[Free Access] UJASUSI (espionage) ni nini? Na MAJASUSI (spies) wanafanya kazi gani hasa? [Sehemu ya Sita: Ujasusi wa kidiplomasia]
Hii ni makala ya sita katika mlolongo mrefu wa makala mbalimbali zinazohusu taaluma ya intelijensia. Huenda baadhi ya makala hizi zikazaa vitabu huko mbeleni kama ambavyo makala kuhusu “Afisa Usalama wa Taifa ni Mtu Gani? Na Anafanya Nini?” zilivyopelekea kitabu bora kabisa chenye jina hilo.
Makala/Sehemu ya kwanza ilihusu maana ya neno UJASUSI. Ni vema ukasoma sehemu ya kwanza na ya pili kabla ya kusoma sehemu ya tatu.
Makala ya pili ilihusu historia ya ujasusi
Makala ya tatu ilihusu aina za ujasusi
Makala ya nne ilimalizia kilichosalia katika sehemu ya tatu kuhusu aina za ujasusi.
Hata hivyo, kabla ya kuingia kwa undani, ni vema kujikumbusha kuwa mpangilio wa mada zinazounda mfululizo wa makala hizi, ambao ni kama ifuatavyo
ambao ni kama ifuatavyo:
👉Maana ya ujasusi
👉 Historia ya Ujasusi
👉 Aina za Ujasusi
👉 Ujasusi kama nyenzo ya diplomasia
👉 Tofauti kati ya Ujasusi na Uafisa Usalama wa Taifa
👉 Majasusi wanapatikanaje?
👉 Majasusi kazini
👉 Changamoto zinazoukabili ujasusi/majasusi duniani
👉 Changamoto za ujasusi/majasusi Tanzania
👉 Mashirika maarufu ya ujasusi duniani na majasusi maarufu duniani.
Ujasusi unavyotumika kidiplomasia
Katika mazingira ya kawaida, diplomasia huoekana kuwa inahusu uwakilishi nje ya nchi kama vile ubalozi pamoja na jitihada za ushirikiano au kutafuta suluhu.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba moja ya majukumu muhimu kwa wanadiplomasia ni wajibu muhimu wa kufuatilia katika vituo vyao vya kazi nje ya nchi na kuripoti na kuripoti.
Je diplomasia inaishia wapi na ujasusi unaanzia wapi? Ni wapi mtu anapaswa kuchora mstari kati ya diplomasia rasmi na ulimwengu wa giza wa ujasusi? "Kila ubalozi duniani una majasusi" anasema Prof Anthony Glees wa Chuo Kikuu cha Buckingham wakati wa mahojiano, mkurugenzi wa Kituo cha Usalama na Stadi za Intelijensia.
Kwa sababu ni kitu kinachotokea siku zote, serikali mbalimbali duniani zipo tayari kufumbia macho kile kinachotokea ndani ya balozi za kigeni. Lakini pia moja ya sababu za kufumbia macho yanayojiri katika balozi za kigeni kuhusiana na ujasusi, ni ukweli kwamba diplomasia hutawaliwa na “nipe nikupe” au “jicho kwa jicho” kwa kimombo wanasema “quid pro quo”. Ukiwatimua maafisa ubalozi wa nchi flani, nchi hiyo nao itawatimua maafisa ubalozi wako.
Majasusi wengi waliopo kwenye balozi za kigeni hufahamika kwa nchi mwenyeji na haswa kwa Idara za Usalama wa Taifa za nchi wenyeji, hususan kitengo cha kupambana na ujasusi - counter-espionage.
Kanuni isiyo rasmi ni kwamba japo majasusi hao waliojivika kifuniko cha uafisa ubalozi wanafahamika kuwa ni majasusi, hawatochukuliwa hatua yeyote hadi wafanye kitu ambacho ni kinyume cha sheria za nchi mwenyeji.
