Dear Magufuli, Iweje Athari Kwa Nchi 8 Ziwe Muhimu Kuliko Uhai Wa Watanzania?

Kwa mara nyingine tena, Rais Magufuli amewathibitishia Watanzania kuwa sio tu hahangaishwi na janga la korona bali pia hathamini uhai wao. Kama mzaha vile, baada ya kupotea tangu Machi 28 mwaka huu,

jana aliibuka na kueleza kuwa serikali yake haitofunga mipaka na hakutokuwa na lockdown.

Lakini cha kukera mno kwenye tamko lake hilo ni madai kwamba kufunga mipaka kutaathiri nchi 8 zinazotegemea huduma na bidhaa kupitia Tanzania. Haya ni matusi kwa Watanzania. Iweje athari kwa nchi hizo 8 ziwe na umuhimu kuliko uhai wa Watanzania?

Kadhalika, kwa kuonyesha kuwa Tanzania ina Rais asiyethamini uhai wa wananchi wake, katika hotuba yake ambayo hata hivyo hakuna video kuthibitisha kweli alikuwa kanisani jana, hakuona umuhimu kutoa pole kwa familia za Watanzania watatu waliofariki kwa korona.

Vilevile kauli ya Rais Magufuli kwamba “msalaba unaokoa…na kwa kupitia msalaba, Mungu ataiokoa dunia dhidi ya majanga mbalimbali ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa korona” inapuuzia ukweli kwamba si kila Mtanzania ni Mkristo anayeamini katika msalaba.

Kadhalika, kwa kutumia kanisa kwa mara ya pili kutoa ujumbe wa kidini kuhusu korona, Rais Magufuli anawabagua wasio Wakristo kwa sababu la muhimu sio ujumbe tu bali pia ujumbe huo unawasilishwa sehemu gani.

Wakati Rais Magufuli akiendeleza mzaha kuhusu janga hilo la korona, taarifa zilizopatikana jana jioni zinaeleza kuwa watangazaji wawili wa TBC wamefariki dunia kutokana na korona, huku mtangazaji mwingine akiwa mahututi. Inaelezwa kuwa watangazaji hao waliambukizwa na mwenzao mmoja aliyefariki majuzi japo “kifo hicho hakikuelezwa kuwa kilitokana na korona.” Endapo taarifa hizi ni za kweli, kuna uwezekano kwa maambukizi ya ugonjwa huo kusambaa sio tu miongoni mwa watumishi wa taasisi hiyo bali pia watu mbalimbali waliokutana nao.

Hatuwezi kuongelea kuhusu kuongezeka kwa maambukizi ya korona, na vifo vinavyotokana na maambukizi hayo, bila kuhusisha Rais Magufuli ambaye tangu mwanzo wa janga hili ameonyesha waziwazi kuwa halimsumbi wala hajali nini kitawasibu Watanzania anaowaongoza.

Makala hii inaonyesha uthibitisho wa jinsi kauli za Rais Magufuli zinavyochangia kuwafanya Watanzania wengi wapuuzie tahadhari kuhusu janga hilo la korona.

Wakati hayo yakitokea, kuna mkanganyiko unaotokana na kauli zenye kukinzana kati ya Waziri Ummy na RC Bashite

Nimalizie kwa kuwasihi Watanzania wenzangu kuwa mmemlea Rais Magufuli kwa muda mrefu sasa na msipochukua hatua za makusudi, mtajilaumu huko mbeleni.

Jingine la muhimu ni kwamba kesho ni Pasaka. Wito wangu kwa Wakristo wenzangu ni kwamba kama unajali afya yako, fanya ibada ya Pasaka nyumbani.

Jikinge dhidi ya korona, na wakinge na wenzio pia.

Ndimi mtumishi wako,

Evarist Chahali