Guest Column: Dear Mama Samia, Ujumbe Kutoka Kwa Kada wa Chama Chenu: "CCM Tujisahihishe au Watanzania Watatusahihisha."

Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Miaka 22 imepita sasa tangu Baba wa Taifa atutoke, Tanzania imeendelea kuwepo na hakika itaendelea kuwepo sana. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa rais wa kwanza wa Taifa letu aliacha hazina ya maongozi na mawazo chanya yenye kusaidia kulibeba Taifa letu katika nyakati zote hata zile ngumu zitakazotujia mbele yetu. Watanzania wengi wanakumbua usia mbalimbali alizotoa Hayati Baba wa Taifa kuhusu Uongozi, Maadili na Utu kwa wale wote wanaofikiria ama kujipanga kuingia kwenye hatamu za kuongoza taifa la Tanzania

Awamu tano zimepita tangu Tanzania bara ipate uhuru wake 1961 ingawa uhuru huu leo umefikia kuhojiwa na kizazi kinachoamini bado Tanzania haijaufikia uhuru kamili. Kuna maeneo mawili makuu yanayotasinifu mapungufu ya uhuru wetu

1.      Uhuru wa kiuchumi ambapo badala yake tunao uhuru wa kujiamulia mambo yake ya ndani ilihali maagizo yaambatanayo na mashinikizo yanatoka kwa waliokuwa wakoloni wa Afrika

2.      Uhuru wa wachache kufanya maamuzi yanayoathiri wengi bila kuzingatia kanuni za utawala bora (hapa Chama cha Mapinduzi kinanyooshewa kidole)

Rais wa Awamu ya Tano Hayati John Pombe Joseph Magufuli (JPM) alipata kusema mara nyingi kwamba Tanzania inapaswa kuendesha vita vya kujikomboa kiuchumi ambapo rasilimali na maliasili za Afrika ziwanufaishe wananchi na siyo kikundi cha viongozi wachache kama ilivyo kwa nchi nyingi za Afrika. Tumeshuhudia sehemu kubwa ya nchi za Afrika ambapo rasilimali na maliasili zimewanufaisha viongozi na siyo ilivyotarajiwa. Hali hii imeanza kuinyemelea Tanzania kwani upo ushahidi mbalimbali wa kimazingira wa viongozi wa serikali na CCM kujilimbikizia mali za umma. Haya yote yanaitwa ni mapito ya nchi kuelekea kwenye uhuru wa kweli, kwani tabaka la watawaliwa wakishapoteza imani dhidi ya tabaka la watawala hutumia silaha yao ya sanduku la kura kuwaadabisha na kuweka uongozi mwingine. Kuna kila dalili hili limewahi kukaribia kufanyika lakini liliepushwa baada ya CCM kufanya maamuzi magumu ya kujisahihisha kuelekea kwenye chaguzi kuu zilizopita.

Machi 19, 2021 Tanzania ilipata pigo kubwa kwa kuondokewa na Rais aliyekuwa madarakani Hayati John Pombe Joseph Magufuli, baada ya kifo chake Tanzania ikapata rais wa kwanza Mwanamke ambapo aliyekuwa Makamo wa Rais kipindi hiko Mhe. Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya Ulinzi na Usalama. Hatimaye CCM ikapata Mwenyekiti wa kwanza wa Taifa ambaye ni Mwanamke.

Chama Cha Mapinduzi kimepitia kwenye nyakati tofauti za kimaongozi ambapo umaarufu wake umekuwa ukipanda na kushuka mara kwa mara. CCM kimewahi kufanya makosa kadhaa hapo nyuma hata kupelekea hayati Baba wa Taifa kutoa kitabu chake cha TUJISAHIHISHE akilenga kufanyika mageuzi makubwa ndani ya mfumo wa CCM kiweze kuondokana na athari zilizosababisha chama kiyumbe nyakati zake. Leo hii katika Awamu ya Sita ya uongozi wan chi yetu, Chama Cha Mapinduzi kinapitia kwenye mtikisiko mkubwa unaotokana na vita vya uongozi ndani ya Chama na Serikalini. Chama hiki ambacho kimekuwa tanuru na kupika na kuandaa viongozi wake na serikali kimefikia hatua ya kuokoteza makada kutoka vyama pinzani ili kupata viongozi wa kiserikali ngazi mbalimbali. Kwa nini CCM imefikia hapo? Jibu halipo mbali nalo ni siasa za makundi. Tangu kuasisiwa siasa za makundi na kupewa nguvu kubwa ndani ya Awamu ya Nne, CCM imeshuhudia mtifuano mkubwa ambao ulifikia kiwango cha juu cha kuchafuana baina ya makada waandamizi wa Chama Cha Mapinduzi hivyo kuzaa Siasa za Kubebana  bila kuzingatia misingi na miiko ya uongozi. Chama kimeshuhudia ongezeko kubwa la Rushwa kipindi cha uchaguzi za ndani ya Chama.

Awamu ya Tano ya Uongozi wan chi yetu tumeshuhudia pia Chama Cha Mapinduzi kikigeuka kuwa Chama Imla kwa kuhakikisha kinatumia mbinu zote safi na zisizo safi kuendelea kushikia mamlaka ya dola ya nchi yetu. Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na vitongoji mwaka 2019 uligubikwa na sintofahamu nchi nzima ambapo ilipelekea CCM kuchukua ushindi zaidi ya asilimia 98%  nchi nzima. Jambo hilo hilo likajirudia tena ambapo kwenye uchaguzi mkuu 2020 CCM ilijirundikia ushindi mkubwa zaidi ya asilimia 90% ya Wabunge, Madiwani na hata ushindi wa kiti cha Urais ushindi ulikuwa mkubwa sana. Suala hili halikufanyika kwenye chaguzi kuu pekee bali hata chaguzi za uteuzi wa wagombea ndani ya CCM uligubikwa na sintofahamu kubwa kupelekea malalamiko mengi ya makada na wagombea mbalimbali ambao waliona taratibu hazikufuatwa. Ubabe uliotumika kupitisha wagombea ndani ya Chama na hata kupelekea kujipatia ushindi wenye shaka kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020 ni dalili ya wazi kwamba demokrasia imekuwa ni jambo linaloepukwa na kada za uongozi ndani ya Chama.

