Chadema vs Ndugai: Nani Anasema Ukweli, Anaongopa?

Sakata la “wabunge 19 wa Viti Maalum wa Chadema,” litabaki kuwa moja ya songombingi za kisiasa zilizodumu kwa muda mrefu. Hata hivyo, kuna namna rahisi tu ya kumaliza sakata hilo.

Kwa kifupi kabisa, sakata hilo lilianza kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza majina ya wanachama 19 wa Chadema ambao kwa mujibu wa maelezo ya Tume hiyo, walipitishwa na chama hicho.

Mara baada ya NEC kutangaza majina hayo, Spika Job Ndugai aliharakisha kuwaapisha kuwa wabunge kamili wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na wakati wa kuapishwa, mmoja wa wabunge hao, Halima Mdee, aliushukuru uongozi wa Chadema kwa kuwateua wao 19 kukiwakilisha chama hicho.

Siku chache baadaye, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kutamka bayana kuwa yeye kama kiongozi mwenye dhamana ya kuwasilisha majina ya wabunge wa viti maalum huko NEC,hakuwahi kufanya kitu hicho. Maana yakehapa ni kwamba NEC waligushi majina hayo. Na ikumbukwe kuwa kugushi ni kosa la jinai.

Baadaye tena, Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe aliongoza kikao cha dharura wa Kamati Kuu ya chama hicho, ambapo kilihitimishwa na mkutano na waandishi wa habari. Mbowe alitangaza akuwa Chadema imewafuta uanachama akina Halima Mdee. Hata hivyo, alitanabaisha kuwa milango ipo wazi kwa wao kukata rufaa.

Siku chache baadaye, Halima Mdee na wenzake nao waliitisha mkutano na waandishi wa habari na kudai kuwa wao kama “wabunge 19 wa viti maalum kwa tiketi ya Chadema” waliteuliwa kihalali. Kadhalika, alisema kuwa watakata rufaa kwa Baraza Kuu la Chadema kupinga maamuzi ya Kamati Kuu ya chama hicho iliyowavua uanachama.

Kinachoendelea kusubiriwa ni maamuzi ya Baraza Kuu la chama hicho ambalo, kwa bahati mbaya au pengine makusudi, haijulikani litakutana lini.

Hata hivyo, kuna vitu vikuu vitatu hivi.

Kwanza, endapo ni kweli kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi iligushi majina hayo, kwanini Chadema hawafikisha suala hilo mbele ya vyombo vya sheria? Ni kweli kwamba mara kadhaa huko nyuma vyombo vya sheria vimekwenda kinyume na taratibu dhidi ya Chadema lakini kwa minajili ya kujitoa lawama, ni muhimu kwa chama hicho kuchukua hatua za kisheria.

Pili, kwamba Ndugai anaendelea kuwakumbatia akina Halima Mdee sio tu ni jambo lisiloshangaza bali pia ana sababu muhimu ya kufanya hivyo. Sio jambo la kushangaza kwa sababu chuki zake dhidi ya Chadema zipo wazi. Ni kupoteza muda kumlaumu mtu anayekuchukia.

Lakini hata tukiweka chuki zakekando, ukweli ni kwamba yeye aliletewa tu majina na NEC. Kwahiyo kimsingi hana kosa kuwatetea wabunge hao kwa sababu wabunge wote huidhinishwa na NEC. Na hii inarejesha tena umuhimu kwa Chadema kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Tume hiyo.

Tatu ni rufaa ya akina Halima Mdee. Binafsi nimebahatika kuongea na Mbowe na Mnyika kwa nyakati tofauti, na wote wameeleza kuwa lojistiki za kuitisha Baraza Kuu ni ngumu, na katika mazingira ya kawaida sio rahisi kwa chama hicho kuitisha kikao hicho kikubwa kabisa ghafla ghafla.

Hata hivyo, niliwaeleza wote wawili kwamba kasoro kubwa imekuwa kwenye mawasiliano. Kwamba kinachohitajika sio kukaa kimya au kuendelea kumlaumu Ndugai - ambaye chama hicho kinafahamu fika chuki zake dhidi yao - bali kuwaeleza wana-Chadema na Watanzania wengine kuhusu lini wanatarajia kuisha kikao cha Baraza Kuu na kutolea hukumu rufaa ya akina Halima Mdee.

Nihitimishe makala hii kwa kuwasihi wana-Chadema kutofanya mambo kama wenzao wa CCM, kwamba kila anayehoji kuhusu suala hilo au kuulizia mustakabali wake basi anakitakia mabaya chama hicho, au katumwa na CCM. Chadema ni chama cha KIDEMOKRASIA na maendeleo, na demokrasia ni pamoja na kuendesha mambo kwa uwazi.

Jumma Mubarak kwa ndugu zangu Waislam mliopo kwenye mfungo wa Mwezi Mtukufu.