Baba Askofu Niwemugizi - moja ya sauti adimu za uongozi wa kiroho - Atahadharisha Kuhusu Korona

Eid Mubarak kwa ndugu zangu Waislam.

Nimekutana na bandiko hili la Baba Askofu Severine Niwemugizi huko Jamii Forums, nikaonelea ni vema kuwashirikisha.

Nawaza kivyangu kwa sauti. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika ibara ya 19 (2) inasema hivi: “Kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi, na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi”.
Kwa kuwa ni hivyo, kwa maoni yangu:

1). Kiongozi wa dini akisubiri aambiwe na mamlaka ya nchi aendeshe ibada au asiendeshe ibada, kufungua au kufunga kanisa hajui haki na wajibu wake.

2). Katika mazingira ya sasa ya janga la COVID 19 kila kona ya dunia ambapo mikusanyiko ya watu wengi inasemekana kuwa hatari kwa maambukizi ya virusi, mtu kusema mikusanyiko ya makanisani au misikitini siyo hatari kwa maambukizi anaudanganya umma na kuuweka hatarini. Sidhani kama Korona inakuogopa huko.

3). Kiongozi wa dini akifikiri kwamba itakuwa halali tu kwa mamlaka ya nchi kusema mikusanyiko hiyo isitishwe na siyo halali kwa kiongozi wa dini kusitisha kwa muda anaepa wajibu wake.

4). Nyuki wakali wakiingia kwenye nyumba ya ibada, kiongozi wa dini ukawaambia waamini wako ingieni tu kwa ibada hamtaumwa kwa kuwa Mungu yuko humo, utakuwa unawatakia mema waamini? Wakiumwa na hata akafa mtu lawama imwendee nani? Mimi najua hata mshumaa ukiobarikiwa unaungua ukiuwasha!

5). Kuna msemo “don’t copy and paste” (usinakili na kuchapisha), kwa ufupi usiige. Ninamfahamu aliyenakili tamko langu kuhusu mali kwa mapadre wa jimbo na kulichapisha kwenye kitabu chake, tena bila kuomba ruhusa kwangu, nami sijamlaumu. Sijamlaumu kwa sababu siyo kosa kuiga jambo zuri. Wataalamu wanatuambia kuna nadharia ya “the best practices”. Kwamba ukiwa na lako jambo si vibaya kujifunza na kutenda ukifuata njia, miongozo au taratibu nzuri zilizowekwa na mamlaka fulani kadiri ya mazingira. Kutotaka kujifunza kwa wengine ni alama ya kiburi, na unaweza kuangamia kwa kung’ang’ania ujinga wako. Bila shaka mjinga naye huwa anaamini yeye ndiye anajua zaidi ya wote.

6). Naamini taarifa na takwimu sahihi ni muhimu kwa kupanga mipango ya maendeleo ya mtu na taifa. Bila hayo ni vigumu kufanya tathmini na kupanga. Naamini kukosekana kwa taarifa na takwimu za kuaminika kuhusu hali ya Korona kuna hasara zaidi kuliko faida.

7). Viongozi wa dini tutende tulivyojifunza namna ya kufanya kazi zetu badala ya kuambiwa cha kufanya na watu ambao hawajui tulifundishwaje huko chuoni.

Niko tayari kupigwa kwa mawe. Bwana awabariki watakaofanya hivyo, maana alisema: “Naam, saa yaja atakapodhania kila awauaye anamtolea Mungu ibada. Na hayo watawatenda kwa sababu hawakumjua Baba wala mimi” (Yn 16:2)

Ndimi mtumishi wako,

Evarist Chahali