Guest Column - Kada Wa CCM: Mitego Ya Kisiasa Dhidi Ya Rais (@SuluhuSamia)

Kuna wingu jeusi la kisiasa linakatiza kuifunika Tanzania. Wingu hili lilikuwepo kipindi Fulani hapo nyuma na ikaonekana kana kwamba anga linafunguka na nuru ya uhai kurejea kwenye misingi inayounda Taifa letu. Jemedari wetu ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Mama Samia Suluhu Hassan almaarufu SSH ameingia katikati ya mtanziko wa Kisiasa unaopelekea sintofahamu kubwa ndani ya nchi.

Kupitia Barua ya Chahali, nilijaribu kutumia Nafasi yangu kama mwanaCCM kuelezea hatari ya makada waliomzunguka Rais wetu kujaribu kumuangusha kisiasa ili kundi hilo linufaike. Naweza kuabiri (siyo kutabiri) wingu la kiza lilianzia siku chache kabla ya tarehe 17/03/2021. Kwa wafuatiliaji wengi wa masuala ya kisiasa za Tanzania waliisoma tweet ya Evarist Chahali kwamba Rais Mgufuli amefariki Hospitali ya Mzena Dar es Salaam lakini Makamu wa Rais hajajulishwa…. Walio wengi tuliona hoja hiyo ni utabiri tu usio na uzito mkubwa, lakini Watanzania tulifichwa hali ya kiafya yaani kuugua hadi kufariki kwa Dr. John Pombe Joseph Magufuli. Mhe. Raisi kama ni kweli hili suala la wewe kutojulishwa kifo cha Rais Mtangulizi wako kwa wakati muafaka ni dalili kulikuwa na mpango (ulioshindwa) wa uhaini dhidi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa utangulizi huo, naweza kusema kwamba kundi la baadhi ya wasiokutakia mema ndiyo hao hao waliopo kulia na kushoto kwako. Inawezekana wataalam wa kukusanya taarifa na kuchakata ni sehemu ya kundi hilo kwani taasisi unayoiongoza imekamilika na inaishi kwa weledi mkubwa. Lakini kuna uwezekano ukawa unaishi na Black Pope ndani ya Taasisi yako.

Mitego ya awali

1.      Baada ya Kuapishwa ulipaswa kuunda Serikali, lakini inaonesha ushauri wa kufanya mabadiliko madogo ya Baraza la mawaziri bila kulivunja na kuliunda upya.

2.      Kutomteua DGIS mpya, inaonesha ushauri huu au maamuzi haya yametokana na ukweli ulikuwa kwenye Nafasi ya Makamu wa Rais hivyo mambo yanaweza kuwa kama hapo awali.

3.      Teuzi za wakuu wa Mikoa na Maafisa Tawala, ni kwamba siku chache baada ya teuzi hizo ulikuja kugundua baadhi hawakupaswa kurudishwa kwenye Nafasi hizo akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza akitokea Mbeya.

4.      Mara  baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa ulifanya mabadiliko ya Kamati Kuu na Sekretarieti ya Taifa ya Chama ambapo uliwaweka makada ambao tuna imani kuwa watakuwa msaada mkubwa kwa Chama na Oganaizesheni zake. Ingawa tangu umemteua Katibu Mkuu Wa Chama Komredi Chongolo inaonekana anashindwa kuimudu nafasi yake kutokana na kutoonekana kuwa kamisaa wa Siasa hasa kipindi hiki ambacho makada wengi wamejitokeza kukosoa sera zako wazi wazi

5.      Bajeti ya Serikali 2021/2022 kupelekwa Bungeni huku ikiwa na pendekezo la Tozo mpya za watumiaji wa miamala ya simu za mkononi

6.      Waziri wa Katiba na Sheria kuwa kimya ghafla kuweka sawa hoja ya Katiba Mpya huku CCM ikikuachia jukumu la kujibu hoja za Katiba Mpya kwa kutofanya uenezi kuhusu agenda ya Katiba Mpya.

