

Discover more from Barua Ya Chahali
UJASUSI (espionage) ni nini? Na MAJASUSI (spies) wanafanya kazi gani hasa? [Sehemu ya Tatu: Aina za Ujasusi]
Hii ni makala ya tatu katika mlolongo mrefu wa makala mbalimbali zinazohusu taaluma ya intelijensia. Huenda baadhi ya makala hizi zikazaa vitabu huko mbeleni kama ambavyo makala kuhusu “Afisa Usalama wa Taifa ni Mtu Gani? Na Anafanya Nini?” zilivyopelekea kitabu bora kabisa chenye jina hilo.
Makala/Sehemu ya kwanza ilihusu maana ya neno UJASUSI. Ni vema ukasoma sehemu ya kwanza na ya pili kabla ya kusoma sehemu ya tatu.
Makala ya pili ilihusu historia ya ujasusi
Makala hii ya tatu inahusu aina za ujasusi. Hata hivyo, kabla ya kuingia kwa undani, ni vema kujikumbusha kuwa mpangilio wa mada zinazounda mfululizo wa makala hizi, ambao ni kama ifuatavyo
ambao ni kama ifuatavyo:
👉Maana ya ujasusi
👉 Historia ya Ujasusi
👉 Aina za Ujasusi
👉 Ujasusi kama nyenzo ya diplomasia
👉 Tofauti kati ya Ujasusi na Uafisa Usalama wa Taifa
👉 Majasusi wanapatikanaje?
👉 Majasusi kazini
👉 Changamoto zinazoukabili ujasusi/majasusi duniani
👉 Changamoto za ujasusi/majasusi Tanzania
👉 Mashirika maarufu ya ujasusi duniani na majasusi maarufu duniani.
“Aina za ujasusi”
Pengine umewahi kusoma kitabu sehemu fulani, na kikakueleza kuwa kuna ujasusi wa aina mbili au pengine tatu. Kwamba kuna “ujasusi wa kidola” na “ujasusi wa kiuchumi”. Ukweli ni kwamba huo mgawanyo huo wa aina za ujasusi sio tu ni finyu bali pia unapotosha hali halisi. Lakini hili sio la muhimu kwa sasa, tutalitupia jicho huko mbeleni.
Si rahisi kuwa na “aina za ujasusi” kavukavu. Hapa inamaanisha kwamba ili kubainisha aina za ujasusi, kuna vitu vingine vinavyopaswa kuangaliwa ili kuweza kutofautisha “aina za ujasusi”.
Lakini kabla ya kuingia huko, ieleweke tu dhamira ya msingi ya kufanya ujasusi ni kupata taarifa. Jinsi gani taarifa hiyo inapatikana, nani anahusika/nini kinahusika kupata taarifa husika, na maswali kama hayo hayabadili ukweli kuwa bidhaa muhimu katika ujasusi ni taarifa za kiintelijensia.
Ujasusi: wana-dola (state actors) na wasio wana-dola (non- state actors)
Kama ilivyoelezwa kwa kina katika sehemu ya pili wa mfululizo wa makala hizi za ujasusi, katika asili yake, ujasusi ulikuwa shughuli iliyohusiana na watawala kwa namna moja au nyingine. Hata katika habari zinazopatikana kwenye Kurani Tukufu na Biblia Takatifu, kuna uhusiano mkubwa kati ya ujasusi na utawala.
Na katika kupanuka kwake karne kadhaa zilizopita hadi zama hizo, ujasusi sio tu unahusiana zaidi na watawala kwa maana ya dola bali pia hisia za watu wengi kuhusu shughuli hiyo ni kwamba inafanywa kwa mujibu wa matakwa ya watawala.
Naam, kwa miaka mingi, shughuli za intelijensia ikiwa ni pamoja na ujasusi zilikuwa zikifanywa na tawala. Na ilipofika nyakati ambapo taasisi za intelijensia ziliundwa rasmi, nazo zilikuwa mikononi mwa watawala.
