Dear Mama Samia, Sikiliza Kilio Hiki Cha Wanao Wanaoteseka Huko JKT. Wanakulilia Na Kuomba Uwanusuru

Dear Mama Samia, nakusalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kazi iendelee. Baada ya salamu hizo, naomba niwasilishe ujumbe huu mrefu kidogo niliotumiwa na wanao wanaoitumikia nchi yetu huko JKT. Naomba niwasilishe ujumbe husika kama nilivyoupokea.

Brother habari yako, samahani Bro!! Mimi ni kijana wa JKT Op Mererani ambao nipo kwenye lile kundi la watu (service man) 2400 lililoahidiwa ajira na Rais Magufuli kwa matamshi mara nyingi tu pale Chamwino, na wenzetu sisi ndiyo wale idadi 854 waliofukuzwa kwa sababu za mgomo.

Kiukweli kabisa sisi tumefanya miradi mikubwa sana huku Dodoma. Safari yetu ya kwanza ilianza kwenye Ukuta wa kilometa 27 tuliouanza kuujenga rasmi kwa awamu ya pili mwaka 2019 (baada ya awamu ya kwanza kujengwa kwa 3KM na wenzetu walioondoka kwenda kuajiriwa intake ya 39) ya RTS Msata. Baada ya Ukuta wa Ikulu kukamilika tuligawanywa, wengine walibaki Ikulu kujenga uwanja wa parade huu ambao waliapishwa maafisa wapya siku kadhaa zilizopita na Mama Samia.

Na wakati huo huo kulikuwa na vimaradi vyengine vingi vinaendelea pale ikulu, ikiwamo nyumba za maafisa wa Tiss na mengine pamoja na hizo Block za Ofisi za Ikulu ambazo zimechukua muda mrefu..sambamba na hayo, wakati wengine wenzetu wamebakishwa ikulu, wengine tulipelekwa mradi wa Jengo la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) lenye floor 8 ambalo tukalijenga kwa usiku na mchana baada watu wa TBA kufukuzwa na Rais Magufuli.

Tulimaliza mradi huu ndani ya miezi ipatayo sita na hatimaye uchaguzi uliopita ukafanyika huku makao makuu yakiwa yameshasimikwa pale Njedengwa Dodoma tulipopajenga sisi. Tumefanya kazi nyingi sana za Ujenzi huku Dodoma lakini kuvhukuliwa kwenda kuajiriwa imekuwa vigumu sana na sisi hayuelewi shida ni nini. Kibaya ni kwamba watu wameumia, wengine wameumwa sana na wengine kutokuwa na stable conditions za miili yao.

Kibaya ni kwamba sisi Op Mererani wametuongeza tena mkataba utakaoanza tarehe 01 Julai mpaka December ambapo kimahesabu tutakuwa tumetimiza miaka Minne kamili JKT. Kibaya zaidi ni kwamba kama unavyojua mambo ya kijeshi hayasemwi popote, shida zetu tunakufa nazo moyoni tu! Tukienda Msata kwa mfano kwenye Recruit course kama unavyojua kuna vipimo vingi sana...kwa hali tuliyokuwa nayo sasa wengi wetu tutasomwa kama 'Unfit to progress'

Halafu hatimaye tutarudishwa nyumbani. Ombi langu naomba ulisemee hili. Nafahamu mama ni mtu wa mitandao sana, na anawasikiliza watu makini kama wewe whether kwa kujua au kutokujua lakini nina imani hiyo!!

Naomba utusaidie kumwambia mama kuhusu hili, tunaumia sana na kazi hizi ngumu za Ujenzi, tunafikiri labda kifo cha rais aliyepita kimechangia, lakini tuna imani sana na mama. Tunaomba utuombee atuajiri au kama serikali imeshindwa basi iturudishe tu nyumbani, maana tuliahidiwa ajira na rais aliyepita na mara zote tuliitwa mashujaa..

Hata wenzetu waliofukuzwa ni kwa sababu ya kuongezewa majukumu na wakuu wetu wakati wanafahamu fika hali zetu za kimwili na kiakili, tumekufa kisaikolojia na ni kama tumekuwa wafu tuliokata tamaa huku miili yetu ikiwa hoi.

Nakuomba utusaidie kwa hilo, japo unilinde usinitaje brother kwa sababu najua wewe unafahamu haya mambo ya kijeshi, kwa sababu pia huwa nakufwatilia sana na in other way you are my Mentor. Naomba utusemee brother.

Nimeandika nikiwa natokwa na machozi mengi. Tumevumilia vingi lakini walau tulitaraji ujira wetu. Familia zetu zimetusubiri sana zikitegemea tunapata chochote kitu lakini sasa zimekufa moyo baada ya miaka kupita. Sasa hivi wametushushia Ration scale ya kula kwa Vijana wa JKT na kuna mradi unaitwa Shule ya mfano upo Iyumbu ambao wengi wetu tulioanzisha miradi huku Dodoma ndiyo tupo. Ni mradi mkubwa ambao hautoisha leo.

Sasa watatuweka hivi mpaka lini? Ukinisaidia kwa hilo brother utakuwa umewasaidia vijana siyo chini ya 1400 ambao hali zao zimedhoofika na wamechoka kiakili kwa kiwango kikubwa.

Mimi binafsi nina shahada tena ya sayansi lakini kwa sasa hivi hali yangu ni kama sijawahi kusoma Chuo kikuu chochote duniani,hata kama nitaitwa kwenye Interview leo, sipo competent kabisa kushindana na mtu aliyetokea uraiani. Naomba unisaidie kwa hilo brother Chahali. Thanks!.

NB: Mungu akubariki brother,hivi navyokuandikia hivi, Order imetoa makao makuu ya JKT kwamba tumeongezewa tena miezi sita..machozi yamenitoka, ndiyo maana ikabidi nikutafute..samahani kwa usumbufu brother.

Halafu kwa clarification tu brother ni kwamba kwenye hizo idadi nilizokutajia hakuna Service girl hata mmoja wote ni wanaume (service man) maana walikataa kuwaleta wasichana kwenye kazi ngumu za miradi. Kwahiyo automatically Service girl wa OP yetu wote walirudi nyumbani baada ya mkataba kuisha, waliobaki ni service girl wasiozidi 100 ambao wapo Kikombo (Makao makuu ya muda ya JWTZ) huku Dodoma. Nao walirudishwa kwa kigezo maalumu cha kuwa wanamichezo.

Kwahiyo kwa sasa navoongea, hakuna Service girl popote, iwe kwenye miradi au vikosi vya JKT ambae ni OP Mererani, isipokuwa hao ambao wapo Kikombo tu wasiozidi 100. Na al kadhalika hakuna Service man wa OP Mererani vikosini isipokuwa sisi tu ambao tupo kwenye miradi Dodoma na Rufiji.

Wenzetu wa OP yetu wote walisharudi nyumbani, sisi tuliongezewa mkataba mara tatu (6 month each) kwa kigezo cha kwamba yuna maelekezo maalumu ya Rais Magufuli, kwahiyo tusiguswe, lakini mambo yalipofikia hapa hatuelewi hata hatma yetu ki ukweli.

Ni matumaini yangu makubwa kwako Mama kuwa utasikia kilo cha wanao hawa.

Asante kwa niaba yao!