Dear Fatma Karume, pole kwa kutukanwa na baadhi ya wana-Chadema. Hata hivyo, wewe na Maria "mmewalea" sana hawa watukanaji mtandaoni
Nianze kwa kutoa pole kwa matusi ambayo mwanaharakati Fatma Karume amekuwa ukivurumishiwa na baadhi ya wana Chadema ambao hawakupendezwa na uamuzi wake wa kwenda kutoa maoni kwenye Kikosi Kazi cha Rais kuhusu masuala ya siasa.
Hata hivyo, huenda wahuni hao wasingeweza kuwa na jeuri ya kumtukana mwanasheria huyo laiti yeye na mwenzie Maria wangechukizwa na tabia ya matusi ya baadhi ya wafuasi wa Chadema ambao pia walikuwa ni mashabiki wakubwa wa akinadada hao.
Pengine Fatma amesahau, lakini huko nyuma wakati mie nina mawasiliano nae (yalivunjika baada ya yeye kunisemea ovyo), niliwahi kumtumia DM kuhusu matusi ya Kigogo dhidi ya Mama Samia lakini sikupata jibu. In fact wakati Kigogo anamkebehi na kumtusi Mama Samia mfululizo, sio tu hakuwahi kumshauri aache kumkosea heshima Rais bali pia alimmwagia sifa kama twiti hii inavyoonyesha

Lakini si matusi ya Kigogo kwa Mama Samia tu ambayo both Fatma na Maria hayakuwasumbua, mvua ya matusi na udhalilishaji tuliofanyiwa na mtu huyo haikuwasumbua pia na waliendelea kuwa maswahiba.
Nilitatizwa sana na hali hiyo kwa sababu naamini kuwa laiti wangemshauri mpenda matusi huyo kwamba aache matusi na awasilishe ujumbe wake kwa lugha ya kistaarabu basi huenda asingeendelea kutukana.
Kilichonisikitisha zaidi ni ukweli kwamba both Fatma na Maria walikuwa wahanga wa matusi ya Musiba, yule mpambe wa Mwendazake ambaye kila kukicha alizusha hili kama sio lile. Kwa maana hiyo, katika mazingira ya kawaida ungetarajia akinadada hao wachukizwe na mtu yeyote aliyefanya mambo kama ya Musiba. Lakini kwa sababu wanazozijua wao, walikaa kimya.
Yayumkinika kutanabaisha bila shaka kuwa umaarufu na kukubalika kwa Kigogo kulichangiwa kwa kiasi fulani na ukweli kwamba alikuwa akikubalika kwa akinadada hawa wawili wanaoheshimiwa na Watanzania wengi.
Akinadada hao wanafahamu vema kuwa Musiba alianza kutuandama watu wachache tu kabla hajaota mapembe na kusambaza hujuma zake hadi kwa baadhi ya wana-CCM. Funzo hapo ni hili: MCHAWI AKIMALIZA KUROGA MTAA MZIMA HUHAMIA KWENYE FAMILIA YAKE.
Kwa maana hiyo kama ambavyo ilikuwa suala la muda tu kabla Musiba hajaanza kuwavaa wana-CCM wenzie, kwa Kigogo nae ilikuwa suala la muda tu kabla hawaanza kuwavaa watu waliokuwa wanamsapoti ikiwa ni pamoja na Fatma na Maria.
Na ndivyo ilivyokuwa. Mara baada ya Kigogo kutibuana na Chadema na kujipeleka CCM, amekuwa mkosoaji mkubwa dhidi ya both Maria na Fatma. Watu walewale waliomuenzi, wamegeuka wahanga wake.
Kwahiyo ungetegemea kuwa development ya Musiba from kutushambulia sie “watu hatari” hadi kuwavamia akina Kinana, na hiyo ya Kigogo from kumtukana Mama Samia na sie wengine hadi sasa kuwageukia akina Maria na Fatma ingekuwa funzo kwa akinadada hao dhidi ya viumbe wote wanaofanya unyanyasaji mtandaoni kwa njia ya matusi. Lakini kwa vile matusi hayo yalitulenga wengine, akinadada hao waliendelea kuwa comfortable.