Katika hali hii, ujasusi ulikuwa na unaendelea kuwa shughuli inayofanywa na dola kupata taarifa za dola nyingine. Kwa lugha rahisi, ni shughuli inayofanywa na taasisi ya kiintelijensia ya nchi flani kusaka taarifa za taasisi za kiintelijensia za nchi nyingine.
Lakini kama ilivyoelezwa katika sehemu ya pili kwamba baadhi ya waliojihusisha na ujasusi walikuwa ni wafanya biashara waliouza taarifa hususan za kibiashara, kadri miaka ilivyokwenda ndivyo ambavyo shughuli hiyo ilitanuka zaidi ya kuwa kwenye miliki ya watawala pekee.
Maendeleo katika nyanja mbalimbali yalilazimisha ujasusi kufanywa na taasisi zisizo za dola lakini kwa njia zilezile zinazotumiwa na vyombo vya dola. Na pengine zaidi.
Kurahisisha, moja ya “aina nyingi za ujasusi” ni hii kati ya majasusi “wana-dola” (state actors) na majasusi “wasio wana-dola”.
Bila kuingia kwa undani sana, mgawanyo huu hapa unahusu “katumwa na nani?” au “anafanya kazi za nani”.
Majasusi “waliozoeleka” ni wale wanaofanya kazi kwenye Idara za Usalama wa Taifa za nchi husika. Na japo kwa kiasi kikubwa maeneo makuu yalihusu siasa za kimataifa na/au diplomasia na masuala ya kijeshi, uchumi pia ulikuwa ni miongoni mwa vipaumbele.
Hata hivyo, ujio wa “majasusi wasio wana-dola” ulianzia zaidi kwenye masuala ya kiuchumi. Majasusi waliowahi kufanya kazi katika Idara za Usalama wa Taifa za nchi mbalimbali walishawishiwa kutoka kwenye kustaafu ili ujuzi wao katika ujasusi utumiwe na taasisi binafsi.
Makampuni makubwa yanatumia kiwango kikubwa cha fedha kwenye ujasusi katika masuala ya biashara. Kinachowindwa ni kilekile - taarifa za siri kuhusu hili au lile.
Mantiki ni ileile iliyoelezwa huko nyuma kuhusiana na ujasusi, kwamba ili kuwa katika nafasi nzuri, ni muhimu kufahamu nini kinaendelea kwa adui. Sasa kwenye masuala ya biashara, kampuni zenye ushindani ni lazima zielewe mwezie anafanya nini. Na kama ilivyo kwenye masuala ya kidola, taarifa muhimu za biashara huwa siri. Kwahiyo ili kuzipata inalazimu wanaozihitaji watume watu wao “kuiba” taarifa hizo kwa njia mbalimbali kama zitakavyotanabaishwa kwenye sehemu inayohusu jinsi gani ujasusi unafanyika.
Siri za biashara (trade secrets) ni “bidhaa” muhimu kabisa katika ujasusi unahusiana na masuala ya biashara
Ujasusi wa viwandani (industrial espionage), ujasusi wa mashirika (corporate espionage), ujasusi wa uchumi (economic espionage)
Ujasusi wa mashirika (corporate espionage) ni ujasusi unaofanywa kwa madhumuni ya kibiashara au kifedha. Ujasusi huu pia unajulikana kama ujasusi wa viwandani, ujasusi wa kiuchumi au ujasusi wa kampuni.
Mara nyingi ujasusi wa kiuchumi unaratibiwa na serikali na ni wa kimataifa katika upeo, wakati ujasusi wa viwanda au ushirika kwa ujumla hufanyika kati ya mashirika. Hata hivyo, mstari unaotenganisha au kutofautisha vitendo hivyo sio tu ni mwembamba bali pia huingiliana.
Kwa mataifa ambayo makampuni mengi makubwa humilikiwa na serikali, ujasusi unaofanywa na makampuni hayo huhusisha majasusi wa serikali pia. Kimsingi, kwa sababu makampuni hayo huwa mhimili muhimu wa uchumi kwa mataifa hayo, nchi husika hulazimika kuyasaidia makampuni kama hayo kwa sababu uhai wake ni uhai wa taifa pia. China ipo mstari wa mbele katika eneo hili kama itakavyoelezwa kwa kirefu katika makala zijazo.
