Transcript:
MAELEZO YA ERICK KABENDERA KATIKA KIKAO NA WAANDISHI WA HABARI KILICHOFANYIKA LEO TAREHE 1 OKTOBA 2024.
Ndugu waandishi wa habari,
Nimewaita leo kwenye mkutano huu na vyombo vya habari kuwaeleza hatua inayofuata baada ya Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam kuifuta kesi ya madai (12799/2024) nilivyoifungua dhidi ya kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania Ltd mwezi Julai mwaka huu 2024.
Kabla ya kuelezea hatua nilizoamua kuchukua, ningependa kuwaelezea kwa kifupi msingi wa kesi yangu dhidi ya Vodacom.
Juni 29 mwaka 2019 nikiwa nyumbani kwangu Mbweni Mpiji, Dar es Salaam, nilivamiwa na watu wasiojulikana na kuzingira nyumba yangu. Baada ya purukushani wakajitambulisha kuwa wao ni askari kutoka vyombo tofauti vya dola ambao walikuja kunikamata kwa makosa ambayo hayakujulikana wakati huo. Hata hivyo, nikiwa ndani ya gari lao huku nimefungwa pingu, waliniambia maneno haya; “Wewe ni mjinga, umekataa kuunga mkono juhudi na sasa utakiona cha mtema kuni.”
Taarifa za kutafutwa kwangu na kuwa maisha yangu yalikuwa hatarini zilianza kusambaa mwezi mmoja kabla ya tukio hilo, yaani Mei mwaka 2019. Tuhuma kubwa dihidi yangu ilikuwa ni kuikosoa serikali ya Rais Magufuli kupitia kazi yangu ya uandishi wa habari. Jambo la kushangaza ni kwamba nilikuwa nafuatwa kila sehemu niliyokuwa naenda na watu wasiojulikana katika kipindi hiki chote. Nilianza kupata hofu kubwa pale nilipokuwa na mwandishi mwenzangu kwenye gari saa saba usiku tarehe 20 Mei 2024 tukitoka kumsalimia rafiki yetu aliyekuwa mgonjwa tulipokoswa koswa kupigwa risasi na kikundi cha watu mwenye magari manne eneo la Bahari Beach. Tulitoa ripoti ya tukio hilo kwenye kituo cha polisi cha Kunduchi. Tulimtambua mmojawapo ya watu waliokuwa miongoni kwa kikundi hicho ambaye aliteuleza siku iliyofuata kuwa wao walitumwa “kuwamaliza” abiria waliokuwa kwenye gari bila wao kujua watu waliokuwa ndani ya gari hilo.
Wasiwasi uliendelea kuwa mkubwa baada ya kuwasha simu tarehe 29 Juni 2019 saa tisa alasiri na kugundua kuwa haikuwa na mawasiliano. Nilifanya hivyo ili kuweza kuchukua pesa kutoka kwenye namba yangu ya simu (+255767456796) ili niweze kununulia mama yangu aliyekuwa mgonjwa dawa. Niliamua kuwapigia huduma kwa mteja ya kampuni ya VODACOM kuuliza sababu zilizopelekea simu yangu kuzimwa bila taarifa. Hata hivyo, wahudumu wa Huduma kwa Wateja walinielekeza niende kwenye Ofisi za Vodacom zilizoko jengo la Kibo Complex, eneo la Tegeta katika Wailaya ya Kinondoni kwa msaada zaidi. Baada ya kuhoji ulazima wa kufanya hivyo, nilifahamishwa kuwa laini yangu ilikuwa na tatizo la kiufundi ambalo nilihitajika kwenda kwenye ofisi zao ili waweze kulitatua.
Kauli hiyo ilinipa wasiwasi kutokana na ukweli kwamba nilikuwa nawafahamu watu zaidi ya wanne waliokuwa wamepewa maelekezo kama yangu na kampuni za simu nilitoa taarifa kwa watu vyombo vya usalama waliofika na kuwachukua watu bila hata makosa yao kujulikana. Ushirikiano usiokuwa wa kawaida kati ya vyombo vya usalama na makampuni ya simu ulinipa wasiwasi kiasi kwamba nilihisi kuwa nilikuwa nimewekewa mtengo.
Nilipopiga simu Huduma kwa Wateja mnamo tarehe 29 Julai mwaka 2019 takribani saa nne asubuhi na kulalamika kuwa nilihitaji kutoa pesa kwenye akaunti yangu, mhudumu aliyenihudumia aliomba nivumilie aongee na wakuu wake kwa kuwa jambo langu lilikuwa nyeti na anahitaji kuongea na bosi wake. Baadaye alirudi kwangu na kunishauri niende kwenye ofisini za Vodacom Mlimani City ili jambo langu liweze kutatuliwa.
Ndugu waandishi wa habari,
Ilipofika saa tisa alasiri tarehe 29 Julai 2019 simu yangu iliwashwa na kuanza kufanya kazi ghafla. Baadae nikapigiwa simu na mhudumu wa huduma za wateja aliyeniomba nimuelezee tena tatizo langu. Nilifanya hivyo lakini akakata simu baada ya dakika tatu. Muda mfupi baadae, nilipigiwa simu kutoka kwenye namba ya Vodacom Huduma kwa Wateja na sauti ya kiume ilijitambulisha kama mhudumu kutoka Huduma kwa Wateja. Alinitaka nijitambulishe na kumwambia eneo nilipokuwa. Nikapata wasiwasi na kujizuia kusema jambo lolote. Kadhalika, kulikuwa na muungurumo mkubwa sana kwenye laini na muungurumo huo uliniumiza masikio. Nilisikia pia kikundi cha watu wakibishana kwenye laini na kusema kuwa nilikuwa nyumbani kwangu na kwamba wasogee na kuzunguka nyumba yangu. Baada ya kauli hiyo nilishtuka na kuchungulia nje na kugundua kuwa nyumba yangu ilikuwa imezingirwa na watu waliovaa nguo za kiraia, wakiwa na silaha na magari kadhaa.