Na kwa hakika, jitihada za kupambana na ujasusi hujikita zaidi katika kuwatambua majasusi wasiofahamika, wale ambao wanaingia nchi ya kigeni bila kujihusisha na ubalozi wa nchi wanayotoka.
Kwa majasusi waliojivika kifuniko cha uafisa ubalozi, Idara ya Usalama ya nchi mwenyeji inajibidiisha kufahamu mtandao wa kijasusi wa jasusi husika.
Japo itaelezwa zaidi kiundani katika makala zijazo, haswa katika kipengele cha jinsi gani majasusi wanavyofanya kazi, lakini kwa kifupi tu, kazi za kiintelijensia hutegemea zaidi mtandao wa watoa habari, na ndio maana Idara nyingi za Usalama wa Taifa duniani huhitaji kuwa na maafisa wachache tu wanaoweza kukusanya taarifa nyingi kupitia mitandao yao ya watoa habari.
Kwa majasusi, kama itakavyoelezwa kwenye makala husika, jukumu la msingi ni kutengeneza mtandao wa watu walio tayari kusaliti nchi zao na kuwezesha upatikanaji wa siri za nchi hiyo.
Hili ni jukumu hatari sana. Lakini pia ni gumu mno.
Licha ya majasusi waliojivika vifuniko vya uafisa ubalozi kuwa wanafahamika kwa Idara za Usalama wa Taifa za nchi wenyeji, bado wanalazimika kufanya jitihada za kutengeneza mitandao ya watu watakaowapatia taarifa za kijasusi. Kimsingi, hata neno “jasusi” kuna nyakati linamaanisha sio afisa usalama wa taifa bali mtu anayetumiwa na afisa wa idara ya usalama wa taifa wa nchi A kwa minajili ya kupata taarifa za nchi B. Rejea makala ya kwanza iliyoeleza maana na neno ujasusi.
Kitengo cha kupambana na ujasusi kitaendelea kuwafuatilia maafisa ubalozi wanaofahamika kuwa ni majasusi lakini kwa vile vile nao wanafahamu kuwa wanafuatiliwa, watajibidiisha kutekeleza majukumu yao ya kijasusi kwa usiri mkubwa. Na ulimwengi wa intelijensia kwa ujumla ni kama mchezo wa kuzidiana kete, kwa maana kila mmoja anamsoma mwenzie na kutegemea kumzidi akili au kutumia mapungufu yaliyopo.
Ujasusi wa Kidiplomasia ni nini?
Ujasusi wa kidiplomasia ni nyenzo ya kupata taarifa. Kuna aina mbili za ujasusi wa kidiplomasia: operesheni za siri (covert operations) na intelijensia. Zote mbili hutokea kwa usiri ili kuepuka kugunduliwa, na kwa hiyo zinahitaji kuzingatia na maandalizi makubwa. Lakini kimsingi, tofauti kati ya aina hizi mbili sio tu ni ndogo bali pia ni ngumu kubainisha.
Operesheni za siri hujumuisha shughuli zinazofanyika katika maeneo mbalimbali ya kimaisha na zile zinazofanyika mtandaoni. Idara za Usalama wa Taifa hutuma majasusi wake kufanya operesheni hizi hasa kwa minajili ya kushawishi nchi ya kigeni.
Operesheni za siri ni za siri kwelikweli, na kwa hakika zipo katika hatua ya juu kabisa ya ujasusi. Operesheni hizi zinaweza kuwa za kutumia mabavu kulazimisha ajenda, kutumia hujuma, wizi, hujuma za kisiasa na propaganda.
Katika aina ya pili ya ujasusi wa kidiplomasia kuna makundi mawili: ukusanyaji wa taarifa za kiintelijensia na uchambuzi wa taarifa hizo. Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, ukusanyaji wa taarifa za kiintelijensia nje ya nchi ni kosa japo ni mpaka ni shughuli pevu kulithibitisha.