Hadi kufikia hapa, “aina za ujasusi” zimejitanabaisha kwa nani anahusika kuliko nini kinafanyika - kwa sababu kuna sehemu maalum huko mbeleni unayozungumzia ujasusi unavyofanyika.
Binadamu vs teknolojia
Pasi mjadala, intelijensia inayokusanywa na binadamu, inayofahamika kama human intelligence kwa kifupi HUMINT sio tu ndio kongwe zaidi lakini pia ni ya kuaminika zaidi. Na katika ujasusi pia, nafasi ya binadamu katika kufanikisha operesheni za kijasusi ni kubwa kupita maelezo.
Kwa kawaida, kuna njia mbili za kijasusi katika kupata taarifa za mlengwa. Ya kwanza ni kwa kumtumia mtu - aidha jasusi aliyetumwa kwenda nchi lengwa au kwa kutumia watu waliopo sehemu nyeti wanaoweza kusaliti nchi yao na kutoa siri husika. Sehemu husika huko mbele itaeleza jinsi gani mambo haya yanafanyika.
Njia ya pili ni kwa kutumia teknolojia. Hata hivyo, yayumkinika kusema kuwa hakuna teknolojia inayojiendesha yenyewe kwa asilimia 100 bila binadamu kuhusika. Pengine ujasusi unafanyika kwa kutumia vijindege vidogo visivyo na rubani (drones). Lakini ili drone ifanye kazi kwa ufanisi, lazima iwe na “rubani” aliyeshikilia rimoti kuiongoza. Na drone hiyo ikishakusanya taarifa kusudiwa, ni afisa (mwanadamu) atakayefanya uchambuzi.
Maendeleo ya teknolojia yamekuwa ni habari njema na mbaya kwa intelijensia. Habari njema kwa sababu kwa kiasi kikubwa, teknolojia kama ya intaneti imesaidia kuongeza udhaifu wa watu (vulnerability).
Kwa mfano, mtandao wa kijamii wa instagram umekuwa na ufanisi sana kwa mashirika ya kijasusi “yanayojielewa” ambapo huwatumia mabinti warembo kama “chambo cha kuwanasa maafisa usalama wa nchi nyingine”. Kwa bahati mbaya - au pengine makusudi - maafisa wengi tu wa Idara ya Usalama wa Taifa ya Tanzania wameangukia katika mtego huu. Tatizo ni mchanganyiko wa tamaa za ngono (aka kushindwa “kudhibiti zipu”) na kasumba hatari ya kujitangaza. Binti aliyetumwa na majasusi hawezi kumjua afisa wa Idara ya Usalama wa Taifa ya Tanzania kama afisa huyo atahifadhi utambulisho wake. Lakini imeshakuwa kama jambo la kawaida kwa baadhi ya maafisa “kutumia vitambulisho vyao vya kazi kwa ajili ya kutongozea kwenye mitandao ya kijamii.”
Kibaya zaidi, yawezekana hata huyo anayetongozwa si mwanamke bali ni jasusi anayetumia utambulisho feki kama mwanamke.
Kwahiyo, kwa upande mmoja teknolojia inawarahisishia kazi majasusi katika baadhi ya nyakati lakini pia inaleta changamoto, kwa mfano kama hizo za watumishi wasio na maadili “wanaojiumbua” kirahisi kwenye mitandao ya kijamii. Kiintelijensia, kujiumbua ni kufanya kitu kwa bahati mbaya au makusudi ambacho kinaishia kuweka wazi utambulisho unaoficha.
Na teknolojia kama ya mitandao ya kijamii inatumiwa pia “kuwaumbua” watumishi wa Idara za Usalama wa Taifa za nchi mbalimbali. Miezi michache iliyopita, Idara ya Usalama wa Taifa ya Ukraine iliweka hadharani majina ya majasusi takriban 300 wa Urusi waliokuwa wakifanya kazi sehemu mbalimbali za bara la Ulaya. Mara baada ya “kuumbuliwa”, nchi kadhaa za Ulaya ziliwatimua “maafisa ubalozi wa Urusi”. Kwa nchi nyingi, “maafisa ubalozi” huwa majasusi.
