[ #TumiaVPN] Tanzania Ya Magufuli ya Uchumi wa Kati Yatahadharishwa na Benki ya Dunia Kuhusu Ukubwa wa Deni la Taifa (Sh Trilioni 47!)

Nimekutana na habari hii kutoka gazeti la Mwananchi hapo jana. Naomba niiwasilishe kama ilivyo.

Benki ya dunia imeitahadharisha Serikali ya Tanzania juu ya ukubwa wa deni lake lililofikia trillion 47+ kwa rekodi mpaka mwezi Mei mwaka huu.

Imetaja japo deni bado ni himilivu lakini Tanzania lazima iwe makini maana linaelekea kutokuhimilika

Licha ya Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo inayotarajia kuboresha masisha ya wananchi, Benki ya Dunia imetahadharisha kuhusu ukopaji unaofanywa na Serikali.

Ingawa deni hilo bado ni himilivu, benki hiyo inasema umakini unahitajika kabla hali haijawa ngumu kwa Serikali kushindwa kutekeleza makubaliano.

Kwa sasa, taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha deni la nje linalohusisha lile la umma na sekta binafsi lilikuwa Dola 21.6 bilioni (takriban Sh49 trilioni) na la ndani ni Sh15.5 trilioni. Takwimu hizo ni mpaka Mei mwaka huu.

Hata hivyo, Benki ya Dunia inasema uwiano wa deni la Taifa na pato la taifa (GDP) kwa mwaka 2018 ulikuwa asilimia 40.1 zikiongezeka kutoka asilimia 37 za mwaka uliotangulia. Pamoja na ukweli huo, uwiano huo ni chini ya ukomo wa asilimia 70 unaopendekezwa kimataifa.

“Ingawa deni ni himilivu lakini ongezeko la mikopo ya kibiashara kutoka benki linapaswa kutazamwa kwa umakini,” inasomeka sehemu ya ripoti ya benki hiyo.

Hivi karibuni, Benki ya Dunia imeindua ripoti ya 12 ya hali ya uchumi Tanzania iliyoangazia umuhimu wa rasilimaliwatu katika kukuza utajiri ambayo pamoja na mambo mengine imetoa ushauri wa namna ya kuboresha ukuzaji uchumi na maisha ya wananchi.

Mwaka 2010/11 ripoti hiyo inasema mikopo kutoka benki za biashara ilikuwa asilimia nne tu ya deni zima lakini imeongezeka mpaka asilimia 30 mwaka 2016/17 hivyo kuipa Serikali gharama kubwa za marejesho.

Kutokana na ongezeko hilo, ripoti inasema Tanzania inatumia asilimia 43 ya mapato yake ya ndani kulipa deni la Taifa ingawa ulipaji wa deni la ndani umekuwa mdogo.

“Mei 2018 Serikali ilianzisha uhakiki wa madeni ya wakanadarasi na wazabuni ili kuharakisha ulipaji na Sh1 trilioni zilitengwa kwa ajili hiyo kwenye bajeti ya mwaka 2018/19 lakini kwenye nusu ya kwanza ya mwaka huo ni Sh322 bilioni pekee zilikuwa zimelipwa,” inasema ripoti hiyo.

Uuzaji nje

Kutokana na bei ndogo iliyopendekezwa na wanunuzi, Serikali ilizuia uuzaji wa korosho kwa kampuni zilizojitokeza mwaka jana na ikaamua kuzinunua yenyewe. Jeshi la wananchi lilihusishwa kwenye mchakato huo.

Kiasi kikubwa cha zaidi ya tani 200,000 za korosho zilizonunuliwa na Serikali hakikuuzwa nje ya nchi hivyo kushusha mapato ya fedha za kigeni kwa asilimia 3.9 kutokana na mapato ya zao hilo kushuka kutoka Dola 529.6 milioni hadi Dola 196.5 milioni.

