inawezekana kuleta tija kubwa na kumpunguzia mwananchi mzigo wa gharama lakini ikaongeza tija kwenye makusanyo ya serikali.

HATI ZA KUSAFIRIA (PASSPORT)

Kwenye eneo hili inawezekana lengo ni kukusanya mapato na kwa serikali lakini ni eneo linalolenga kuwapatia wananchi wake hati za kusafiria nje ya nchi. Uwekezaji mdogo na mkubwa haukwepi eneo la usafiri. Wafanyabiashara walio wengi wanafanya safari zao kwa lengo la kutafuta bidhaa na masoko.

Utoaji wa Hati za Kusafiria nchini umekuwa ni jambo maaluu ambalo limegubikwa na urasimu mkubwa. Kuna wakati wafanyabiashara wanakata tama kama kweli serikali imedhamiria kuendana na sera yake ya uchumi wa soko. Kipengele cha kwenye maombi ya Hati ya Kusafiria kinachomtaka muombaji ataje sababu ya safari ni kipengele kinachoondoa haki ya Mtanzania kupata Hati ya kusafiria.  Serikali itambue kwamba mtu anapokuwa na hati ya kusafiria anaweza kusafiri muda wowote kwa sababu yeyote halali na ijulikane kwamba hata Wataalam wetu wa sekta na fani mbalimbali wanaweza kuwa ni sehemu ya uwekezaji wa kitaaluma nje ya nchi.

Nashauri eneo hili, serikali iondoe urasimu na kumuwezesha kila Mtanzania mwenye uwezo amiliki hati ya Kusafiria na kusiwepo na urasimu mkubwa kwenye eneo hili

LESENI ZA MAGARI

Baada ya Jeshi la Polisi kuingia kwenye ukusanyaji wa mapato badala ya kusimamia na kutekeleza sharia imeongeza urasimu mkubwa sana kwenye eneo la uendeshaji wa vyombo vya moto. Hivi karibuni Rais Samia Suluhu alielekeza Jeshi la Polisi kujikita kwenye kusimamia sharia ili kupunguza ajali na changamoto za barabarani kuliko kujisifia kuwa inakusanya mapato kupitia faini mbalimbali. Angalizo hili ni muhimu sana liungwe mkono na wapenda maendeleo wote.

Tukija kwenye Leseni za Udereva, kuna mambo kadhaa yanayoleta kero

1.       Gharama za kuchapisha leseni mpya na kuhuisha iliyokwisha muda wake ni Tshs 70,000/- ambapo sharia inayoelekeza hizi gharama haijafafanua kwa nini kitambulisho ambacho utengenezaji wake hauzidi Tshs 10,000/- kinauzwa ghali namna hiyo. Kama inawezekana basi kuomba Leseni isizidi Tshs 30,000/- na kila baada ya muda wa uhai wake kuisha gharama za kuihuisha isizidi 20,000/-.  Napendekeza hivi kwa sababu Serikali ilipaswa kutoa mchanganuo wa gharama badala ya kuwatwisha wananchi wake unrealistic costs kwenye eneo hili. Ikumbukwe Leseni ya Udereva haiwekewi Data Chip hivyo ni materials zake ni PVC cards kwa kiasi kikubwa

2.       Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama wa Barabarani wapewe super computer ili kuingiza leseni zote za udereva zilizotolewa na kuziunganisha na biometric data ili kudhibiti ongezeko la ajali kwa kuwaondoa barabarani madereva waliokubuhu kwenye uzembe wawapo barabarani.

3.       Serikali ikiona vyema iongeze  gharama za Leseni ua Udereva kwenye bei ya mafuta ili iingie kwenye kugharimia leseni kama ilivyofanya kwenye Road Licence kwa kuingiza gharama zake kwenye bei ya mafuta.

KODI YA MAJENGO

Serikali imeonyesha nia njema kabisa kwenye hili eneo kwa sababu ilishusha gharama za kodi za majengo kwa kiwango cha Tshs 10,000/- kwa kila Nyumba ya kawaida na kwa Nyumba za ghorofa Tshs 50,000/- kwa kila floor ya ghorofa. Pamoja na gharama hizi kushuka lakini bado kuna tatizo kwenye elimu na ukusanyaji wa kodi hii.  Kuna mapendekezo kadhaa kwenye hili eneo

1.       Serikali iendelee kuweka gharama ya Nyumba kiwango kile kile kwa sababu pamoja na changamoto zake lakini kinaweza kulipika na wengi. Bado kuna wananchi wengi hawawezi kumudu hizi gharama ambao ni wazee, walemavu na wanaoishi chini ya kiwango cha umaskini. Serikali iainishe aina za Nyumba ambazo zinapaswa kulipiwa kodi na kuwapa msamaha wale wanaobainika kwa sababu zinazoeleweka hawawezi kulipia kodi hizi.

2.       Serikali isitishe kutoza kodi ya majengo kwenye nyumba za biashara. Katika eneo hili itoze gharama ya asilimia 0.7 kwa kila mkataba wa pango na hiyo ilipwe kupitia stamp duty ya TRA kwa uratibu wa TAMISEMI. Wamiliki wengi wa majengo wamekopa kupitia taasisi za fedha hivyo ulipaji wa kodi ukiwa rahisi utasaidia hata wale ambao wanakwepa kulipa kodi kurejea kwenye utamaduni wa ulipaji wa kodi. Mmiliki anayepaswa kulipia gharama hizo ni Yule ambaye jumla ya kodi ya pango anayokusanya kwa mwezi ni zaidi ya Tshs 60,000/-

Maoni haya yanaweza kuwa na tija lakini hayana ulazima wa kuyafuata endapo tija yake haiendani na wakati tulio nao sasa wa mbio za Uchumi wa Soko

Mwandishi ni Mtanzania anayeamini katika uhuru wa maoni na haki ya kuwasiliana

Endapo nawe una maoni unayotaka yachapishwe katika kijarida hiki, usisite kuwasiliana nami.