Niliwapigia simu majirani na vijana kadhaa wanaofanya shughuli za kuendesha pikipiki ili wafike nyumbani. Baadhi ya watu waliofika nyumbani kwangu na kuanza kuchukua video za tukio zima walitishiwa na simu zao kuchukuliwa. Baadhi yao walifanikiwa kusambaza video kwa watu mbalimbali.
Kwa kuwa kulikuwepo na kundi kubwa nje ya nyumba yangu na kampuni ya ulinzi iliyokuwa inalinda nyumba yangu ilishatuma wawakilishi wake, niliamua kutoka nje. Watu waliovaa kiraia wakiwa na mitutu walinifunga pingu na kuniweka kwenye gari. Kutokana na taarifa za kutekwa kwangu kusambaa kwa kasi, walianza kupata wasiwasi na kuamua kunihamishia kwenye gari jingine baada ya kuendeshwa kwa takribani kilomita tano kutoka nyumbani kwangu kwa kuhofia kuwa watu wangelitambua gari hilo ambalo lilikuwa limepigwa picha.
Ndugu waandishi wa habari,
Kutokana na maelezo haya, mambo mawili yako bayana.
Mosi, kampuni ya Vodacom ilihusika moja kwa moja katika kufanikisha utekaji wangu.
Pili, bila watumiaji wa mitandao yay a kijamii, vyombo vya habari kusambaza taarifa kwa kasi, ni wazi kwamba ningeweza kupotezwa na pengine kuuwawa.
KUCHELEWA KUPELEKA KESI MAHAKAMANI
Ndugu waandishi wa habari,
Kama wote mnavyofahamu, nilitoka jela nikiwa mgonjwa na nikidaiwa kiasi kikubwa cha fedha ambao nilitakiwa kulipa kabla ya kuruhusiwa kusafiri nje ya nchi kutafuta matibabu. Mazingira ya kisiasa ya wakati huo yalipelekea kupata wasiwasi kuwa pengine haikuwa salama kutafuta matibabu ndani ya nchi. Hali yangu pia iliwapa wasiwasi ndugu na marafiki wa karibu kuwa pengine nilikuwa nimepewa sumu.
Kutokana na hali hiyo kipaumbele hakikuwa kufungua kesi mahakamani bali kupata matibabu ya uhakika. Kwa macho ya kawaida, ushiriki wa Vodacom katika utekwaji wangu ulikuwa wazi lakini kisheria kuna kazi kubwa ilihitajika kufanyika. Tulihitaji kufanya uchunguzi na kupata ushahidi wote muhimu kabla ya kwenda mahakamani. Tulihitaji kushirikiana na wachunguzi mbalimbali kutoka sehemu tofauti duniani pamoja na wanasheria kuhakikisha tupata ushahidi unaoweza kukubalika mahakamani.
Kufanya uchunguzi na kukusanya ushahidi unaoweza kutumika kwenye mahakama yoyote ni jambo linalochukua muda mrefu na linahitaji ushirikiano wa watu mbalimbali.
Kadhalika, tuhuma za hivi karibuni dhidi ya kampuni moja ya simu za mikononi nchini Tanzania kuwa ilitoa taarifa zilizowasaidia watu waliojaribu kumuua Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Mheshimiwa Tundu Lissu, Septemba 2017, zinatoa mwangaza kuhusu uwepo wa tatizo la baadhi ya makampuni ya simu za mkononi kutoa taarifa za wateja wao isivyo halali, kama Vodacom walivyofanya kwangu.
UAMUZI
Hata hivyo, kabla ya kusikilizwa kwa ushahidi huo kwenye mahakama ya Tanzania, kesi yangu iliwekewa pingamizi na kushindwa kuendelea. Baada ya kushauriana na jopo la wanasheria, tumekubaliana yafuatayo.
1. Kukata rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa dhidi za pingamizi lililowekwa dhidi yangu kwa kuwa mimi na wanasheria wangu tunaamini kuwa kesi yangu ina mashiko na inastahili kusikilizwa ili tuweze kuwasilisha ushahidi wetu mbele ya mahakama ambapo tunaamini una nguvu za kuhakikisha ninatendewa haki.
2. Kutokana na ushahidi nilioukusanya na wanasheria wangu baada ya miaka mitatu ya uchunguzi, mimi na wanasheria wangu tumeona kuwa ushahidi huo ni mkubwa kiasi kwamba unatosha kuishitaki Vodacom Tanzania na kampuni zake tanzu nchini Afrika ya Kusini na Uingereza. Wanasheria wangu kutoka nchi Uingereza na Afrika ya Kusini wanakamilisha utaratibu wa kufungua kesi dhidi ya Vodacom Group South Africa na Vodafone Group PLC ambayo ina makao yake makuu nchini Uingereza haraka iwezekanavyo.
Ninawashukuru kwa kunisikiliza.
Tamko hili limetolewa leo tarehe 1 Oktoba 2024
Erick Kabendera
West Sussex, England
Video na transcript: Press Conference ya Erick Kabendera Kuhusu Kesi Yake Dhidi ya Vodacom Anayoituhumu Kuisaidia Kukamatwa Kwake