Askofu Aongelea Suala la Wanaharakati vs Serikali Kuhusu Mkopo wa Benki ya Dunia

SAKATA LA MHESHIMIWA ZITTO, SERIKALI NA BENKI YA DUNIA LITUFUNGUE MACHO KUHUSU UMUHIMU WA MARIDHIANO YA KISIASA NCHINI

Nimeona barua iliyoandikwa na Mheshimiwa Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini kwenda Benki ya Dunia kuiomba Benki hiyo izuie au iahirishe kutoa mkopo kwa Serikali ya Tanzania uliokuwa unaelekezwa katika sekta ya elimu nchini. Pia, nimesikiliza mahojiano kati ya Mheshimiwa Zitto na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuhusiana na jambo hilo. Kwa ujumla Mheshimiwa Zitto ametoa tuhuma au sababu kadhaa zikiwemo;
Serikali kuweka Sera ya kuwabagua wasichana wanaopata uja uzito wawapo shuleni, Serikali kuminya Uhuru wa Kujieleza na Vyombo vya Habari; Serikali kuminya Demokrasia kwa kuzuia mikutano ya hadhara kwa vyama vya upinzani, kuenguliwa kwa wagombea wa vyama vya upinzani katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Novemba 2019, na hofu ya vyama vya upinzani kuwa Fedha hizo zilizoombwa zitatumiwa na Serikali ya CCM kukinufaisha CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.

Kwa ujumla, kwa muono wangu, nimejiridhisha kuwa huu ni mzozo wa kisiasa na unaakisi malalamiko ya vyama vya upinzani dhidi ya Serikali ya Tanzania. Benki ya Dunia imetumika kama sehemu ya kuzungumzia mgogoro wa kisiasa na viongozi ambao wameshindwa kufikia muafaka katika ardhi ya nchi yao.

Bila shaka Benki ya Dunia itaweza kutumia weredi na uzoefu wake katika kufikia maamuzi yake ya mwisho kuhusiana na tuhuma hizo dhidi ya Serikali ya Tanzania. Ni matarajio yetu kuwa Benki ya Dunia itapenda kujiridhisha zaidi kwa kusikia pia ukweli kutoka upande wa Serikali ambayo itabidi ipangue kwa ushahidi hoja zilizotolewa na Mheshimiwa Zitto.

Kwa kuwa katika hatua hii hatujaziona hoja za utetezi za Serikali ya Tanzania, tutajikita zaidi katika kuangalia hisia, mazingira, na saikolojia inayozunguka hoja za Mheshimiwa Zitto. Ikumbukwe kuwa Zitto ni miongoni wa viongozi wa vyama vya upinzani ambao wamekuwa wakiilalamikia Serikali ya Tanzania kwa mambo mbalimbali yakiwemo ya kukandamiza upinzani nchini.

Hivi katika hali ya kawaida Serikali itegemee kuungwa mkono na wanasiasa ambao imewaburuza Mahakamani kwa kesi za uchochezi? Viongozi wa vyama vya upinzani ambao kwa miaka yote minne wamepigwa marufuku kuendesha mikutano ya hadhara watakuwaje na uzalendo kwa miradi ya Serikali ambayo wanahisi itazidi kuijenga na kukiimarisha chama tawala wakati vyama vya upinzani vikidhoofu? Viongozi wa upinzani ambao wamenyimwa haki ya kushiriki kuongoza Serikali za Mitaa kutokana na hisia kuwa wagombea wao wameenguliwa, wataungaje juhudi za Serikali ambayo wanaituhumu kuwafanyia dhuluma katika Uchaguzi huo? Wanasiasa ambao wanahisi kuwa hata vyombo vya habari havina uhuru wa kutoa taarifa kuhusu taarifa zao watatoaje ushirikiano kwa Serikali wanayodhani kuwa ndio iko nyuma ya mkakati wa kuminya uhuru wa kujieleza?
Kwa ufupi inaonekana Mheshimiwa Zitto anataka 'kumwaga mboga kwa kuwa wenzake wamemwaga ugali'! Hili haliwezi kutusaidia! Ni lazima tuingilie kati ugomvi huu ili tusilale na njaa!

Kwa ujumla, hapa tulipofikia ni matokeo ya vita vya kisiasa nchini ambayo imezidi kukua kila mwezi kutokana na siasa za ubabe, chuki na mabavu ambazo zimekuwa zikiendeshwa katika miaka ya hivi karibuni. Vita hii inaweza kuleta athari mbaya sana kwa uchumi na maendeleo nchini. Ni dhahiri kuwa matamko ye yote ya kukemea, kulaani, kupongeza au kuunga mkono upande wo wote katika mzozo huu hayataleta tija zaidi ya kuzidi kujenga ufa katika jamii yetu. Suala hili linahitaji suluhu ya kisiasa. Jamii inatakiwa ielewe madhara ya mkwamo wa kisiasa katika nchi hii na hivyo itoe shinikizo la kushinikiza Serikali na Viongozi wa Vyama vya Siasa kuingia katika maongezi ya maridhiano.

Katika vita ya kisiasa hakuna adui dhaifu kwani hata huyo aliye dhaifu anaweza kuleta madhara makubwa sana. Katika vita ya namna hii wote wanahitaji kuona haja ya kukwepa gharama! Kubaguana katika kuendesha siasa za nchi hii hakutalifadia taifa hili zaidi ya kuliharibu na kujenga chuki mbaya miongoni mwa jamii. Huko nyuma mimi na viongozi wengine wa dini tumeandika na kushauri sana kuhusu mambo haya. Tumeonya, tumekemea, na kushauri pasipo kuchoka.

Ninasimama tena katika zamu yangu na kusihi Serikali pamoja na viongozi wakuu wa vyama vya siasa katika nchi hii kuanza kufikiria umuhimu wa kukaa pamoja katika meza ya maridhiano. Fikra na mtazamo wa kikundi kimoja kula mkate mzima haziwezi kufanya kazi katika zama hizi. Wanasiasa, na Vyama vya Siasa lazima watambue na kukubali kuwa haiwezekani kupata ushindi wa asilimia zote katika zama hizi na hivyo kufanya utawala au uongozi shirikishi kutokuepukika. Kwa sasa tumeona haya ya Benki ya Dunia, hatujui huko mbele yatakuja mambo gani.

Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!

Askofu Mkuu Emmaus Bandekile Mwamakula - Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania & Afrika Mashariki na Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Makanisa ya Moravian ya Uamsho Duniani