Askofu Mwamakula Amuonya Magufuli, Spika na Wabunge Kuhusu Kuondoa Ukomo wa Urais

Naiwasilisha kama nilivyokutana nayo huko Jamii Forums:

ONYO KWA WABUNGE, SPIKA, NA RAIS MAGUFULI

Nimemsikia Mbunge mmoja akiongea Bungeni akitaka Bunge libadilishe Katiba ya Nchi ili kumfanya Rais Magufuli aendelee kutawala hata baada ya kumaliza kipindi chake cha kikatiba cha miaka 10. Kama hilo halitoshi, Spika Ndugai amesikika akimhakikishia Mbunge husika kuwa kazi hiyo ya kubadilisha kipengere cha Katiba kinachoweka ukomo wa Rais kuwa miaka 10 itafanywa na wao wote [Wabunge] katika Bunge lijalo. [Spika anaonekana kuwa na uhakika kuwa Rais Magufuli na wao wenyewe watachaguliwa tena katika Uchaguzi wa Mwaka huu].

Ninapenda niwalejeze Spika Ndugai, Wabunge, na Watanzania wote kwa ujumla kuhusu habari ya Mfalme Darius na Bunge lake katika Dola ya Uajemi (Persia) na Umedi (Mede) yapata miaka 2500 iliyopita.

Mfalme Darius aliunda Baraza (Bunge) lake lenye Wajumbe 120 aliowateua yeye wenyewe. Katika hali ya kutaka kumkomoa Danieli ambaye alionekana kuwa na uwezo mkubwa wa kiuongozi kuwazidi wao, Wabunge wenye nia ovu walianzisha mikakati ya siri ya kutaka kumnyamazisha Danieli. Mikakati yote iliposhindwa, waliamua kutunga sheria ambayo walijua kuwa itamfurahisha Mfalme Darius lakini huku ikiwa na lengo lililojificha la kumnyamazisha kabisa Danieli kwani walijua kuwa hatima ya sheria ile ilikuwa ni kifo cha Danieli. Walitunga sheria ya kutukuza mawazo ya Mfalme kwa kusifu na kuabudu mradi au sanamu aliyoitengeneza Mfalme. Walimshawishi Mfalme aitie muhuri au aisaini sheria ile. Wakapitisha Azimio la Ki-Bunge la kuzuia mtu ye yote au mamlaka ye yote kutangua sheria ile. Hata hivyo, Mungu hakuruhusu uovu ule na akaingilia kati. Wabunge wote waliopitisha Azimio lile waliuawa pamoja na wake zao na watoto wao lakini Danieli alipona na aliendelea kustawi zaidi. Kwa uelewa zaidi kuhusu habari hii someni Biblia Takatifu katika Kitabu cha Danieli 6:1-28.

Tunapenda kuwaonya na kuwatahadharisha Wabunge na watu wote wanaofanya mikakati ya kutaka kutunga Sheria mbalimbali zenye hila mtambuka ikiwemo kutaka kumfurahisha Rais aliyeko madarakani lakini lengo kuu lililojificha likiwa ni kulinda matakwa yao binafsi kwa njia ya kuwazuia au kuwanyamazisha watu wengine wanaoonekana kuwa ni tishio kwa nafasi zao na matakwa yao! Mungu anatoa onyo kali kwa watu na viongozi wa namna hiyo (Isaya 10:1-4).

Ushauri wangu kwa Rais Magufuli ni kuwa awe makini sana na watu ambao kila kukicha wanapenda kumsifia tu pasipo hata kumtahadharisha. Akiwafuata watu wa namna hiyo, basi ajue kuwa anaikaribisha hasira ya Mungu kwake mwenyewe na kizazi chake!

Ninamshukuru Mungu mwenye rehema nyingi kwa kunipa ujasiri wa kuyaandika haya (Ezekieli 33:1-20).

Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!

Askofu Mkuu Emmaus Bandekile Mwamakula - Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania & Afrika Mashariki na Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Makanisa ya Moravian ya Uamsho Dunianie