Kwa bahati mbaya - au makusudi - balozi zetu zimejaa ndugu na jamaa za vigogo badala ya majasusi. Lakini pengine katika hilo itakuwa ni kuwaonea bure wahusika kwa sababu ili mpeleke majasusi kwenye balozi zenu shurti muwe nao, na kwa bahati mbaya - au makusudi - Tanzania inakabiliwa na uhaba mkubwa wa watu hao. Hilo litaongelezwa kwa kirefu kwenye sehemu inayohusu ujasusi nchini Tanzania.
Maendeleo ya teknolojia pia yameibua fursa na changamoto ya udukuzi. Ni fursa kwa sababu, kwa mfano, wakati wa utawala wa Rais Magufuli, aliomba msaada kwa kampuni moja ya udukuzi ya Israeli, na wakamsaidia kuzidukua simu za wakosoaji mbalimbali wa serikali ambao hawakuwepo Tanzania. Udukuzi unasaidia kwa kiasi fulani kuondoa haja ya kumtuma jasusi akanase mawasiliano ya mlengwa.
Lakini udukuzi pia ni changamoto kwa sababu taasisiyoyote ile inaweza kudukuliwa. Moja ya idara za usalama bora kabisa duniani, NSA, ambayo pamoja na mambo mengine inahusika na - guess what? UDUKUZI - ilidukuliwa.
Na udukuzi huo haukufanyika kwa siku, wiki, mwezi au mwaka mmoja. Inaaminika ulikuwa endelevu kwa takriban miaka 20. Bila kuingia kiundani kwenye hilo, huu ni mfano wa jinsi teknolojia kama udukuzi inavyoweza kuwa fursa kwa nyakati flani lakini pia ikawa changamoto kwenye nyakati nyingine.
Magaidi na teknolojia
Moja ya majanga yanayohofiwa sana ni pindi “teknolojia hatari” zitapoangukia mikononi mwa magaidi. Kwa sasa, vikundi vya kigaidi kama Islamic State na matawi yake na Al-Qaeda vimekuwa mstari wa mbele katika matumizi ya teknolojia angalau kufikisha ujumbe kwa watu kusudiwa. Baadhi ya programu tumizi (apps) za simu kama vile Telegram zimekuwa nyenzo muhimu kwa magaidi kufanya mawasiliano yao.
Japo hadi wakati huu hakuna kikundi cha kigaidi kilichofanikiwa kufanya shambulizi la kigaidi kwa kutumia teknolojia (cyberterrorism), ni siri ya wazi kuwa vikundi vya kigaidi vinahangaika kwa udi na uvumba kupata uwezo wa kufanya mashambulizi kama hayo.
Ujasusi wa kimtandao (cyberespionage)
Katika miaka ya hivi karibuni, udukuzi umekuwa ni nyenzo muhimu sana katika kufanya ujasusi. Na ujasusi wa kimtandao umejenga uhusiano kati ya taasisi za kijasusi na makundi binafsi ya wadukuzi. Kama itakavyotanabaishwa kwenye makala husika, Urusi, China, Korea ya Kaskazini na Irani ni mataifa yaliyo mstari wa mbele katika “ushirika usio mtakatifu” kati ya Idara za Ujasusi za nchi hizo na wadukuzi binafsi.
Na kwa kutambua fursa zilizopo kwenye “sekta” hiyo, baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakijihusisha na uendeshaji wa makampuni ya udukuzi ambayo hatimaye yakidhihirisha uwezo wake huishia kupata tenda za serikali mbalimbali.
Mmiliki wa jeshi la mamluki la Wagner Group la Urusi, Yevgeny Prigozhin, anamiliki kampuni kubwa ya udukuzi ambayo imekuwa ikitumiwa na serikali ya Rais Vladimir Putin kufanya ujasusi wa kimtandao.
Makala iishie hapa
Ili kuepusha kuwachosha, ni vema makala hii ikaishia hapa. Mada ya “aina za ujasusi” itakamilika katika makala ijayo ambayo pia itahusu “ujasusi kama nyenzo ya diplomasia.”