Dear Mama Samia, Kesi Ya Mbowe ni ya Kisiasa Na Inatia Doa Utawala Wako, Ushauri wa TISS Kuwa "Mbowe Afungwe Kisha Umsamehe ili Upate Political Capital" ni Fyongo. Hujachelewa, Chukua Hatua Stahili.

Nitanabaishe mapema kuwa bado ninamuunga mkono Mama Samia Suluhu, sio kwa sababu za “kusubiri uteuzi” au “kujikomba,” bali kwa sababu mbili kuu. Ya kwanza na ya msingi kabisa ni ukweli kwamba kufanikiwa kwake ni kufanikiwa kwetu sote.

Sawa, ni Rais anayetokana na CCM, ambayo naichukia with passion, lakini ni Rais wa Watanzania wote, at least theoretically. Akifeli yeye, tumefeli sote. Jumba bovu likimuangukia yeye, limetuangukia sote.

Sababu ya pili unatokana na kile Waingereza wanausia, “don’t give up on a good person,” yaani “usimkatie tamaa mtu mwema.” Mama Samia is a good person, lakini kama ilivyo kwa kundi dogo la watu wema ndani ya CCM, inawawia vigumu kuonyesha wema wao kutokana na falsafa nzima ya uongozi wa chama hicho tawala.

CCM haijawahi kuupenda upinzani. Sio tu upinzani ulioruhusiwa mwaka 1992 bali hata upinzani ndani ya chama hicho. Kwa bahati mbaya - au pengine makusudi - historia pekee inayofahamika kuhusu chama hicho ni ile tu ambayo chama hicho inataka ifahamike.

Huwezi kukutana na maelezo yoyote kuhusu jinsi Idara ya Usalama wa Taifa ilivyoshiriki kikamilifu katika kutengeneza muungano wa TANU na ASP na kuzalisha CCM. Huwezi kufahamu kuhusu mazingira yaliyopelekea Mwalimu Nyerere kuachia ngazi mwaka 1985. Huwezi kufahamu yaliyowakumba “wakorofi ndani ya CCM” kama Marehemu Horace Kolimba, Marehemu Aboud Jumbe Mwinyi, Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad (alipokuwa Waziri Kiongozi Zanzibar), Marehemu Dokta Omari Ali Juma, nk.

Lakini hata “matukio yasiyohusiana na watu kupoteza uhai,” huwezi kupata taarifa sahihi kuhusu tukio muhimu kabisa kwa siasa za Tanzania, linalofahamika kama Azimio la Zanzibar, ambalo kimsingi ndio lililochinjilia mbali siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, na kuhalalisha ufisadi katika jina la “uchumi wa soko huria.”

CCM ni chama cha kiharamia. Wana-CCM wenyewe wanajua hilo vyema. Kwa bahati mbaya haya ndiyo mazingira ambayo Mama Samia anafanyia kazi. Simtetei, lakini natanabaisha mazingira yasiyo rafiki kwa mtu mwema.

Lakini changamoto nyingine kwa Mama Samia ni uwepo wa makundi mbalimbali ndani ya chama hicho, kila moja likiwa na maslahi binafsi. Kundi hatari zaidi kwa sasa lipo huko Idara ya Usalama wa Taifa ambako wahafidhina wanahangaika na kulinda maslahi yao kwa kisingizio cha “kudumisha legacy ya Mwendazake (Magufuli)” japo kwa hakika wanaficha madhambi yao tu.

Kuna kundi kubwa la watu walioshiriki kwenye kampeni endelevu za kuteka, kutesa, kubaka na hata kuua watu wasio na hatia (rest in peace Injinia Lwajabe, Ben Saanane, Azory Gwanda, na wengineo). Wapo walioshiriki kufanya uharamia mkubwa kabisa wa kutumia ulawiti kama silaha ya kisiasa. Wapo waliopora mali za watu na hata wake za watu. Mliyosikia kwa Sabaya na “trela” tu ya kilichojiri kati ya Novemba 5, 2015 hadi Machi 12 mwaka huu aka zama za Mwendazake.