7.      Mfumuko wa bei wa bidhaa muhimu kwa maisha ya wananchi bila kupatiwa ufumbuzi wa kudumu

8.      Spika wa Bunge kuonesha mwenendo wenye mashaka kwenye suala la Tozo la Miamala.

9.      Kufufua mashtaka ya Ugaidi dhidi ya Mbowe jambo ambalo lilitakiwa kufanyiwakazi tangu Julai 2021.

10.   Kuendelea kwa makundi ndani ya CCM ambayo yameanza kuungana dhidi yako kwa lengo na manufaa ya makundi hayo na siyo kwa CCM na serikali kwa jumla

Nimekutajia baadhi ya maeneo ambayo yanaonekana kwa wazi huku kwetu kwa wananchi. Lakini sisi wananchi tunaamini kwamba yawezekana kuna mengi ya chinichini yanaendelea ili kuhakikisha unakwama katika juhudi zako kuliletea maendeleo Taifa letu

Mheshimiwa Rais haya ni mapendekezo kwako na wasaidizi wako ili kama yanaweza kusaidia yatumike kuipeleka nchi kwenye Uchumi wa Kati wa Juu na kurejesha utulivu, amani na mshikamano kwa nchi yetu

1.      Haujachelewa kuvunja Baraza la Mawaziri

2.      Suala la wakuu wa vyombo vya Ulinzi lifanye kwa Busara kubwa. Tunapenda kuiona nchi yetu inapanua wigo wa Kiintelejensia na ulinzi unaoendana na hali ya sasa ya Dunia bila kusahau misingi ya tulipotokea.

3.      Mheshimiwa Rais, kuna watu wameumizwa, kupotea ama kupata athari zitokanazo na baadhi ya watu ndani au nje ya Serikali waliokuwa na lengo la kuichafua serikali kwa watu wake. Jambo hili itafaa sana endapo utaunda Tume ama Kamati ya Upatanisho ya Kitaifa itakayokaa na kusikiliza pande zote zilizoathirika na ikiwezekana kuwafikia wahusika na ipewe hadidu za kuchungua uzito wa athari kwa wananchi na Serikali ili itoe ushauri.

4.      Kuna wawekezaji wazawa na pia wapo watumishi wa Umma waliokimbiza kuficha pesa nje ya nchi. Yatengenezwe mazingira ya win win ili kuwawezesha kurudisha pesa nchini na kufanya miradi ya uwekezaji yenye tija na malengo marefu kwa uchumi wetu. Vita ya kuwabana warudishe tutakuwa hatujatatua tatizo. Tufute makosa, tuanze upya lakini kukiwa na utaratibu wa kisheria unaotekelezeka kuzuia utoroshwaji wa fedha za nchi na ufisadi.

5.      Amani ya nchi inategemea sana mshikamano wa raia wan nchi. Serikali ilinde ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka sharia zinazotunza uzalendo na uhuru wa kutoa maoni

6.      Mheshimiwa Rais, kuna mengi ambayo kikawaida wasaidizi wako hawakuambii ukweli. Nao ni kupungua kwa kuungwa kwako Mkono ngazi ya wananchi ambao ndiyo mtaji wa Kura. Viongozi wachache waliopamoja nawe hawafikii turufu ya kura unazopaswa kuzilinda kupitia utendaji wao.

7.      Suala la Tozo la miamala ni jambo ambalo linaumiza sana uchumi binafsi wa watu wa chini, wanalipa kodi stahiki kwa kila muamala lakini ongezeko la Tozo lisilozingatia uhalisia ni kupingana na kauli uliyoitoa wakati wa Kuapisha Mawaziri na wakuu wa Mamlaka za serikali kwamba Serikali yako haitovumilia hukusanyaji wa kodi kupitia pato la dhuluma, ikikupendeza tunaomba Tozo la Miamala lisizidi Tshs 100 kwa kila muamala ilasaidia kupunguza mkwamo lakini wananchi watajionea ufahari kulipa tozo hili.

8.      Anzisha utaratibu wa TIJA (productivity) kwa watumishi wa umma na wateule wako. Nchi ni kampuni kubwa ya wote, kila mtu awajibike kwenye eneo lake. Lakini bila usimaizi wa karibu tena wa kisheria husababisha kila mtumishi kufanyakazi bila kuwajibika na kuonesha matunda ya kazi zake.

9.      Serikali ache kuwawinda Watanzania ambao wamekimbia nchi kwa kuhofia maisha yao kudhuriwa.

10.   Asilimia kubwa ya wabunge waliopo Bungeni leo pamoja na Madiwani, walipitishwa kugombea kwa kuacha mpasuko mkubwa ndani ya chama, tiba inahitajika kuhakikisha CCM inaingia 2025 ikiwa moja

Mheshimiwa, ninaamini kwamba umeshapokea maoni mbalimbali, kupitia nafasi hii nimetimiza wajibu wangu kutoa maoni.

Mtoa maoni ni mwanachama wa CCM