Kwa nini CCM ijirekebishe

Chama Cha Mapinduzi ni miongoni mwa vyama vikuu vichache havizidi kumi ndani ya Afrika, vilivyopambania Uhuru wa Nchi zao na bado vipo madarakani. Nasema havizidi kumi nikimaanisha vinaweza visifike hata vitano. Sababu kubwa ya vyama vyingi vikubwa kuanguka ni pale ambapo maslahi binafsi ya watawala na vyama hivyo kuamua kuwa juu zaidi ya maslahi ya nchi na wananchi wake. Baada ya Uhuru CCM enzi hizo kikiitwa TANU kilijikita kwenye kuhamasisha ujenzi wan chi na Uzalendo. CCM ilisubirisha maendeleo ya nchi ili kuwekeza nguvu na mikakati ya kuifanya Afrika yote iwe uhuru na kujitawala. Ukiangalia uasisi wa Umoja wa Afrika, Chama Cha Mapinduzi kimeshiriki kwa nafasi kubwa hata kutumia ardhi ya Tanzania kuwa sehemu ya wapigania Uhuru wa Afrika walio Mstari wa Mbele. Historia nzuri na makini ya CCM imefunikwa na hulka za namna makada wake wanavyopambania madaraka ndani ya chama mpaka serikalini. CCM imefunika kisima cha fikra kupitia UVCCM hadi kufikia kuitwa Wabeba Mabegi, CCM imejibananisha na Dola yaani watumishi wa Dola ambao kikatiba na kisheria hawapaswi kufungamana na siasa wamejikita kwenye ndoa ya siri (ambayo sasa imekuwa wazi) na CCM. Intelejensia ya Serikali imefikia mahala kufanya kazi za CCM jambo ambalo ni hatari kubwa kwa demokrasia ya Taifa.

Chama Cha Mapinduzi kimefikia mahala ambapo yeyote anayekikosoa anaandamwa hata maisha yake kuwa hatarini kwa sababu anakosoa mambo ambayo wenye mamlaka wanachukia kuyasikia. Kuna Watanzania wengi wameuawa hata kupata ulemavu ama kwenda ukimbizini kuhofia maisha yao kuwa hatarini. Chama chetu kimekuwa kikipiga wimbo wa kuunga mkono kila jambo linalopitishwa na watawala bila kuangalia athari za maamuzi hayo kwa wananchi kwa ujumla. Hivyo tumefikia eneo ambalo naweza kusema tumetiwa upofu na uziwi tukiamini tutaendelea kuiongoza nchi hii milele yote.

Baba wa Taifa wakati anang’atuka kwenye uenyekiti wa Taifa wa chama alisema “Bila CCM Imara, nchi itayumba”. Na hili limeshaanza kujidhihirisha sasa kwani hatua zote ambazo CCm imezitumia kupata madaraka ya nchi zimeacha SONONEKO kubwa sana ndani nan je ya Chama

Nini Kifanyike?

Kwa minajili ya kujenga, kuna maoni machache yanayoweza kuchakatwa kupata mwelekeo

1.      Chama kijitathmini kuanzia ndani ili kupima uwezo wake kwenye siasa za kisasa ambazo zinalenga kutatua matatizo mtambuka ya wananchi na kisekta

2.      CCM ina dhima kubwa kujenga demokrasia nchini kwa kuasisi uwiano sawa wa kufanya siasa kwa vyama vyote bila kuweka mikingamo yoyote

3.      Kutenganisha Dola na Siasa kivitendo. Hili suala litawezekana endapo Katiba iliyopo ikatekelezwa kikamilifu na kama kuna ugumu ielekeze serikali kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya kama nyaraka wakfu ya wananchi na serikali

4.      CCM iielekeze serikali kuunda tume ya Upatanisho na Maridhiano ili kujenga upya mshikamano na udugu baina ya Watanzania

5.      CCM itumie uzoefu uliopo kwenye kada za chini za Chama na Serikali ambapo Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji, Madiwani na Wabunge hawaruhusiwi kugombea nafasi za uongozi ndani ya Chama, hivyo kwenye ngazi ya Taifa hilo lifanyike ili kuweka uwiano mzuri na muafaka wa kuisimamia serikali na kuasisi chama.

Kwa maoni na mapendekezo hayo machache naamini upo uwezekano mkubwa kwa CCM kuendelea kushika hatamu za nchi hii kwa zaidi ya miaka 100 ijayo kwa sababu itakuwa imeonesha kivitendo kujali na kuheshimu matarajio na matamanio ya wananchi.

CCM ikirudisha imani yake ya awali kwamba Tanzania na Watanzania wana nafasi ya kwanza kwenye kila kitu basi itaimarika na kuishi mioyoni mwa wapigakura  kwa muda mrefu sana. Bila kufanya hivyo upo uwezekano mkubwa wapigakura wakaisahihisha CCM kwa kuiweka pembeni na kuchagua chama kingine kuongoza dola.

Nimetumia haki yangu ya Kikatiba ya Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa maoni yangu.

Mwandishi ni mwanachama hai wa CCM