#Coronavirus: Mbinu/Nyenzo Za Kujengea Uimara Nyakati Za Hofu/Shaka

Kuanzia wiki hii nitakuwa nikikuletea mada mbalimbali za "jinsi ya kuwa mtu imara katika nyakati za hofu/shaka kama hizi za janga la korona."

Kwa lugha ya kitaalamu, mada zitalenga kukupatia mbinu/nyenzo za "personal development" kama mkakati wa kukabiliana na janga la korona.

Mada hizi zitakuwa fupi, na za lugha nyepesi kueleweka. Endapo utahitaji ufafanuzi, usisite kunishtua.

Mada ya kwanza ni utangulizi. Najaribu "kukushawishi" Kwanini nyenzo/mbinu hizi ni muhimu kwa wakati huu na pengine hata baada ya janga hili.

Mie ni bachela. Naishi peke yangu. Laiti nikiwa mbinafsi, naweza kirahisi tu kusema "ah hiyo korona na ije tu, maana hata ikiniondoa hakuna atakayepata hasara."

Lakini kuwa bachela hakumaanishi kutokuwa na ndugu. Hofu yangu kubwa kuhusu korona sio nini kitachotokea kwangu bali kwa ndugu, jamaa na marafiki na hata jamii kwa ujumla.

Kwahiyo Funzo hapa, endapo nawe ni bachela kama mie, ni kutokuwa mbinafsi. Kwamba usifikirie korona kuhusu wewe tu bali pia ndugu, jamaa, marafiki na jamii kwa ujumla.

Na kutokuwa mbinafsi wakati huu kutakuwezesha pia kuchukua maamuzi sahihi yatakayopelekea kuepusha maambukizi kwa watu wengine.

Ni kama kutokuwa mbinafsi kwa mwathirika wa ukimwi, au TB, au maradhi mengine ya kuambukiza.

Nimesema mie ni bachela. Lakini ukiwa na familia, mbinu/nyenzo hizi za "kuwa mtu imara katika nyakati za shaka/hofu" ni zaidi ya muhimu. Kama wewe ni baba maana yake familia yakuangalia kupata uongozi wako. Unakuwa kama Magufuli anavyoangaliwa na Taifa kutoa uongozi kwa taifa.

Ni wazi kuwa huwezi kutoa uongozi kwa familia kama wewe mwenyewe umejaa hofu na mashaka. Au kibaya zaidi, endapo unapuuzia uzito wa janga la korona.

Lakini pia kwa wote - mabachela na wasio mabachela - nyenzo/mbinu hizi ni muhimu pia kwa maandalizi ya wakati ujao (future).

Japo hatujui lini korona itaondoka, yayumkinika kuhisi kuwa ikiondoka itatuachia hali mbaya mno hasa kiuchumi. Kuna watu watapoteza ajira, kuna watakaofilisika kwenye biashara, na hatari kama hizo.

Baadhi ya mbinu/nyenzo hizo zaweza kukusaidia kujiajiri endapo utapoteza ajira, "kukurejesha relini," na vitu kama hivyo.

Fuatana nami katika safari hii. Tukutane next time.

Ndimi mtumishi wako,

Evarist Chahali