Bashite Kupigwa Marufuku Marekani, Mlengwa Ni Baba Yake (Magufuli)

Kuna Dalili Japo Kiduchu Za Shinikizo Kutoka Nje Dhidi Ya Utawala Wa Kidikteta Wa Magufuli

Jana ilikuwa siku ya mwisho wa mwezi Januari, mwazi wa kwanza kwa mwaka huu 2020, ambao kwa Watanzania una umuhimu wa kipekee. Oktoba - miezi minane tu kutoka sasa - Watanzania watakuwa na fursa adimu dhidi ya kumhukumu Rais Magufuli na utawala wake wa kidikteta.

Na jana itabaki kwenye kumbukumbu za Watanzania wengi baada ya serikali ya Marekani kutangaza kwamba inamzuwia Daudi Albert Bashite kuingia nchini humo.

Kama lugha haipandi, alichoandika Waziri wa Mambe ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo, ni hiki,

Leo tunamtangaza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Christian Makonda kuwa haruhusiwi kuingia Marekani kutokana na kujihusisha kwake na ukiukwaji wa hali ya juu wa haki za binadamu. Tunatatizwa sana na kuzorota kwa heshima kwa haki za binadamu na utawala wa sheria nchini Tanzania.

Kabla ya kwenda mbali nakuomba urudie kusoma mstari unasema “kujihusisha kwake na ukiukwaji wa hali ya juu wa haki za binadamu.” Je ni matukio gani yaliyopelekea Wamarekani kuhitimisha hivyo?

Anachoongelea mdau ni hiki👇

Binafsi nimeshasikia mara kadhaa kuhusu unyama wa Bashite. Miongoni mwa taarifa nilizonazo ni kwamba amewatupa jela mamia kama si maelfu ya watu kwa sababu tu ya chuki zake za kipumbavu. Kadhalika, inaelezwa kuwa Bashite anahusika na “kupotea” kwa watu kadhaa. Sambamba na hilo, yaaminika kuwa mwanasiasa huyo kipenzi cha Rais Magufuli - licha ya kufoji jina na cheti cha kidato cha nne - ndiye mwasisi na kiongozi mkuu wa #WatuWasiojulikana, genge la kiharamia ambalo limewafanya Watanzania kuishia kwa roho juu katika muda wote wa utawala wa Rais Magufuli.

Lakini huhitaji kuwa na uelewa kuhusu uendeshwaji wa nchi kubaini kwamba hakuna jambo linalofanywa naBashite bila ridhaa ya “baba yake,” yaani Rais Magufuli. Kwa mantiki hiyo, hukumu ya Wamarekani dhidi ya Bashite kwamba anajihusisha na ukiukwaji wa hali ya juu wa haki za binadamu ni hukumu kwa Rais Magufuli maana sote twajua kuwa sio tu ndiye anayempa jeuri “mwanae” Bashite, bali pia ndiye anayempa maagizo.

Isingewezekana kwa Marekani kumwekea zuio Rais Magufuli lakini wamemgusa kwa kumwadhibi mwanae kipenzi. Na ndio maana hisia zangu za kijasusi zinaniambia kuna uwezekano wa Rais Magufuli kulipa kisasi

Unaweza kujiuliza “kwani kumzuwia Bashite kwenda Marekani kuna athari gani kwake?”

Lakini hatua hiyo ya Wamarekani inaweza kuwa mwendelezo wa dalili za matumaini adimu kuhusu uwezekano wa Rais Magufuli kung’olewa madarakani (kwa njia halali, ofkoz).

Na “loba” hiyo ya Wamarekani dhidi ya Bashite imekuja siku moja tu baada ya Rais Magufuli “kupewa za uso” na Benki yaDunia iliyoamua kuzuwia mkopo wa dola za kimarekani milioni 500, zuio lililotokana na kelele za baadhi ya Watanzania kwa taasisi hiyo ya kimataifa ya fedha, kuhusu usikukwaji mkubwa wa haki za binadamu hukumfano rahisi ukiwa kauli ya Rais Magufuli kuzuwia wanafunzi wa kike wanaopata ujauzito wasiendelee na masomo.

Awali “mzee wa mipasho” alishaanza kuleta ngebe

Nimeshawahi kuandika mara kadhaa huko nyuma kuwa forces mbili muhimu zinazoweza kuleta mabadiliko kusudiwa - kwa mfano kumng’oa Magufuli kwa njia halali - ni viongozi wa dini na nchi/taasisi wahisani.

Unfortunately viongozi wetu wengi wa dini “wameshanunuliwa” Sauti pekee ni za akina Baba Askofu Dkt Bagonza na wengine wachache.

Kuhusu nchi/taasisi wahisani, hawa wanaweza kuwa na mchango mkubwa katika kusaka mabadiliko kusudiwa.

Nihitimishe uchambuzi huu kwa kurudia kutamka kuwa mwezi Januari umeisha vyema sana kwa habari za Wamarekani kupiga loba Bashite, tukio ambalo sie wengine tunaona kuwa mlengwa ni Magufuli mwenyewe na Bashite ni kisingizio tu.

Uchambuzi huu ni endelevu. Nitaandika tena kutapojitokeza mrejesho mpya.

Nawataki wikiendi njema

Ndimi mtumishi wako,

Evarist Chahali