Umuhimu
Hata kama nchi ni marafiki, urafiki wao unakuwa wa mashaka kama hazijuani vya kutosha. Lakini wakati nchi zinaweza kuwa marafiki kwa maana ya kuwa na uhusiano mazuri au zenye kushirikiana, kijasusi - na kwa hakika kiintelijensia - kila nchi ni adui, kama si wakati uliopo basi ni wakati ujao, yaani adui mtarajiwa.
Kwahiyo ni lazima kufahamu kinachoendelea katika nchi nyingine. Kwa njia “halali” kama za kutumiwa diplomasia ya kijasusi au kwa kutumia majasusi kamili pasi kuhusisha miundombinu ya kidiplomasia.
Kama ilivyoelezwa katika makala iliyopita, diplomasia ina nafasi muhimu katika uhusiano wa kimataifa. Mchango wa diplomasia katika kuleta amani ni mkubwa kama ulivyo katika kuepusha migogoro sambamba na kaika kuimarisha mahusiano baina ya nchi na nchi.
Sasa ukichanganya na ujasusi, diplomasia sio tu ina miundombinu mbalimbali ya kuwezesha ujasusi kufanyika kwa ufanisi bali pia ukweli kwamba diplomasia makini ni ile inayowezeshwa na taarifa za kiintelijensia ikiwa ni pamoja na ujasusi unaofanyika kupitia diplomasia.
Kwa mfano, kabla ya nchi kuafiki kusaini mkataba na nchi nyingine, ni muhimu kwa kila taifa kufahamu faida na hasara za mkataba huo. Lakini mara nyingi, faida zinazotajwa huwa tofauti na faida halisi. Na huwa kuna jitihada kubwa za kuficha hasara za mkataba husika.
Kwahiyo ni wajibu wa Idara ya Usalama wa Taifa ya nchi husika kujiridhisha kuwa mkataba huo utakuwa na faida halisi na endapo kuna hasara basi nazo zinafahamike, kisha kupimwa dhidi ya faida (cost-benefit analysis).
Sheria za kimataifa
Mkataba wa Vienna wa Mahusiano ya Kidiplomasia wa 1961, unatoa mwongozo wa kina kuhusu shughuli ya kidiplomasia, ambapo mwongozo huo unatanabaisha kuhusu, kwanza, usawa huru wa mataifa na, pili, wajibu wa kudumisha utaratibu wa kimataifa kwa kukuza mahusiano ya kirafiki kati ya mataifa.
Mkataba unafafanua kazi ya diplomasia, kinga na uwakilishi wa maslahi ya taifa na wajibu wa kudumisha amani kimataifa. Katika Mkataba hu, imeelezwa bayana kwamba njia ya kupata taarifa inaweza tu kwa njia halali.
Hata hivyo, Mkataba huo haubainishi kwa usahihi njia gani ni halali.
Lakini inafahamika kuwa matendo kama mwanadiplomasia kutoka nje kuwasiliana na watu ambao hawajaidhinishwa hutafsiriwa kama ishara za ujasusi.
Ukiukaji wa mara kwa mara wa njia halali (njia zinazoruhusiwa) katika kazi ya wanadiplomasia kutokea kuhusiana na ujasusi.
Kichekesho ni kwamba kwa sehemu kubwa, kinga kwa wanadiplomasia ni kama imewekwa kwa ajili ya kuwawezesha wanadiplomasia kujihusisha na ujasusi.
Ujasusi ni moja ya aina mbili kuu za makosa ya ukiukwaji wa kinga ya kidiplomasia. Aina nyingine ni ugaidi. Aina hizi mbili hufahamika kama ukiukwaji wa kisiasa, tofauti na ukiukwaji wa binafsi, kwa mfano mwanadiplomasia anapokiuka taratibu za usalama barabarani.
Hata hivyo, wanadiplomasia wengi huwa hawakiuki kinga hiyo ya kidiplomasia, na kwa wachache wanaokiuka, mara nyingi huwa ukiukwaji wa binafsi kuliko wa kisiasa.
