Askofu Akemea Kauli ya Kipumbavu ya Bashite

Habari ya kutia matumaini kidogo ni kwamba kuna baadhi ya watumishi wa Mungu - japo wachache - wanajielewa na hawana uoga wa kukemea maovu.

Mfano hai ni tamko la Askofu Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania na Afrika Mashariki,Emmaus Mwamakula, lililotokana na twiti hii ya Bashite

Tamko la Baba Askofu ni hili

Mkuu wa Mkoa ni Mteule wa Rais na hivyo anamuwakilisha Rais au anawakilisha taswira ya Rais na Serikali kwa ujumla. Kipekee, nafasi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ni nafasi nyeti sana katika Taifa hili. Dar es Salaam ni kitovu cha dini, mila, siasa, biashara, itikadi, elimu, uchumi, uongozi na hata makabila. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam anatakiwa awe na dhana ya ulezi dhidi ya makundi hayo yote ili aweze kuyaongoza vizuri. Ndio maana haitakiwi hata kidogo kumdharau Mkuu wa Mkoa.

Nimestushwa sana na 'twiti' (imeambatanishwa) inayosambaa kuanzia leo mitandaoni yenye anwani ya Mheshimiwa Paul Makonda ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Kupitia 'twiti' hiyo, mwandishi anajinasibu kuwashughulikia wakosoaji wote wa Serikali kwa kutumia [kuwabambikia?] kesi za Utakatishaji Fedha na Uhujumu Uchumi ambazo hazina dhamana! Kauli hii inakuja siku chache baada ya wana harakati kadhaa na wakosoaji wa Serikali 'kutekwa' au 'kukamatwa' katika mazingira ya kutatanisha huku wakiwa hawajulikani walipo. Baada ya kelele nyingi kutoka katika kwa jamii ya Watanzania na Jumuiya ya Kimataifa, mamlaka kupitia Jeshi la Polisi, zilitoka hadharani na kutoa matamko kuwa zilikuwa zunawashikilia watu hao na wakafunguliwa kesi za Uhujumu Uchumi, Uakatishaji Fedha, nk. Miongoni ni Mwandishi wa Habari za Uchunguzi Erick Kabendera ambaye hali yake imeelezwa ni dhoofu huko mahabusu, ndugu Tito Magoti ambaye ni mfanyakazi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu.

Mwandishi wa 'twiti' hiyo anaonekana anakerwa sana uwepo wa wakosoaji wa Serikali. Anakwenda mbali zaidi kwa kuonyesha kutokufurahishwa na matokeo au maamuzi ya Mahakama dhidi ya watu hao hivyo anaona njia njia nzuri ni kuwapa kesi zisizokuwa na dhamana ili kuwakomoa na kuwanyamazisha kabisa. Anashindwa kuelewa kuwa ukosoaji ni sehemu tu ya Uhuru wa Kujieleza (Freedom of Expressions) na Uhuru wa Kujumuika (Freedom of Association) ambavyo kila binadamu huzaliwa navyo. Ndio maana kila mtoto anapozaliwa ni lazima alie ili kuthibitisha huo uhuru wake.

Tunapenda na tunasisitiza kuwa hakuna mamlaka au jeshi ambao walifanikiwa kabisa kuzimisha uhuru wa kujieleza duniani. Ukimzuia mtu kuongea hadharani ataongea kifichoni na ukimzuia kuongea kifichoni ataongea nafsini mwake! Ni hatari sana kujenga jamii ya watu wanaonung'unika, wanaokandamizwa, na waozuiwa hata kutoa mawazo yao. Tusiipeleke nchi yetu huko! Tunapenda kuwakumbusha watu wote kwenye mamlaka kuwa mamlaka kamili ipo mikononi mwa watu wa kawaida au wanyonge na haipo mikononi mwa vyombo vya dola au kwenye mamlaka au wenye fedha. Tusiwaze na wala kupanga kuhujumu watu katika maficho yetu (Mika 2:1-11).

Kama 'twiti' hiyo ni ya Mheshimiwa Makonda mwenyewe, basi kwa upole na unyenyekevu mwingi, tunamshauri atoke hadharani baada ya kutubu kwa Mungu awaombe pia msamaha Watanzania. Kama siyo 'twiti' yake, basi atoke pia hadharani aikane na hao walioiandika watafutwe nao wajitetee mbele ya vyombo vya sheria.

Mheshimiwa Makonda ni kiongozi kijana ambaye ndio kwanza ameyaanza maisha ya siasa na uongozi. Tunamshauri na kumuonya kuwa kama ni yeye 'aliyetwiti' hivyo, basi asirudie tena na ajitenge kabisa na siasa au uongozi wa mabavu na vitisho! Mtu, au jamii au taasisi ye yote inayojitanua kwa misingi ya kiburi, vitisho, kuminya uhuru na haki za watu haijawahi kusimama, haiwezi kuja kusimama, na haitaweza kuja kusimama (Nahumu 1:12a).

Kwa Watanzania wote kwa ujumla hasa mliokwazika na 'twiti' ya Makonda, tunawasihi sana kutokumchukia Mheshimiwa Makonda bali tumuombe Mungu atupe upendo wa dhati kwake uli tupate kibari cha kumuombea neema na rehema kwa Mungu.

Kwa wale ambao ni marafiki, washauri, na hata viongozi wake wa kiroho, tunaomba Mungu awape ujasiri wa kumshauri, kumwambia ukweli na hata kumuonya kwani kwa kufanya hivyo, mtamsaidia.

Mwisho, tunamsihi Mheshimiwa Makonda, apatapo ujumbe huu asipoteze muda kutumia mamlaka yake kutaka kujua 'maumbile' ya mwandishi. Anachotakiwa kufanya ni kutambua kuwa ujumbe huu umetoka kwa Askofu asimamaye katika zamu yake kama Habakuki (Habakuki 2:1) na kuwaonya wafalme na watawala (Ezekieli 33:-20). Mungu wetu humuonya ampendaye, humkweza mnyenyekevu, na humshusha kwenye kiburi. Ole wangu mimi kama nitaogopa kuwaonya na kuwaambia ukweli watawala na wenye mamlaka!

Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!

Askofu Mkuu Emmaus Bandekile Mwamakula - Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania & Afrika Mashariki na Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Makanisa ya Moravian ya Uamsho Duniani

Asante Baba Askofu.

Nimalizie kwa tangazo kuhusu vitabu vyangu

Ndimi mtumishi wako wako,

Evarist Chahali