Dear Chadema, Mapungufu Yenu Ambayo Mkiambiwa Mnakuwa Wakali, Yanawarahisishia CCM Kuwanyanyasa

Natambua fika kuwa viongozi na wananchama wa Chadema watapokea makala hii kwa ukali kama sio matusi. Kimsingi, linapokuja la kuchukia ukweli, hakuna tofauti kati ya wafuasi wa Chadema na wale wa CCM. Ukitaka kuwa adui yao, waambie ukweli. Lakini ukweli unabaki ukweli hata ukipokelewa kwa matusi.

Bila haja ya kurudi nyuma sana, tutupie jicho matukio ya hivi karibuni. Baada ya viongozi na wana-Chadema kadhaa kukamatwa Mwanza waliopanga kufanya kongamano la Katiba, zilisikika kelele nyingi ikiwa ni pamoja na tishio la maandamano lakini ukweli ni kwamba kilichowatoa rumande waliokamatwa sio shinikizo la Chadema bali huruma ya polisi. Kwa lugha nyingine, haki za Chadema - kama hizo wanazopigania kwenye Katiba mpya - zipo mikononi mwa polisi.

Unaweza kusema “ndio maana tunapigania katiba mpya.” Hold on. Katiba sio kuhusu haki tu bali pia wajibu. Sasa wajibu kwa mtu anayeonewa ni nini kama sio kuchukua hatua stahili? Ukiangalia jinsi Chadema walivyoshughulikia tukio hilo la kukamatwa viongozi wa kongamano hilo (la kwanza) haina tofauti na wanavyoshughulikia suala la akina Halima Mdee. Ni mwendo wa kulalamika tu, lakini hakuna hatua ya maana wanayochukua.

I know waliwatimua akina Mdee, lakini mpaka leo bado wapo bungeni na Chadema hawajaenda mahakamani kudai haki yao. Ukiwauliza, wanatukana.

Mapungufu mengine kadhaa ni katika suala la Mbowe. Hivi nini hasa kilimsukuma Mbowe kwenda Mwanza na kushinikiza kufanya kongamano huku akijua bayana kuwa ataishia kukamatwa kama walivyokamatwa viongozi na wanachama walioandaa kongamano la awali?

Kuna wanaoweza kusema kuwa huo ni ujasiri. Hapana. Kujiingiza matatizoni bila faida sio ujasiri. Ni ukosefu wa busara. Ndio maana polisi wamepata kisingizio kudai kuwa “Mbowe alijua atakamatwa ndio maana akakimbilia Mwanza kudai anataka kufanya kongamano la katiba ili akikamatwa asingizie kongamano hilo.” Polisi ni wazushi lakini unaweza kujiuliza, kwanini Mbowe aling’ang’ania kufanya kongamano hilo akijua bayana kuwa atakamatwa?

Lakini kuna mapungufu kwa upande wa chama kwa ujumla. Ni dhahiri kwamba hakukuwa na Plan B, kwamba endapo safari hii polisi watazuwia au kuwakamata viongozi wetu, tutafanya hiki.

Awali Lissu alitoa wito kwa wakazi wa Mwanza kuandamana. Wakampuuza. Sijui alishasahau kuwa Novemba 2 mwaka jana, si wanachama tu bali hata viongozi wenzie walipuuza wito wa kujitokeza kwenye maandamano ya amani kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2020.

Na baada ya Mbowe kukamatwa, zimepita siku 6 kabla hajafikishwa mahakamani, na hakukuwa na hatua yoyote ya maana kumpigania zaidi ya kutengeneza hastag kudai Mbowe sio gaidi na nyingine zikisema Mama Samia ni dikteta. Je hashtag hizo zimesaidia nini?

Tatizo jingine ni ombwe lililoanza kujitokeza kitambo lakini sasa limeshamiri ambapo “wanaharakati wa mtandaoni” ni kama wamepora uongozi wa chama hicho na kuonekana wakitoa muongozo kuhusu nini kifanyike kuhusiana na suala la Mbowe na madai yao ya katiba mpya. Huhitaji kuwa na uelewa mkubwa kwamba maslahi ya wanaharakati hao ni yao binafsi, na Chadema inawapatia tu jukwaa la kufanya harakati zao.

Lakini huwezi kuwalaumu kwani hii si mara ya kwanza kwa “Chadema kushindwa kujiongoza.” Mwaka 2015, ikiwa katika nafasi bora kuliko zote kuing’oa CCM madarakani, ikaamua kumsimamisha kada mzoefu wa CCM, Edward Lowassa kuwa mgombea wake katika nafasi ya urais. Kitendo tu cha Chadema kumpokea Lowassa kilipelekea watu wengi kuachana na chama hicho kilichopata umahiri mkubwa kwa kusimamia ajenda ya vita dhidi ya ufisadi.

Kwa vile Chadema ndio walioshikilia bango kuhusu “ufisadi wa Lowassa” tangu Februari 2006 hadi walipompokea Julai 2015 - miaka 9 hiyo - walilazimika kulamba matapishi yao na kuzunguka nchi nzima kumsafisha Lowassa katika kampeni za uchaguzi mkuu wa 2015 ambapo walitumia muda mwingi kudai “kama CCM wana ushahidi kuwa Lowassa ni fisadi basi wamfungulie mashtaka.” Hapo walijitoa ufahamu kuwa waliomtuhumu Lowassa kuwa ni fisadi ni wao Chadema na sio CCM.

