Askofu Bagonza Akerwa na Kukemea Kauli Ya Kangi Lugola Kuwa 'Magufuli ni Yesu.'

Anaandika Baba Askofu Benson Bagonza, PhD, katika ukurasa wake wa Facebook

Image may contain: 2 people, text that says "E EATV East Africa TV 17 mins "Rais Magufuli amekuwa kama Yesu Kristo, Watanzania wanamlilia na kumfuata na ndiyo maana hata aliponitengua nilisema, ulinipa heshima ya huu Uwaziri leo umeutwaa Uwaziri ulio wako jina la Magufuli libarikiwe, tunapokuwa na Rais huyu hatutakiwi kuingia kwenye mijadala ya kumtafuta mwingine" -Kangi Lugola. #Bungeni"

KUFURU HAINA KINGA

Kwa Wakristo, dhambi isiyosameheka katika Agano Jipya ni kumkufuru Roho Mtakatifu. Katika Agano la Kale ni dhambi ya ibada ya sanamu (idolatry). Amri ya kwanza aliyopewa Musa inasema, "Mimi ni Bwana Mungu wako, usiwe na miungu mingine" (Kutoka 20:3-6). Kufuru haina kinga duniani na mbinguni. Ghadhabu ya Mungu iko wazi katika misahafu yote.

Tuzitendee haki kumbukumbu zetu.

1. Mjinga mmoja akatumia uhuru wake vibaya huko Denmark. Akachora katuni yenye kufuru. Dunia nzima iliwaka moto.

2. Mpuuzi mmoja huko Marekani akachoma msahafu. Hakuna jiwe lililosalia juu ya jiwe.

3. Huko Mbagala utoto ukavuka mipaka, msahafu ukakojolewa; amani yetu ilitoweka, majivu yakawa majivu.

4. Huko Sumbawanga, msimu wa uchaguzi kama huu, ulimi wa mmoja ukateleza, akaufananisha UTATU mtakatifu na mafiga matatu ya chama chake. Hapakutosha. Mzee Pinda, mtu wa amani ana cha kusimulia mpaka leo.

Mungu wetu hafananishwi, halinganishwi, na hashindanishwi.

Ni ibada ya sanamu kupenda kitu kingine kuliko unavyompenda Mungu wako. Ni ibada ya sanamu kuchukia kitu kingine kuliko unavyomchukia shetani. Ni ibada ya sanamu kumlinganisha muumbaji na uumbaji wake.

Hatumtendei haki Mungu kumlinganisha na aliowaumba.

Hatuwatendei haki tunaowapenda kuliko tunavyompenda Mungu aliyewaumba.

ITOSHE. Walinzi na waangalizi wa imani, kama hatuwezi kukemea hili basi angalau tuchukie na tuonekane tumechukia.

NAKEMEA na NIMECHUKIA.