Kuhusu sheria za kimataifa na ujasusi, kuna mitazamo miwili ya msingi. Mtazamo wa kwanza ni kwamba sheria za kimataifa hazizuwii bayana shughuli za kiintelijensia. Kwa maana nyingine ni kama sheria za kimataifa zinaruhusu ujasusi japo haijawekwa wazi.
Mtazamo wa pili ni ushirikiano baina ya mataifa katika masuala ya intelijensia. Kwa mfano, japo Marekani inafahamu kwamba Israeli inatumia wengi wa wanadiplomasia wake nchini humo, nchi hizo mbili zina ushirikiano wa kiintelijensia.
Sheria za kimataifa zinaruhusu nchi kujilinda. Lakini ili nchi kujilinda, inahitaji taarifa kuhusu nchi nyingine, ambazo hupatikana kwa njia ya ujasusi. Je haki ya kujilinda inatoa ruhusa kwa nchi kufanya ujasusi dhidi ya nchi nyingine?
Na kwa mujibu wa Sheria ya Kimataifa ya Migogoro inayohusisha Silaha (International Law of Armed Conflicts), ujasusi sio jambo linalozuiliwa. Hata hivyo, sheria za kimataifa hazimtambui jasusi aliyekamatwa kazini kama “mateka wa vita” (prisoner of war).
Katika stadi za sheria za kimataifa kuhusiana na ujasusi, kuna angalau mitazamo mitatu ya msingi. Mtazamo wa kwanza ni ujasusi kama suala ambalo “sio lisilo la kisheria” ( not illegal). Mtazamo wa pili ni ujasusi kama suala ambalo ni kosa la jinai (criminal offence). Mtazamo wa tatu ni ujasusi kama suala ambao sio lisilo halali wala sio halali (neither illegal nor legal).
Japo sio mwafaka unaokubalika kwa wote, ujasusi unaonekana kama shughuli ambayo haina mwafaka kimtazamo wa sheria za kimataifa.
Kufukuzwa kwa wanadiplomasia wa Urusi
Kama kuna mfano mzuri na wa hivi karibuni zaidi ni matukio ya kufukuzwa kwa wanadiplomasia wa Urusi katika nchi mbalimbali hususan za Magharibi. Kwa mujibu wa shirika la habari la Urusi TASS, hadi kufikia Januari mwaka huu zaidi ya wanadiplomasia 600 wa Urusi wametimuliwa na nchi za Magharibi.
Japo baadhi ya nchi zilizowatimua wanadiplomasia hao hazikuwatuhumu kuwa ni majasusi, lakini timua timua hiyo imeibua upya mjadala kuhusu mstari mwembamba kati ya diplomasia na ujasusi.
Kadhalika, nchi za Magharibi zimejikuta lawamani kwamba zimekuwa zikifumbia macho harakati za kijasusi za Urusi na badala yake zimetilia mkazo zaidi mapambano dhidi ya ugaidi, sambamba na kutegemea zaidi kunasa mawasiliano (intercepts).
Lakini pia kufahamika kwa idadi kubwa ya wanadiplomasia waliotimuliwa kumezua mjadala mwingine kuhusu kwanini nchi za Magharibi zinaruhusu Urusi kuwa na wanadiplomasia wengi kiasi hicho ilhali inafahamika bayana kuwa wengi wao kama si wote ni majasusi.
Kwa mfano Urusi ina wanadiplomasia 290 nchini Austria ilhali nchi hiyo ina wanadiplomasia 30 tu huko Urusi. Kumekuwa na maoni kwamba kuna haja ya uwepo wa uwiano kati ya idadi ya wanadiplomasia kati ya nchi husika.
Hitimisho
Makala hizi mbili zimetupia jicho uhusiano kati ya diplomasia na ujasusi, ambapo makala iliyopita ilijikita zaidi kuelezea kuhusu diplomasia na hii imejikita kueleza kuhusu jinsi ujasusi unavyotumia miundombinu ya diplomasia kutekeleza azma kusudiwa.
Makala ijayo itahusu tofauti kati ya ujasusi na uafisa usalama wa taifa