Ni mazingira haya yaliyozua kesi dhidi ya Mheshimiwa Freeman Mbowe. Na kinachomponza Mheshimiwa Mbowe na Chadema kwa ujumla ni kile kinachohofiwa na CCM kuwa ni “nguvu ya watu wa Kaskazini” hususan Wachagga. Lakini pia Chadema ndio chama pekee kinachoweza kutishia ulaji wa CCM kwa wakati huu. Na hakikufika hapo kilipo kirahisi. Wakati wa utawala wa JK, wana-Chadema kadhaa waliuawa kwenye matukio mbalimbali halali ya chama hicho. Na kipindi cha Mwendazake, kuwa mwana-Chadema ilikuwa kitu hatari kuliku kuwa muuza unga.

Lakini jitihada zinazofanyika ili Mama Samia aendeleze chuki za kisiasa za zama za Mwendazake zina sura pana zaidi. Ikumbuke kuwa Mama Samia alipoingia madarakani, alionyesha dalili za wazi za kutaka siasa za maridhiano. Akaenda mbali na kutanabaisha kuwa sio tu angekutana na viongozi wa upinzani kujadili masuala muhimu kuhusu ustawi wa taifa letu bali pia alitanabaisha kuwa katika uongozi wake angetilia mkazo uwezo wa mtu katika kazi na sio itikadi yake ya kisiasa, akimaanisha kuwa hata wanasiasa wa upinzani wangeteuliwa kwenye serikali yake.

Sasa kwa wanufaika wa siasa za chuki, ikiwa ni pamoja na maovu yao kufichwa katika mfumo wa kulindana ulioshamiri ndani ya CCM, walitambua kuwa maslahi yao yapo hatarini. Kwa bahati mbaya pia, baadhi ya kauli za viongozi wa Chadema waliokuwa wakijazwa upepo na “wanaharakati wa mtandaoni” ziliwasaidia maharamia huko CCM na serikalini wanaotaka siasa za chuki/mfarakano.

Baadhi yetu tulitahadharisha kuhusu lugha zinazotumika kumtaka Mama Samia afanyie kazi kadhia mbalimbali, kwamba yaweza kumfikisha mahala akaamua “nitawaonyesha Rais ni nani.”

Hiyo ni rough background ya “tumefikaje hapa.” Hata hivyo bado kuna nafasi kwa Mama Samia kurekebisha mambo. Kwa sababu nyingi tu, lakini kubwa zaidi ni kwamba kinyume na ushauri wa hao wahafidhina wa Idara ya Usalama wa Taifa wanaomhadaa kuwa “akimfunga Mbowe kisha akamsamehe atajenga mtaji wake wa kisiasa (political capital)”, kesi hiyo inachafua taswira nzuri yake Mama Samia binafsi na kwa Tanzania kwa ujumla.

Yeye anafahamu fika jinsi nchi yetu ilivyotengwa kimataifa, na ndio maana majuzi serikali yake imemkodi Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair kusaidia kukarabati taswira ya Tanzania kimataifa.

Kwa bahati mbaya, hata baadhi viongozi wachache wa CCM ambao hawapendi kuona Tanzania ikirudi kwenye zama za siasa za chuki, ikiwa ni pamoja na wale waliowahi “kufanyiziwa na Mwendazake,” hakuna mwenye ujasiri wa kumshauri vema Mama Samia katika suala hili, kisa ni kilekile kinachotuangusha sana; kuweka mbele maslahi binafsi. Watu wanaogopa kutoa ushauri kwa kuchelea kumwaga ulaji wao.

Nihitimishe kwa kutoa wito kwa Mama Samia, hata kama hautomfikia. Japo hajatulazimisha kumuunga mkono, katika hili la kesi ya Mheshimiwa Mbowe anatuangusha kwa namna mbili. Kwa kwenda kinyume na matarajio yetu makubwa kuwa atakuwa “malkia wa upatanishi,” na kutuangusha kwa maana ya taswira yetu kimataifa ambayo tangu aingie madarakani ilianza kusafishika japo kiduchu.

Kesi ya Mheshimiwa Mbowe haina tija yoyote kwa Mama Samia, CCM na hata hao wahafidhina wa Idara ya Usalama wa Taifa. Nothing good will ever come out of this case.

Good day!