Dear Mama Samia, Kumezuka "Vijimaneno" Kuhusu Safari Zako "Mfululizo" Kwenda Zanzibar, Mwanza.

Kwanza kabla sijaingia kwenye mada husika, naomba nirudie tena msimamo wangu kuwa bado ninamuunga mkono Mama Samia Suluhu. Na japo silazimiki kusema kwanini namuunga mkono, haina ubaya kutanabaisha sababu kuu tatu za uamuzi wangu huo mgumu.

Yes, ni uamuzi mgumu kumuunga mkono japo mjumbe wa nyumba kumi wa CCM let alone Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho dhalimu, ambaye unfortunately ndio Rais wetu. Lakini wanasema “ukipenda boga, penda na ua lake.” Katika kumuunga mkono Mama Samia, inabidi kufumbia macho u-CCM wake, japo sio kazi rahisi.

Sababu ya kwanza ya kumuunga mkono Mama Samia ni ukweli kwamba ndani ya nafsi yangu naamini ni “mtu mwema.” Sasa, busara zinatuusia kwamba “never give up on a good person.” Si vema kumkatia tamaa mtu mwema. Nishaeleza mara kadhaa kwanini naamini kiongozi huyo ni “mtu mwema.”

Pili, namuunga mkono kwa sababu “she is all we have got.” Hatuna Rais mwingine. Sasa kwa vile kaingia madarakani “majuzi tu,” itakuwa mapema mno kukata tamaa ilhali amekuwa madarakani kwa takriban miezi 6 na ushee hivi. Ni kama kwenye mahusiano, kama wewe sio mchepukaji, basi inabidi ujibidiishe kumstahimilia mwenza wako kwa sababu ndo pekee uliyenae “angalau kwa wakati husika.”

Tatu, kufanikiwa kwa Mama Samia, au kufeli kwake, ni kwetu sote. Kwahiyo natamani sana kuona anafanikiwa kwa sababu akifanikiwa yeye tunakuwa tumefanikiwa sote. Na akifeli, tumefeli sote. Sote tumeshasafiri, iwe kwa ndege, treni, basi au bodaboda, na sidhani kama kuna msafiri mwenye akili timamu amewahi kutamani “dereva afeli” (mfano akosee kufunga breki kwenye makutano au aingie mtaroni). Kufanikiwa kwa dereva wa chombo cha usafiri tunachotumia ni kufanikiwa kwetu kama abiria.

Hata hivyo, kumuunga mkono Mama Samia sio kazi rahisi kwa sie tunaofahamika kwa kila jina baya - wahaini, makuwadi wa mabeberu, nk. Kuna lundo la watu ambao hawapo comfortable na huku kumuunga mkono kiongozi huyo. Ukipita huku na kule hutokosa kukutana na twiti za wahuni mbalimbali wanaodai “huyo jasusi uchwara anajipendekeza kwa vile anataka kurudi nyumbani.” Wengine wanatuhumu “anataka u-DC.”

Mie mtumishi/jasusi wako ni mmoja wa Watanzania wanaotukanwa mno mtandaoni. Na uamuzi wa kumuunga mkono Mama Samia umewaongezea sababu hao watukanaji. Ni kama nimewapa sababu ya ziada.

Lakini jingine ambalo linaleta ugumu katika kumsapoti Mama Samia ni ukweli kwamba chama chake CCM ni mzizi wa mtatizo yote yanayoikabili Tanzania yetu. Sasa sio kazir rahisi kumuunga mkono kiongozi nambari wani wa taasisi mbovu kama CCM. Lakini ndo hatuna jinsi. Ukipenda boga shurti upende na ua lake.

Nibingirike kwenye mada husika. Mie jasusi wako nasikia mengi. Yaliyopo hadharani na yaliyopo faraghani. Ya kusikilizwa kwa masikio ya kawaida, na ya kudakwa kwa “masikio ya kijasusi.” I hear a lot. Na alhamdulilah, kuna idadi si haba ya wazalendo wanaojibidiisha kunihabarisha kuhusu “hili au lile.” Ofkoz, miongoni mwa “wazalendo” hao kuna wazushi wanaojibidiisha kunilisha matango pori ili niishie kuwa kama Mlawa aka Kigogo kwa kulisha watu matango pori.

Kwahiyo katika “pitapita zangu” nimesikia “vijimaneno” kuhusu “safari mfululizo za Mama Samia huko Zanzibar na Mwanza.” Jana alikuwa Mwanza, na kutoka huko ameenda Zanzibar. Mie sijui amezuru Mwanza mara ngapi au ametembelea Zanzibar mara ngapi ila ninaweza kutamka bila shaka kuwa, ukiondoa Dar na Dodoma, maeneo hayo mawili - Zanzibar na Mwanza - yanaongoza kwa kutembelewa na Mama Samia.

Katika “vijimaneno” hivyo, wanasema “Mama yupo kiguu na njia kwenda Mwanza ili kuwapoza wakazi wa Kanda ya Ziwa walioondokewa na kipenzi chao John Magufuli.”

Kuhusu Zanzibar, “wasio na jema” hao wanadai “by the way, kila wikiendi Mama huenda Zanzibar, kwahiyo wala haina haja ya kutangaza kuwa amezuru Zanzibar.”

Sasa, wakati hakuna ubaya kwa Rais kutembelea sehemu kadhaa tu mfululizo, ni muhimu kuweka uwiano kwenye ziara za mkuu wa nchi ili kuepusha kujengeka hisia kuwa ni “Rais wa sehemu flani tu.”

Pamoja na mapungufu yake kadhaa, Jk hakuwa “kiguu na njia” kwenda Msoga ambako ni “hatua chache tu” kutoka Dar.

Tunajua kuwa Magufuli alikuwa “kiguu na njia” kwenda Chato, lakini miongoni mwa sababu muhimu ya safari hizo ilikuwa kuuguliwa na mama yake mzazi sambamba na matibabu yake binafsi.

Binafsi sina tatizo na hizo safari “mfululizo” japo natambua kuwa ni mzigo kwa walipakodi kwa sababu kila safari ya Rais hugharimu mamilioni.

Wasiwasi wangu ni wa kijasusi zaidi. Sidhani kama hao watu wa Idara ya Usalama wa Taifa wapo well-equipped katika kuhakikisha “pattern inayojengeka kuhusu ratiba za Rais” haitoi mwanya kwa wenye dhamira mbaya dhidi yake.

Pengine sintoeleweka vizuri kwenye angle hiyo ya kijasusi lakini nachoweza kutanabaisha ni hiki nilichotwiti Machi 20 mwaka huu, siku moja tu baada ya Mama Samia kuapishwa Urais.

Wenye kuelewa watakuwa wameelewa.

Nihitimishe kwa kurudia kuyumkinisha kuwa concern yangu pekee kuhusu safari hizo “za mfululizo” ni kwenye usalama wa Rais wetu, japo nitakuwa mnafiki kama sintoguswa na gharama zinazohusiana na safari hizo. However, kwa vile mie si mlipakodi Tanzania wala si mchumi, pengine nitakuwa si mtu sahihi kuongelea hilo la gharama za safari hizo.

Mwisho, wakaribishwa kujiunga na kijarida cha kila siku cha masuala la ujasusi duniani, kilichopo katika lugha ya Kiingereza.

Jumma Mubarak 🕌