Barua Ya Chahali Toleo la Pili

Bombadia Changa La Macho?

Karibu tena katika toleo jingine la “Barua Ya Chahali,” inayokuijia kila wiki ikisheheni habari, elimu na burudani.

Nadhani umeona mabadiliko kati ya barua hii na ile ya wiki iliyopita. Ni kwamba nimeamua kubadili jukwaa. Uzuri wa jukwaa hili jipya ni kwamba unaweza kusoma matoleo yaliyopita ya barua hii kwa kutembelea HAPA.

Wiki hii tuongelee masuala mawili yanayotawala anga za habari za Tanzania yetu. Suala la kwanza ni ‘bifu’ kati ya Spika wa Bunge Job Ndugai na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Assad.

Kwa kifupi, chanzo cha ‘bifu’ hili ni kauli ya Profesa Assad kuwa “bunge ni dhaifu.” Na si kwamba alitoa tuhuma kiholela bali alitoa mifano hai kusapoti hoja yake. Alieleza kuwa Bunge hili la Ndugai limekuwa likizembea kuhoji matumizi yasiyoeleweka ya serikali ya Magufuli. Hivi unajua kuwa huo uwanja wa ndege wa kimataifa unaojengwa kijijini kwa Magufuli huko Chato, fedha za ujenzi hazijaidhinishwa na Bunge? Je wajua hata ununuzi wa hizo ndege zinazofikia sita sasa “unafanyika kiholela” kwa maana ya kutopata ridhaa ya Bunge wala kuhojiwa.

Na hadi muda huu, Bunge la Ndugai limekalia kimya “upotevu” wa shilingi TRILIONI MOJA UNUSU ambazo serikali ya Magufuli “imezitumia” bila maelezo ya kueleweka. Na kwa hakika wala haijulikani kama zilitumika au zilioptea au ziliibiwa. Na bunge limekaa kimya. Kuna taarifa mpya zinadai kuna fedha nyingine takriban shilingi TRILIONI NNE nazo hazijulikani zimetumikaje lakini Bunge la Ndugai lipo kimya.

Ila hili ‘bifu’ kimsingi sio la Ndugai na Profesa Assad bali Spika anatumika tu kwa maagizo ya Magufuli, ambaye vyanzo vinaeleza kuwa hamtaki CAG Assad. Na sababu ya kutomtaka msomi huyo ni ukweli kwamba yupo makini sana katika utendaji kazi wake. Hapendi kuingiliwa wala sio mtu wa kuyumbishwa. Sasa Magufuli anapenda watu anaoweza kuwapelekesha atakavyo.

Kwa uelewa wangu wa siasa za Tanzania, mwisho wa suala hili sio mzuri kwa Ndugai na Magufuli. Suala hili litasaidia kuwafumbua macho Watanzania kuwa UFISADI UMERUDI. Na pengine sio kwamba umerudi bali ulikuwepo na haukusikika tu.

Tofauti ya ufisadi katika Awamu hii ya Magufuli ukilinganisha na Awamu ya Nne ya Kikwete ni kwamba kwa Kikwete ilikuwa kama “fursa sawa kwa kila anayetaka kufisadi.” Kama ulikuwa na uwezo wa kuingiza unga, ingiza. Kama ulikuwa na uwezo wa kusafirisha unga, safirisha. Kama ulikuwa na uwezo wa kutengeneza noti feki, tengeneza. Kama ulikuwa na uwezo wa kuuza watu huko Uarabuni, uza. Kikwete alikuwa bize na safari zake huku nchi ikijiendesha yenyewe kwa “autopilot.”

Kwa upande wa Magufuli, amejitahidi kubana mianya mbalimbali ya ufisadi, lakini sio kwa maslahi ya nchi bali kwa ajili ya genge lake dogo la marafiki zake kutoka Kanda ya Ziwa. Kwa mujibu wa taarifa, ufisadi uliokwishafanyika katika miaka mitatu ya Magufuli unazidi hata uliofanyika miaka 10 mizima ya Kikwete. Na hapo hatujaongelea udikteta.

Na kuhusu ufisadi, ndio tunagusia mada ya pili ambayo ni suala la BOMBADIA.Jana mliona kwenye ukurasa wangu wa Insta niliweka post yenye maneno “changa la macho.”

Kwa kweli, katika mazingira ya kawaida tu, haiingii akilini kwa ndege tunazoambiwa ni mpya, hazina hata muda mrefu tayari zinapelekwa matengenezoni, tena kwa gharama ya mabilioni. Basi angalau wangetuambia kuwa ndege hizo ni mitumba kwa hiyo zitakuwa zikihitaji matengenezo ya mara kwa mara.

Lakini jingine linalokera ni kwamba kwa vile fedha za ununuzi wa ndege hizo ulifanywa kiholela, hata hizi za matengenezo nazo zimetolewa kiholela tu. Na hakuna wa kuhoji kwa sababu Ndugai hana jeuri ya kulifanya Bunge analoongoza lihoji matumizi ya serikali ya Magufuli.

Naomba ieleweke kuwa mie ni miongoni mwa watu ambao wangetamani sana kuona Air Tanzania ikipaa kimataifa kama wanavyofanya wenzetu wengi lakini hiyo haimaanishi kuwa fedha za walalahoi zitumike ovyo kwa vile tu “mindege” hiyo ni muhimu.

Halafu kwa busara tu, kipaumbele kwa sasa ni kuwasaidia walalahoi wajikwamue kiuchumi kwanza, kunoresha huduma za jamii, kukabiliana na changamoto za ukosefu wa ajira, nk kisha ndio tugeukie ununuzi wa “mindege.” Kuna faida gani kuwa na “mindege” sita ambayo wananchi wa kawaida wataishia kuiangalia tu hewani kwa vile ni masikini wa kutupwa wasioweza kumudu japo nauli ya bodaboda?

Na hata tungekuwa tuna uwezo wa kununua “mindege” hata mia, lakini sio kwa minajili ya kubeba nyama ya mbuzi kwenda Dubai. Huu ni uhuni. Na uhuni huu unapaswa kukemewa kwa nguvu zote.

Basi naomba niishie hapa, maana mie nikipandisha mdadi wa uzalendo nakuwa kama nimemeza albamu ya muziki 😁

Wiki ijayo naahidi kufupisha barua, maana hii imekuwa ndefu mno. Usisite kunitumia ushauri au hata kunikosoa. Pia naomba kukuhakikishia kuwa sio kila wiki tutaongelea ishu za siasa. Nina mada kama milioni moja hivi za kukushirikisha.

Siku na wiki njema.

Wasalam,

Evarist