Wakati uuzaji nje ukipungua kwa kiasi hicho, ununuaji uliongezeka kwa asilimia 7.8 kutoka Dola 2.7 bilioni hadi Dola 3.2 bilioni kulikochangiwa na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam.

“Hata hiyo, mapato yatokanayo na huduma hasa utalii yalifika Dola 189 milioni yakilinganishwa na malipo yaliyofanywa nje, Dola 56 milioni. Mapato hayo yalichangiwa na ongezeko la watalii na usafirishaji wa bidha kwenye nchi jirani,’ inasema ripoti hiyo.

Kushuka kwa akiba ya fedha za kigeni kumechangiwa na kupungua kwa uuzaji wa mauzo nje ya nchi kulikosababishwa na kutouzwa kwa korosho (page 20).

Utajiri wa wananchi umeshuka kutoka Dola 20,900 mwaka 1995 hadi Dola 17,451 mwaka 2014. (page 43).

Changamoto ya kwanza inayoifanya Tanzania ishindwe kukabiliana na umasikini hivyo kuboresha maisha ya wananchi wake ni kasi kubwa ya kuzaliana. Ongezeko la watu nchini ni asilimia 3.1 kwa mwaka, kiwango cha juu ikilinganishwa na asilimia 2.7 kwa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kupunguza idadi ya watoto kwa kila mwanamke, kuimarisha elimu kwa mabinti, kupunguza ndoa na mimba za utotoni na kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye shughuli za uchumi ni miongoni mwa njia za kukabili changamoto hiyo.

Udumavu na umasikini

Ingawa utajiri wa Tanzania umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 45 kwa miongo miwili iliyopita, kasi kubwa ya ongezeko la watu imeshusha utajiri wa kila mwananchi kwa Dola 3,500.

Mwaka 2014 utajiri wa Tanzania unaojumuisha thamani ya rasilimali zote ilizonazoukitoa madeni ulikuwa Dola 904.33 bilioni ukilinganishwa na Dola 624.99 bilioni mwaka 1995. Lakini, utajiri wa kila raia ulipungua kutoka Dola 20,900 mwaka 1995 hadi Dola 17,451 mwaka 2014.

Licha ya kupungua kwa utajiri wa kila mwananchi, idadi ya masikini imeongezeka pia kutoka milioni 12.3 waliokuwepo mwaka 2012 hadi milioni 13.3 mwaka 2016. Ndani ya miaka minne, masikini milioni moja wameongezeka.

Mtafiti na mchumi mwandamizi, Profesa Samwel Wangwe anasema hiyo inaweza kuwa imechangiwa na ukuaji mkubwa wa sekta zisizoajiri watu wengi zaidi.

“Watanzania wengi ni wakulima au wafanyabiashara wadogo. Tunahitaji mipango itakayowainua waliopo kwenye maeneo hayo ili kuufanya uchumi wetu uwe jumuishi,” anasema Profesa Wangwe.

Kuhusu ongezeko kubwa la watu, naibu waziri wa afya, Dk Fustine Ndugulile anasema kunachangiwa na mambo mengi ikiwamo jitihada za Serikali kuboresha huduma za afya hasa chanjo kwa watoto.

“Hata hivyo, udhaifu wa sheria na ukosefu wa elimu ni chanzo cha ndoa na mimba nyingi za utotoni,’ anasema Dk Ndugulile.

Mkurugenzi mkazi wa Benki ya Dunia nchini, Bella Bird anasema wananchi wanahitaji kuelimishwa ili kukabiliana na changamoto zilizopo. Elimu, anasema itawasaidia kuboresha maisha, kukuza kipato na kuwa na uzazi unaohimilika.

“Elimu ya mama ni muhimu kwa maendeleo ya baadaye ya mtoto kielimu na kiuchumi. Watoto milioni tatu chini ya miaka mitano nchini wana udumavu. Msichana mmoja katika kila watatu anaolewa akiwa na chini ya miaka 18 na mmoja katika kila wanne anazaa akiwa chini ya umri huo,” anasema Bella.

Ndimi mtumishi wako,

Evarist Chahali