Athari za ujio wa Lowassa huko Chadema ni kubwa kuliko faida. Moja ya athari hizo ni kuwarahisishia Idara ya Usalama wa Taifa kupandikiza watu wao ndani ya chama hicho kwa kisingizio cha “wafuasi wa Lowassa walioamua kumfuata Chadema.” Na mapandikizi hayo - ambayo baadhi yetu tunayafahamu - yanaendelea kukitafuna chama hicho kimyakimya.

Mwezi uliopita, Chadema walifanya utoto kwa shinikizo la wanaharakati, wakaungana nao kushawishi Watanzania “wasimpigie kura Diamond Platnumz.” Kichekesho ni kwamba chama hicho kinachotarajiwa kuwa makini wala hakijihangaisha kujua kuwa ushindi wa category aliyokuwa anawania Diamond haukuwa ukihusisha kura za kila mtu bali kundi la watu 500 hivi waliounda BET Award Voting Academy.

Baada ya kubaini kuwa hata wakihamasisha kutompigia kura Diamond itakuwa kazi bure, wakaungana na wanaharakati kufanya petition kutana BET wamuondoe msanii huyo kwenye kuwania tuzo hizo. Bahati nzuri BET wakapuuza ujinga huo.

Sababu ya wao kuungana na wanaharakati dhidi ya Diamond ni kwamba “msanii huyo alishiriki kumnadi Magufuli, na kwamba hakukemea maovu ya utawala uliopita.” Sawa, ni kweli Diamond alimpigia kampeni Magufuli, na ni kweli hakukemea maovu. Lakini kila mwenye akili timamu anafahamu kuwa msanii huyo hakuwa na choice ya kukataa kumpigia kampeni dikteta huyo. Na kubwa zaidi, alilipwa mamilioni kwa kazi hiyo. Kwa kijana aliyetoka kwenye umasikini mkubwa hadi kufikia hatua ya juu kabisa kiusanii sio Tanzania pekee bali barani Afrika kwa ujumla, angekuwa mjinga wa hali ya juu kuhatarisha kila alichonacho kwa vile tu haafikiani na mtawala aliyepo madarakani. Kila Mtanzania anafahamu kuwa hakuna mti aliyekuwa na jeuri ya kukataa matakwa ya Magufuli.

Lakini hata kama Diamond angekuwa na nafasi ya kukataa, kirefu cha CHADEMA ni Chama cha DEMOKRASIA na Maendeleo. Sasa, demokrasia ni pamoja na kutofautiana kimtazamo bila kugombana. Kwanini basi demokrasia iwekwe kando kwenye uamuzi wa Diamond kumuunga mkono Magufuli, jambo ambalo sio kosa kikatiba?

Bottom line is ombwe la uongozi ndilo lililowezesha wanaharakati kushawishi chama hicho kiunge mkono hoja hiyo fyongo.

Ni fyongo kwa sababu msanii huyo ana followers milioni 12.4 huko Instagram pekee. Hao ni zaidi ya idadi ya wana-Chadema wote. Kwahiyo akihamasisha wafuasi wake dhidi ya chama hicho, hakiwezi kufua dafu.

Lakini pia kampeni hiyo iliwakwaza vijana wengi tu wanaomuona msanii huyo kama “role model” wao kwenye suala zima la kujituma kimaisha. Wanamuona kama ushuhuda kwamba kuzaliwa Tandale hakumzuwii mtu anayejituma kuja kuwa tajiri na maarufu.

Tukiweka kando hilo, kulikuwa na mapungufu katika mkakati wa kudai Katiba mpya. Naam, katiba mpya ni muhimu lakini kosa kubwa la Chadema katika suala hilo ni ndoa yao ya mkeka na wanaharakati wa mtandaoni, baadhi yao wakiwa wale wanaofahamika kwa kuwatukana viongozi hadharani. Ofkoz, Chadema haipaswi kupangiwa mtu wa kushirikiana nae au kutoshirikiana nae lakini kujiweka karibu na watu wanaofahamika kwa kuwatukana viongozi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mama Samia, sio uamuzi wa busara.

Lakini Chadema hawakufanya hivyo kwa bahati mbaya. Uhusiano huo ni kama ule wa CCM na Idara ya Usalama wa Taifa. Kibaiolojia unaitwa symbiotic. Kubaki madarakani kwa CCM kunategemea sapoti ya Idara ya Usalama wa Taifa. Lakini kuhifadhiwa kwa madudu ya Idara hiyo kunategemea uwepo wa CCM madarakani.

Kwa Chadema, ombwe la uongozi linakifanya chama hicho kiamini kuwa ili ujumbe wake uwafikie watu wengi ni lazima kijiweke karibu na wanaharakati hao, ambao nao wanatumia vema ukaribu huo kusambaza kampeni zao mbalimbali.

Naweza kuendelea kuandika zaidi na zaidi lakini niishie hapa kwa kutoa wito kwa vijana “wafia chama” kutokubali kuona chama hicho kinaporwa na watu ambao hawajakitolea jasho wala kukivujia damu. Hizo kiki za mtandaoni sio muhimu kama kukubalika kwa chama mtaani.

Na japo huu si wakati mwafaka kuhoji uwepo wa Mbowe madarakani kwa miaka 17, pengine kuna haja ya fikra mpya zinazoweza kuleta mabadiliko ya mwelekezo na fikra, na pengine kufanikiwa kukiingiza Ikulu, kama si mwaka 2015 basi 2030. Kwa mazingira yaliyopo sasa, Chadema itabaki kuwa chama cha kianaharakati tu lakini kisicho na uwezo wa kuing’oa CCM.

Thanks!