Katika moja ya twiti zake, Fatma anasema

Yuzuu @Yuzuumwakisunga
@fatma_karume Auntie mbona Leo uko very furiously 😂😂✌️🤔Lakini anakwepa kuongelea UNAFIKI WA WANAHARAKATI ambao sio tu wanakalia kimya ukiukwaji wa haki za watu mbalimbali wanaotukanwa mtandaoni kwa vile tu hawaafikiani na hoja za watu flani bali pia wana uswahiba na watukanaji hao.
Majuzi tumeshuhudia Mheshimiwa Freeman Mbowe akiwatolea uvivu viongozi wenzie na wanachama wengine wa Chadema na kuwaeleza bayana kuwa matusi hayakubaliki, sambamba na kukemea lugha isiyo ya kistaarabu dhidi ya viongozi wa vyama vingine. Japo hakuvitaja vyama hivyo, ninaamini alikuwa akiongelea ukosefu wa nidhamu miongoni mwa wana-Chadema wengi dhidi ya Mama Samia na Mheshimiwa Zitto Kabwe, kiongozi mkuu wa ACT-Wazalendo.
Both Fatma na Maria wanafahamu kuwa jambo pekee linalohitajika kwa maovu kushamiri ni kwa watu wazuri kama wao kukaa kimya. Ndio maana naamini kwa dhati kabisa kuwa laiti wanaharakati hawa wangekuwa mstari wa mbele kukemea matusi kama tunavyofanya wengine, basi huenda tabia hiyo isiyopendeza ingepungua sana.
Kama sauti muhimu kwenye ajenda ya katiba mpya, ungetegemea wanaharakati hao wawakumbushe wafuasi wao wanaoendekeza matusi kwamba “matusi yananajisi mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya”. Ni hivi, kama hawa wanaopigania katiba mpya ni madikteta ambao usipoafiki hoja zao wanakutukana, je wakiingia madatrakani si watanyonga kila mtu?
Nimalizie kwa kutumaini kuwa labda experience hii isiyopendeza ya matusi dhidi ya Fatma itamsaidia sio tu kutambua tena kuwa “MCHAWI AKIMALIZA KUROGA MTAA MZIMA HUVAMIA KWENYE FAMILIA YAKE” yaani hao wapenda matusi wakishamaliza kumtukana Mama Samia na akina sie watawageukia haohao akina Fatma na Maria (na mfano hai ni Kigogo wa leo vs Kigogo yule aliyekuwa swahiba wa both Maria na Fatma) bali pia itampa jasiri wa kuwakumbusha “fans wake” pindi wanapoanza kutumia matusi kama nyenzo ya kuzuwia maoni wasiyotaka kuyasikia.
Watanzania tuna kasumba ya kuvumilia maovu. Hakuna anayekumbuka wala kujali yaliyojiri zama za ufisadi katika wamu ya Jk kama hakuna anayesumbuliwa na yaliyojiri zama za udikteta wa Mwendazake. Ni kama hakuna baya lililojiri huko nyuma.
Na ni katika namna hiyohiyo, ni watu wachache tu wanaotatizwa na tabia inayozidi kushamiri ya matusi mtandaoni. Kwa watu wengi tu, tatizo hilo haliwahusu kwa sababu wao sio wahanga. Lakini wanachosahau kuwa kushamiri kwa matusi mtandaoni kunamfanya kila mtumiaji wa mtandao kuwa mhanga mtarajiwa.
Mwisho, ni matumaini yangu kuwa Fatma ataichukulia makala hii kwa mtazamo chanya na ikiwezekana kufanyia kazi ushauri uliomo.
TANZANIA BILA MATUSI INAWEZEKANA.
Jumma Mubarak!