Dear CHADEMA, Katika Hili la Namba ya Simu ya Mheshimiwa Mbowe Kuwekwa Hadharani na Mlawa, na Nyie Kulikalia Kimya, Mnamuangisha Mwenyekiti Wenu.

Jana, Didier Abdallah Mlawa aka Kigogo aliweka hadharani namba ya simu ya Mheshimiwa Freeman Mbowe huko kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.

Sasa, kisheria, ni kosa la jinai kuweka taarifa za binafsi za mtu hadharani bila idhini yake.

Lakini kwa Twitter, moja ya makosa yanayoweza yanayochukuliwa kwa uzito mkubwa kiasi cha kuweza kuepelekea akaunti ya mtu ifungwe ni kuweka hadharani taarifa binafsi za mtu bila idhini yake. Na moja ya taarifa hizo ambazo hutumiwa sana na wanyanyasaji wa mtandaoni ni namba za simu.

Kuna kitu kwenye udukuzi kinafahamika kama DOXING. Kinakaribiana na alichofanya Mlawa jana.

Hata hivyo, kiuhalisia, doxing huhusisha udukuzi kwa maana ya kutafuta taarifa binafsi za mtu aidha zilizopo hadharani au kwa kumdukua, kisha kuzichapisha mtandaoni kwa dhamira ovu.

Tangu atimuliwe na Chadema, Mlawa amekuwa akijitahidi sana kukihujumu chama hicho na viongozi wake, huku jitihada za makusudi zikielekezwa kwenye kesi dhidi ya Mheshimiwa Mbowe. Kinachochochea hujuma hizo ni chuki kubwa kabisa aliyonayo dhidi ya chama hicho.

Kwa bahati mbaya ni kama anashinda katika vita hiyo ya chuki. Yayumkinika kuhitimisha kuwa Chadema wameshindwa kumdhibiti mtu huyo licha ya kuwa na nyenzo kadhaa dhidi yake.

Wajuzi wa mambo wanasema kuwa “viongozi wengi (wa Chadema) wanamuogopa kwa sababu anajua siri zao nyingi.” Lakini pengine wameamua kumpuuza tu kwa sababu si mtu muhimu kihivyo.

However, vyovyote ilivyo - iwe anaogopwa au anapuuzwa - athari za kumpa uhuru wa kuhujumu chama hicho na viongozi wake ni kubwa. Uongo usipokemewa unaweza kugeuka kuwa ukweli.

Chadema kama chama cha siasa inahitaji kuaminika na kuaminiwa. Jitihada zozote dhidi ya kuaminiwa na kuaminika kwake zinapaswa kukabiliwa kwa nguvu zote. Kwa maana hiyo, ni muhimu kwa chama hicho kutafakari upya mkakati wake dhidi ya hujuma za wazi za Mlawa.

Lakini jambo moja ambalo viongozi na wanachama wa Chadema ni kama wanakwepa kulichimba ni ukweli kwamba aliyempaisha Mlawa hadi kufikia alipo sasa anafahamika. Ni Maria. Hata hivyo, sio tu amekaa kimya wakati Mlawa anawachafua viongozi wa Chadema bali hajawahi kumkemea.

Maria anafahamiana na Jack CEO wa Twitter, na kwa kufahamiana huko, ndio alimwezesha Mlawa kuwa verified. Kwanini basi anashindwa kumripoti mtu huyo kwa Jack kutokana na orodha ndefu ya hujuma anazofanya dhidi ya Chadema?

Kama hana pa kuanzia, basi apewe twiti HII na HII ambayo imekiuka kanuni za faragha za Twitter zinazokataza kukweka taarifa binafsi za mtu hadharani pasi idhini yake. Mlawa ameweka namba za Mheshimiwa Mbowe hadharani bila idhini yake.

Nihitimishe kwa kutanabaisha kuwa baadhi yetu japo sio wana-Chadema tunaumizwa sana na madhila yanayomkumba Mheshimiwa Mbowe. Hata hivyo, hilo la uhuni wa Serikali kumbambikizia kesi lipo nje ya uwezo wa wananchi wa kawaida. Lakini hili la hujuma za Mlawa lipo ndani ya uwezo wa Chadema.